BAADA ya makipa wawili wa Simba, Moussa Camara na Yakoub Suleiman kuumia huku wakitarajiwa kurudi uwanjani Februari 2026, kipa aliyebaki, Hussein Abel ametoa kauli ya upambanaji.
Abel ambaye hajapata nafasi ya kucheza msimu huu mechi yoyote ya mashindano ndani ya Simba, ndiye amebaki kuwa tegemeo akitarajiwa kukaa langoni katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi 2026.
Akizungumza na Mwanaspoti, Abel amesema kutokana na kukaa kwake nje muda mrefu huku akiwa amepita katika mikono ya walimu wengi, anaamini nafasi anayokwenda kuipata kuna kitu cha tofauti atakionyesha.
“Wanasimba wategemee mengi mazuri kutoka kwangu kwa sababu nimejiandaa kwa muda mrefu, nimepita katika mikono ya walimu wengi, nina imani nafasi hii ninayokwenda kuipata wataona kitu cha tofauti zaidi kutoka kwangu.
“Sisi kama wachezaji anapokuja mwalimu mpya huwa tunampokea na tunapokea kile ambacho anakuja nacho, tunafuata maelekezo yake, naamini kila mchezaji yupo tayari kuonesha kitu chake,” amesema Abel.
Kuumia kwa Camara na Yakoub, kunaifanya Simba kubaki na Abel peke yake eneo la golini, hali iliyoilazimu timu hiyo katika Kombe la Mapinduzi 2026 inayofanyika Zanzibar, kuambatana na makipa wengine wawili kutoka timu yao ya vijana.
Yakoub aliumia akiwa kambini katika mazoezi ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kabla ya kucheza mechi ya kwanza ya Kundi C ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 inayoendelea Morocco.
Kabla ya Yakoub kuumia huko, Simba ilikuwa ikimtegemea kikosini baada ya Camara kuwa nje akifanyiwa upasuaji wa goti aliloumia katika mechi ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United iliyochezwa Septemba 28, 2025.
Kwa mujibu wa ripoti ya kitabibu kutoka Simba, makipa hao wanaweza kuwa nje kwa muda mrefu kiasi cha kukosa baadhi ya mechi za makundi za Ligi ya Mabingwa Afrika timu hiyo ikiwa Kundi D pamoja na Esperance ya Tunisia, Stade Malien ya Mali na Petro Atletico.
Yakoub anatakiwa kuwa nje kwa mwezi mmoja na siku 10 wakati Camarra ilielezwa angekuwa nje kwa kati ya wiki nane hadi 10 baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti, hivyo kuwaweka wote katika hatihati ya kukosa mechi za Januari 2026 dhidi ya Esperance, ugenini Januari 23, 2026 na nyumbani Januari 30, 2026.
Baada ya hapo, Februari 2026 itacheza dhidi ya Petro na Stade Malien ambapo zilipokutana awali, Mnyama alilala zote kwa bao 1-0 na 2-1.
Wakati Abel akisalia, imeripotiwa Simba kuanza msako wa kipa mwingine wa kusaidiana naye wakati wasikilizia hali ya Yakoub na Camara.
