Dar es Salaam. Ikiwa imepita miezi sita tangu alipofariki dunia, Rais mstaafu wa Zambia, Edgar Lungu, bado mazishi yake yametawaliwa na sintofahamu kutokana na mvutano kati ya familia na Serikali ya Zambia.
Lungu alifariki dunia Juni 5, 2025 katika hospitali ya Mediclinic Mediforum mjini Pretoria, Afrika Kusini alikokuwa akipatiwa matibabu hadi alipofariki dunia, akiwa na umri wa miaka 68.
Kifo cha kiongozi huyo mstaafu kiliibua mzozo kati ya familia yake na Serikali ya Zambia kutokana na madai kwamba kifo hicho kilisababishwa na Serikali ya Rais Hakainde Hichilema, iliyokuwa ikimzuia kwenda nje ya nchi kupata matibabu.
Familia ya Lungu ilifanya uamuzi wa kumzika mpendwa wako Afrika Kusini alikofia, lakini Serikali ya Zambia iliweka zuio mahakamani ikitaka kiongozi huyo azikwe Zambia kwa heshima ya kitaifa anayostahili, kama mtu aliyewahi kuliongoza taifa hilo.
Ingawa Mahakama Kuu ya Pretoria nchini Afrika Kusini iliamuru mwili wa Lungu urejeshwe Zambia kwa mazishi ya kitaifa, familia ya Lungu ilikata rufaa dhidi ya uamuzi huo, ikidai kuwa uamuzi huo haukuzingatia matakwa ya familia.
Uamuzi huo wa familia umesababisha kucheleweshwa kwa mchakato wa kurejesha mwili, huku mazungumzo rasmi na Serikali ya Zambia yakiendelea.
Hadi sasa, mwili wa Lungu umehifadhiwa katika nyumba ya huduma za mazishi ya Two Mountains nchini Afrika Kusini.
Kutokana na kukosekana kwa maelewano baina ya pande hizo zinazovutana kuhusu mahali pa kuzikwa kiongozi huyo, jitihada nyingine zilianza kuchukuliwa nje ya mahakama ambapo Rais mstaafu wa Malawi, Dk Bakili Muluzi alianza kazi ya upatanishi.
Katika hali isiyo ya kawaida, Novemba 12, 2025, Dk Muluzi alitangaza kujiondoa katika mchakato wa upatanishi uliokuwa ukihusu maandalizi ya mazishi ya Lungu.
Uamuzi huo aliutoa kupitia taarifa rasmi, takribani miezi mitano baada ya kifo hicho.
Kwa mujibu wa jarida ya mtandaoni la Lusaka Times, Dk Muluzi alisema licha ya hatua muhimu kupigwa katika kushughulikia masuala kadhaa na kujenga uelewano baina ya pande mbili, bado kulikuwa na changamoto za kimsingi zilizozuia kufikiwa kwa mwafaka wa mwisho.
Kutokana na hali hiyo, aliona ni vema kuukabidhi mchakato huo kwa familia ya marehemu Rais Lungu, Serikali ya Zambia na wananchi wa Zambia.
“Imekuwa muhimu sasa kujiondoa katika mchakato wa upatanishi na kulirudisha suala hili kwa familia, wananchi wa Zambia, Serikali ya Zambia na taratibu nyingine husika,” amesema Dk Muluzi.
“Hatua hii itawawezesha kukamilisha maandalizi ya mazishi ya aliyekuwa Rais kwa namna watakayoona inafaa, yenye heshima na kulifikisha suala hili tamati.”
Kiongozi huyo wa zamani wa Malawi amesisitiza kuwa ushiriki wake katika mchakato huo haukuwa wa kisiasa wala wa kiitikadi, bali uliongozwa na mshikamano wa Kiafrika, heshima kwa Taasisi ya Urais na imani yake kuwa nguvu ya Afrika ipo katika umoja, hususan nyakati za misiba na changamoto.
Katika kipindi hicho cha miezi mitano iliyopita, Dk Muluzi alikuwa akitekeleza jukumu la kuwezesha upatikanaji wa suluhu ya amani na yenye staha kuhusu mazishi ya marehemu Rais Lungu.
Alieleza shukrani kwa wananchi wa Zambia kwa subira, utulivu na mshikamano waliouonyesha katika kipindi cha huzuni ya kitaifa, licha ya maumivu yaliyotokana na kumpoteza aliyekuwa mkuu wao wa mchi.
Aidha, alimshukuru Rais Hichilema kwa ushirikiano na uwazi aliouonyesha katika mchakato mzima, akibainisha kuwa utayari wake wa kushiriki mazungumzo na kusikiliza ushauri wa wapatanishi, uliwezesha kutafutwa kwa njia za uelewano na suluhu ya amani.
Vilevile, Dk Muluzi aliishukuru Serikali ya Afrika Kusini na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa pamoja na Wizara ya Uhusiano ya Kimataifa na Ushirikiano (DIRCO), kwa msaada wao wa kidiplomasia katika kipindi chote cha upatanishi.
Alipongeza pia mshikamano wa viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc), akisema walionyesha dhamira ya dhati ya ushirikiano wa kikanda na undugu katika kushughulikia suala hilo.
Kufuatia kujitoa kwa mpatanishi huyo, sintofahamu ya mazishi ya kiongozi huyo inaendelea wakati mwaka mpya wa 2026 ukianza, huku mwili huo ukifikisha miezi sita tangu mwanasiasa huyo alipofariki dunia.
Serikali imeshikilia kwamba Lungu anahitaji maziko ya kitaifa kwa kuwa alikuwa kiongozi wa nchi hiyo, hivyo hawezi kuzikwa nje ya Zambia, bali kwenye makaburi ya viongozi wastaafu, kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo.
Kwa upande mwingine, familia nayo inasisitiza kwamba inataka Lungu azikwe nje ya Zambia kwa sababu Serikali haikumjali tangu alipokuwa mgonjwa na mara kadhaa alizuiliwa kila alipojaribu kwenda nje ya nchi kutafuta matibabu.
Misimamo hii ya pande mbili zinazovutana inaonyesha kwamba maziko ya Lungu yataendelea kucheleweshwa hadi pale watakapofikia mwafaka na kukubaliana sehemu mwafaka ya kumpumzisha Lungu.
Hata hivyo, ucheleweshaji wa maziko ya kiongozi huyo wa kitaifa, ni dhahiri kwamba yanaondoa heshima yake na nchi yake kwani anahitaji kuzikwa kwa heshima kwa mazishi ya kitaifa, kutambua mchango wake kwa taifa.
Maziko ya Lungu yatamaliza sintofahamu hiyo na kuhitimisha mjadala wa muda mrefu uliogubikwa na mvutano wa pande mbili, jambo linaloipunguzia heshima taifa hilo mbele ya uso wa Jumuiya ya Kimataifa.
Mgogoro wa Lungu, Hichilema
Lungu na Hichilema walikuwa na historia ndefu ya uhasama wa kisiasa nchini Zambia, ambayo haiwezi kutenganishwa na mzozo unaoendelea sasa.
Lungu alimshinda Hichilema katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2016 na Serikali yake ilimfunga gerezani Hichilema kwa miezi minne mwaka 2017 kwa mashtaka ya uhaini, ikidaiwa msafara wake uliingilia msafara wa Rais.
Hatua ya kumfunga gerezani Hichilema ilikosoolewa na jamii ya kimataifa na Hichilema aliachiwa huru na mashtaka yalifutwa.
Baada ya Hichilema kuchukua madaraka, Lungu alimshutumu mrithi wake kwa kumwandama kwa vitendo, ikiwamo kumweka chini ya kifungo cha nyumbani.
Mwaka 2023, polisi walimzuia Lungu kutoka nyumbani kwa ajili ya mazoezi ya kukimbia, wakisema ni utendaji wa kisiasa na ilikuwa inahitaji idhini kabla, ili kuhakikisha usalama wa umma.
Kuna wakati Lungu alijaribu kurudi kwenye siasa, lakini alizuiwa kuwania tena urais katika uchaguzi. Mahakama ya Katiba ya Zambia iliamua kuwa kipindi alichokuwa Rais baada ya kifo cha aliyekuwa Rais, Michael Sata, mwaka 2015 kilihesabiwa kama muhula kamili wa kwanza.
