TaSUBa, Ubalozi wa India wawaibua ‘wakali’ sanaa ya uchoraji

Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) kwa kushirikiana na ubalozi wa India, umewashindanisha wanafunzi 20 katika sanaa ya uchoraji iliyobeba mada kuu ya uhusiano wa Bahari wa Hindi na tamaduni za nchi ya Tanzania na India.

Mashindano hayo yaliyofanyika kwa siku tatu chuoni hapo ambapo mshiriki alitakiwa kuonyesha uhusiano wa kiutamaduni uliopo kati ya nchi hizo na Bahari ya Hindi.

Akizungumza katika hitimisho la mashindano hayo, Naibu Mkuu wa Chuo, Taaluma ,Utafiti na Ushauri, Gabriel Kiiza amesema katika mashindano hayo wamepatikana washindi watano na kutunukia zawadi ya fedha taslimu,

“Katika mashindano hayo, wachoraji walitakiwa kuonyesha namna bahari ya Hindi inavyounganisha tamaduni mbili za watu wa India na Tanzania.

“Hivyo washindani waliweza kuchukua fikra zao uzoefu na vitu mbalimbali vinavyowasilisha watanzania na wahindi,” amesema Kiiza.

Ameeleza kuwa wanafunzi waliohusika ni kuanzia ngazi ya cheti hadi shahada  mwaka wa pili ambapo amekiri vipaji vya washiriki hao ni vizuri kwani wameweza kutafsiri kazi waliyopewa lakini kutumia vema vitendea kazi na muda waliopewa.

Kuhusu changamoto zilizopo katika sanaa ya uchoraji, Kiiza  amesema ni pamoja na upatikanaji wa rangi na brashi ambazo nyingi kwa sasa zinatoka nje ya nchi.

Hata hivyo, pamoja na changamoto hiyo, amewataka vijana kuwa wabunifu kwa kutumia vitu vinavyopatikana katika mazingira yao kwa kuwa hiyo ndio sanaa yenyewe.

Ofisa Mwandamizi Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Jalala Sammatta, akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, amesema picha walizochora vijana zinapendeza na kudhihirisha kuwa kitu wanachosomea wanakipenda.

Aidha Sammatta amesema sanaa ni maisha ya binadamu na kubwa ni uchumi, hivyo ni vema wanafuzni hao wakaandaliwa vizuri ambapo serikali kwa upande wake itaendelea kujitahidi kuwekeza hela katika tasnia hiyo.

“Pia mashindano hayo sio madogo kwani yanabeba taswira kubwa ya ushirikiano kati ya nchi ya India na Tanzania ambao umeanza miaka mingi iliyopita.

“Wito kwa watanzania kupenda vitu vya kwao vya sanaa kwa sababu wakifanya hivyo siyo tu wanaitangaza Tanzania na sanaa yake bali wanaimarisha uchumi kuanzia ngazi ya kaya,”amesema.

Mwakilishi kutoka Ubalozi wa India, Lakshay Arand, amesema mashindano hayo ni wazo kutoka kwa balozi wao kutaka kuihusisha Bahari ya India na tamaduni za nchi hizo mbili katika mambo mbalimbali ikiwemo vyakula, lugha, masuala ya ulinzi na usalama.

Arand amesema katika uwasilishaji wa michoro hiyo wanafunzi wamejitahidi kuwasilisha mawazo yao na kueleza wanafurahia namna  Tanzania imekuwa na ushirikiano wa karibu na nchi ya India katika masuala mbalimbali.

Naye Neema Labia, aliyeibuka mshindi wa kwanza katika mashindano hayo, amesema  amejisikia vizuri kwa ushindi huo ukizingatia kulikuwa na ushindani mkubwa kwa wachoraji wenzake.

Neema amesema matarajio yake baada ya kumaliza chuo ni kuifanya kazi ya sanaa kuweza kuonekana zaidi kwani baadhi kwa sasa huona kama kuifanya ni kupoteza muda.