Mbeya. Wananchi wa kata za Itewe, Igoma na Ulenje, Wilaya ya Mbeya Vijijini, wamemwomba Mbunge wao, Patali Shida, kuingilia kati changamoto ya ubovu wa barabara wakisema imekuwa kikwazo kwa shughuli za kiuchumi na upatikanaji wa huduma za kijamii.
Kilio hicho kimetolewa leo Ijumaa Januari 2, 2026, katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwa pamoja katika kata hizo tatu, ikiwa ni sehemu ya ziara ya mbunge huyo ya kusikiliza kero za wananchi na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Wananchi wamesema barabara hizo ni kiungo muhimu cha shughuli za kiuchumi baina ya kata hizo, lakini kwa muda mrefu zimekuwa katika hali mbovu, hali inayokwamisha usafirishaji wa mazao kwenda sokoni, kuwafikia wagonjwa kwa wakati pamoja na watoto kuchelewa au kushindwa kuhudhuria masomo.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Sekela Solomon amesema wanatambua jitihada za mbunge wao na kumuomba afikishe kilio hicho kwa mamlaka husika ili kipatiwe ufumbuzi wa kudumu.
“Tunaomba msaada wako. Hizi barabara ni kero ya muda mrefu. Tunakwama kusafirisha mazao, kuwapeleka wagonjwa hospitalini kwa wakati, wakiwemo akina mama wajawazito,” amesema.
Mbunge wa Mbeya vijijini, Patali Shida akizungumza na wasimamizi wa mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Ulenje ambachimo Serikali. Picha na Hawa Mathias
Amesema licha ya wananchi wengi kujihusisha na kilimo, changamoto ya barabara duni imekuwa ikipunguza tija ya shughuli zao kutokana na ugumu wa kufikisha mazao sokoni.
Kwa upande wao, madiwani wa kata hizo wamekiri kuwapo kwa changamoto hiyo kwa muda mrefu licha ya kuifikisha mara kadhaa katika vikao mbalimbali vya halmashauri.
Diwani wa Kata ya Ulenje, Laurent Isote, amesema ziara ya mbunge ni fursa ya mwisho ya wananchi kupata suluhu ya kudumu.
“Barabara hii imelalamikiwa kwa kipindi kirefu. Tunaomba sauti ya wananchi hawa ifikishwe kwa mamlaka husika ili hatua zichukuliwe,” amesema.
Akizungumza katika mkutano huo, Mbunge Shida, amesema ziara yake inalenga kusikiliza kero za wananchi na kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi kwa kushirikiana na taasisi husika.
Ameitaka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuchukua hatua za haraka kutengeneza maeneo yaliyoathirika, akisisitiza Serikali tayari imetoa fedha kwa ajili ya matengenezo ya barabara hizo.
“Hakuna sababu ya kuchelewesha utekelezaji. Serikali imetoa fedha, hivyo matengenezo yafanyike kwa wakati,” amesema.
Katika hatua nyingine, Patali amekagua ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Ulenje kinachojengwa kwa zaidi ya Sh600 milioni, akisema lengo ni kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.
Amepongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha miundombinu ya barabara, afya, elimu na maji, huku akiwataka wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi hizo.
Pia, amewataka wakandarasi kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa viwango vinavyolingana na thamani ya fedha za umma.
“Nitaendelea kufuatilia kwa karibu miradi yote ya maendeleo ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaostahili,” amesema.
