Serikali yatangaza kipaumbele cha ajira kwa vijana

Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itaweka kipaumbele katika utoaji wa ajira kwa vijana kwa kuhakikisha fursa zinazotokana na miradi ya maendeleo zinafika hadi ngazi ya shehia badala ya kubaki katika ofisi za mikoa na wilaya pekee.

Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa, Januari 2, 2025, na Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji Zanzibar, Shaaban Ali Othman, wakati wa hafla ya ufunguzi wa nyumba za wafanyakazi Pangatupu katika Hospitali ya Wilaya ya Kaskazini Unguja.

Waziri Shaaban amesema ni muhimu ajira zote zinazotolewa na Serikali zisimamiwe kwa karibu ili kuhakikisha zinawanufaisha vijana wa Zanzibar, ambao ndio walengwa wakuu wa miradi inayotekelezwa nchini.

“Ajira zinazotolewa na Serikali hazipaswi kubaki katika ngazi za juu pekee. Wananchi wanaishi kwenye shehia, hivyo ajira zinapaswa ziwafikie vijana waliopo kwenye maeneo hayo,” amesema.

Amesema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi, aliwafuata wananchi hadi kwenye shehia wakati wa kampeni za uchaguzi, hivyo ni wajibu wa Serikali kuhakikisha manufaa ya maendeleo yanawafikia wananchi huko huko walipo.

“Tumezoea kuona ajira zikibaki katika ofisi za mikoa na wizara. Sitokubali hali hiyo iendelee. Ajira hizi ni lazima ziwafikie vijana wanaochomwa na jua wakihudhuria mikutano na kuunga mkono mipango ya maendeleo,” amesema.

Ametoa wito kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kusimamia utekelezaji wa sera hiyo ili kuhakikisha vijana wananufaika na ajira zinazotokana na miradi ya Serikali, akisisitiza kuwa hiyo ndiyo roho ya Mapinduzi.

Kwa mujibu wa Waziri Shaaban, matunda ya Mapinduzi ni kumwezesha kijana wa Kizanzibari kujitegemea kiuchumi, kuhimili maisha na kuijenga kesho yake pamoja na familia yake.

Aidha, ameitaka Wizara ya Afya kuhakikisha inaajiri madaktari waliopo katika maeneo husika ili kupunguza mzigo kwa Serikali na kuboresha utoaji wa huduma, hususan nyakati za dharura.

Pia, amesema katika mpango wa Wizara ya Afya wa kuanzisha huduma za matengenezo na ukarabati wa majengo, nafasi za ajira zitolewe kwa vijana wa mikoa husika ili kusaidia kupunguza tatizo la ajira.

Ametoa rai kwa wizara zote kuzingatia uwiano wa ajira kwa watumishi wanaotoka katika maeneo ambako miradi inatekelezwa ili kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo wananufaika moja kwa moja.

Vilevile, amewataka watumishi wa afya wanaopangiwa maeneo ya kazi kuheshimu vituo walivyopangiwa na kuishi katika nyumba zinazojengwa kwa ajili yao, badala ya kuziacha bila matumizi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dk Mngereza Mzee Miraji, amesema mradi wa nyumba za wafanyakazi Pangatupu umegharimu Sh5.4 bilioni, ambapo hadi sasa Sh4.9 bilioni tayari zimeshatolewa.

Amesema nyumba hizo zitaboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi kwa kuwawezesha watumishi wa afya kuwa karibu na maeneo yao ya kazi, hivyo kupunguza changamoto za dharura.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Cassian Gallos Nyimbo, amesema utekelezaji wa miradi ya maendeleo unaonesha wazi matunda ya Mapinduzi, akisisitiza kuwa huduma za kijamii zimeimarika katika mkoa huo.