Unguja. Ujenzi wa viwanda vya nguo na dawa za binadamu katika eneo la viwanda Dunga Zuze umetajwa kuondoa gharama za uagizaji wa bidhaa hizo nje ya nchi na kuzifanya zipatikane kwa haraka na kwa bei nafuu visiwani Zanzibar.
Hayo yamebainishwa wakati wa uwekaji wa mawe ya msingi wa viwanda vya nguo (Mama Africa Textile Co Ltd) na dawa za binadamu (Africa Bio Chem Co Ltd) vyenye thamani ya Sh205 bilioni, vikitarajiwa kuajiri zaidi ya wafanyakazi 600.
Akizungumza katika hafla hiyo, Januari 2, 2026, Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff amesema sekta ya viwanda ndio nguzo ya uchumi maana bidhaa zake ndio zinatoka nchi moja kwenda nyingine.
“Tunataka kuondosha kuagiza bidhaa za viwanda kutoka nje ya nchi, kwa mantiki hiyo, Serikali inaweka mazingira mazuri kushawishi uwekezaji zaidi,” amesema Shariff.
Hata hivyo, ametumia fursa hiyo kuiagiza Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji (Zipa) kuhakikisha wawekezaji waliochukua maeneo hayo kama hawayaendelezi wanyang’anywe na wapewe wawekezaji wenye nia ya kweli kuwekeza.
“Serikali haipo tayari kuchezewa, ninaagiza waliochukua muda mrefu bila kuendeleza maeneo wafutiwe hati zao,” amesema.
Pia, amesema lazima wawekezaji wanaowekeza wazingatie sheria ya uwekezaji Namba 10 ya mwaka 2023 ambayo inataka asilimia 90 za ajira wawe wazawa na zingine 10 ndio ziwe za wageni.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Dk Habiba Hassan Omar amesema eneo la viwanda Dunga Zuze Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja ni moja kati ya maeneo yanayoendelezwa na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda likiwa na ukubwa wa ekari 61.83.
Tayari serikali imekamilisha ujenzi wa miundombinu ya barabara yenye urefu wa kilometa 7.83 uliotekelezwa na kampuni ya China ya CCECC kwa gharama ya Sh23.367 bilioni.
Mradi mwingine ni ujenzi wa tanki la maji lenye ujazo wa lita milioni moja, uchimbaji wa visima vitatu na usambazaji wa mabomba ya maji katika eneo lote la viwanda ambayo imegharimu Sh3.467 bilioni.
Amesema kwa mwaka 2025/26, Wizara imepanga kuendeleza mitaa ya viwanda kwa kutekeleza miradi mingine ya ujenzi wa ukuta na na mabanda ya viwanda ambapo tayari wizara imeshasaini mkataba na kampuni ya CCECC kwa gharama ya Sh32.748 bilioni.
“Kukamilika kwa viwanda hivi kunatarajia kuzalisha ajira zaidi ya 600 kwa wananchi wa Zanzibar, jumla ya wawekezaji 12 wamepatiwa maeneo ndani ya eneo la viwanda kati ya hao wawekezaji watano, wamepatiwa mikataba ya ukodishwaji na wengine saba wamepatiwa barua za dhamira,” amesema.
Bidhaa mbalimbali zitazalishwa kupitia miradi hii vikiwemo vifaa vya umeme, ujenzi, nguo, dawa za binadamu, vyuma, plastiki, aluminium, mbao na chuma.
Amesema jumla ya viwanda sita vimeanza ujenzi, viwanda vitatu vimewekewa mawe ya msingi na vingine vipo hatua za awali za ujenzi. Kwa ujumla miradi hiyo inagharimu Sh205 bilioni.
Katibu Mkuu amesema kwa sasa wamebadili mfumo wa ukodishaji wa maeneo hayo, wanatoa barua ya mkataba mpaka wafikie asilimia 20 ya uwekezaji kwa kipindi cha miezi mitatu baada ya hapo ndio wanapewa mkataba wa ukodishwaji na anayeshindwa ndani ya muda huo ananyang’anywa.
Meneja wa Kiwanda cha Mama Africa Textile Co Ltd, Rashid Salim amesema ushirikiano wanaoupata kutoka wizarani umewapa hamasa ya kuendelea kuwekeza Zanzibar.
Amesema kiwanda hicho kitajihusisha na uzalishaji wa kanga na batiki hivyo kupunguza gharama za uingizaji wa bidhaa hizo.
Hata hivyo, ameiomba Serikali kuangalia namna bora ya kushughulikia changamoto zinazojitokeza ikiwemo utaratibu wa usafirishaji wa bidhaa hizo kwenda Tanzania Bara, Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc).
“Bidhaa zinazozalishwa zifanyiwe ukaguzi haraka ili kutoa fursa za kupeleka bidhaa hizo sokoni jambo ambalo litaongeza mnyororo wa thamani,” amesema Salim.
Naye Mtendaji Mkuu wa kiwanda cha Africa Bio Chem, Du Gongming amesema Afrika kwa sasa inaingiza kati ya asilimia 90 na 99 ya bidhaa zake za dawa. Utegemezi huu unazifanya dawa za kuokoa maisha kuwa ghali na muda wa utoaji usiweze kukubalika.
“Sasa kwa kutengeneza hapa hapa Zanzibar, itarahisisha sana upatikanaji wa wa dawa na kuokoa maisha ya watu kwani kuna wakati mwingine mgonjwa anaweza kupoteza maisha kwa kukosa dawa,” amesema Gongming.
Pia, amesema uzalishaji utakaofanyika utapunguza gharama kwa takibu 30 kwa kuondoa usafirishaji mzito na ushuru wa uagizaji.
Ametaja dhamira ya kuwekeza Zanzibar imetokana na ahadi ya serikali ya kutoa miundombinu ya kimataifa kutoka barabara za lami hadi mifumo mikubwa ya usambazaji wa maji iliyokamilika hivi karibuni katika eneo hilo imeunda mazingira bora kwa uwekezaji wa dawa za hali ya juu.
“Miundombinu hii inatuwezesha kuleta teknolojia ya kibayoteki ya kisasa Zanzibar, kuhakikisha kwamba Zanzibar inakuwa kitovu cha uvumbuzi wa matibabu katika eneo la Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara,” amesema.
