Unguja. Uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja la Uzi–Ng’ambwa pamoja na barabara zake umeibua matumaini mapya kwa wakazi wa visiwa vya Uzi na Ng’ambwa, ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya usafiri kutokana na kutegemea maji ya bahari kupwa na kujaa ili kuingia na kutoka visiwani humo.
Kwa muda mrefu, hali hiyo imekuwa kero kubwa kwa wananchi, hususan wajawazito wanaohitaji huduma za dharura za afya, ambapo wakati mwingine walilazimika kujifungua katika mazingira hatarishi kutokana na kukosa usafiri wakati maji ya bahari yamejaa.
Akizungumza leo Ijumaa, Januari 2, 2025, wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi wa mradi huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi, amesema ujenzi wa daraja hilo ni hatua ya kihistoria itakayobadilisha maisha ya wakazi wa visiwa hivyo.
“Mradi huu unaondoa changamoto ya muda mrefu iliyowakabili wananchi wa Uzi na Ng’ambwa. Ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya kuboresha maisha ya watu wake,” amesema Dk Mwinyi.
Rais Mwinyi amewataka wananchi kuunga mkono miradi ya maendeleo na kuepuka kuwa vikwazo vinavyoweza kuchelewesha utekelezaji wake, hususan katika suala la ulipaji wa fidia kwa waliopisha mradi huo.
Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi (kulia) akifungua kitambaa kuashiria uwekaji wa jiwe la Msingi la ujenzi wa daraja la Uzi Ng’mbwa lenye urefu wa kilometa 2.2 linalokatisha juu ya bahari katika Mkoa wa Kusini Unguja. kushoto ni Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Dk Khalid Salum Mohamed.
“Nawasihi waliobaki kuchukua fidia zao ili ujenzi wa barabara zinazounganisha daraja hili ukamilike kwa wakati. Wachache wasiwe kikwazo cha manufaa ya wengi,” amesema.
Ameagiza viongozi wa Mkoa wa Kusini Unguja kwa kushirikiana na masheha wa Shehia husika kuendelea kuwasiliana na wananchi waliobaki ili kukamilisha zoezi hilo.
Kuhusu ubora wa daraja hilo, Rais Mwinyi amesema ujenzi wake umezingatia viwango vya juu vya usalama, likiwa na urefu wa mita 4.5 kutoka usawa wa bahari, wakati maji ya bahari yanapofikia kiwango cha juu cha mita 2.5.
“Wataalamu wametuhakikishia kuwa hata bahari ikijaa zaidi, bado daraja litakuwa salama na litaweza kutumika kwa zaidi ya miaka 100,” amesema.
Akitoa taarifa ya kitaalamu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Ali Said Bakari, amesema daraja hilo lina urefu wa kilometa 2.2, likiambatana na barabara zenye urefu wa kilometa 6.5, mradi unaotekelezwa na Kampuni ya CCECC ya China.
Amesema ujenzi wa mradi huo ulianza Januari 11, 2025 na unatarajiwa kukamilika Machi 2026.
Huu ndio mwonekano wa daraja la Uzi Ng’ambwa lenye urefu wa kilometa 2.2 lililowekewa jiwe la msingi leo na Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi katika Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk Khalid Salum Mohamed, amesema serikali imeshatoa Sh2.46 bilioni kwa ajili ya fidia kwa wananchi waliopisha mradi huo, ambapo kati ya wananchi 214 waliostahili kulipwa, 168 tayari wameshalipwa.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Uzi na Ng’ambwa, Omar Mohamed amesema ujenzi wa daraja hilo ni ndoto iliyosubiriwa kwa muda mrefu.
“Ahadi zimekuwa nyingi, lakini leo tunaona utekelezaji. Daraja hili litabadilisha kabisa maisha yetu,” amesema.
Amesema mradi huo utafungua fursa mpya za kiuchumi na kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, elimu na biashara kwa wakazi wa visiwa hivyo.
