SIMBA inaendelea kuhusishwa kuwapigia hesabu makipa wawili wazawa, Yona Amos wa Pamba Jiji na Patrick Munthary wa Mashujaa ili kuongeza nguvu ikiwa na pengo la Moussa Camara na Yakoub Suleiman ambao ni majeruhi wanaodaiwa watakuwa nje kwa muda mrefu.
Hata hivyo, makipa hao nao wameibuka na yao, ikielezwa ni ngumu kwa Munthary sasa kutua Msimbazi kwa sababu hawezi kuvua magwanda ya jeshi Mashujaa, huku Amos akidai kila kitu kipo kwa mabosi wa Pamba Jiji kama kuna dili la kutakiwa na Simba.
Amos aliyemaliza na ‘clean sheets’ 11 katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita, amesema simu aliyopigiwa ni ile ya kurejea kambini, lakini mengine kama yapo viongozi wa Simba watawafuata waajiri wake.
“Simu niliyopokea ni kwenda kujiunga na wenzangu katika mazoezi ya timu yaliyoanza Jumatano. Kuhusu kuhusishwa na Simba kama hilo lipo, basi watakwenda kuzungumza na mabosi wangu,” amesema Amos.
“Mimi ni mchezaji naweza nikacheza popote, lakini jambo la msingi ni utaratibu, ndiyo maana nasisitiza kama hilo litakuwepo viongozi wa Pamba ndiyo wenye mamlaka kutokana na mkataba nilionao.”
Jambo lingine alilolizungumzia Amos ni namna kitaani kwake Tukuyu, Mbeya alivyokuwa anachukuliwa na watu kuwa ana pesa nyingi baada ya kuona taarifa za kuhusishwa na klabu hiyo kongwe.
“Unakutana na mtu anakwambia mwanangu saizi una pesa ya kutosha, hizo Simba na Yanga zinazokutaka zitakuwa zimekupa kibunda cha maana. Nilikuwa naishia kucheka tu, kwani ngumu watu kuelewa mambo ya mpira yanaendaje.”
Kipa huyo aliwahi kuhusishwa pia na Yanga wakati akiitumikia Tanzania Prisons kabla ya kuibukia Pamba Jiji na Yanga kumbeba aliyekuwa kipa wa Singida Black Stars, Abukabar Khomein.
Kwa upande wa Munthary aliyemaliza na clean sheets 14 msimu uliopita, amesema: “Siwezi kuzungumzia suala hilo labda uniulize maandalizi baada ya kurejea kambini, nje na hapo utanisamehe.”
Chanzo kutoka ndani ya Simba kinadai imekuwa ngumu kumpata Munthary kwa sababu ni mwanajeshi, hivyo sio rahisi kuinasa saini yake bila kuzingatia taratibu za kijeshi.
Ilikuwa rahisi kufanya mazungumzo ya kimkataba wa kisoka kwa miezi sita iliyosalia, lakini kwa mchakato wa kijeshi inachukua muda.
Kuhusu Amos aliyebakiza mkataba wa miezi mitano na timu yake bado tunaendelea kulifanyia kazi suala lake,” kilisema chanzo kutoka Simba kilichothibitisha kuwa ni kweli Simba inataka kipa mzawa kuziba nafasi ya Yakoub atakayekuwa nje kwa zaidi ya mwezi mmoja pamoja na mwingine wa kigeni wa nafasi ya Camara.
Rafiki wa karibu wa Munthary amesema: “Msimu uliopita Azam FC na Yanga ziliwahi kuhitaji huduma yake, lakini zilikwama kutokana na taratibu za kijeshi. Huyu jamaa ni askari kama hujui ni ngumu kutoka Mashujaa kirahisi.”
Wakati hilo likiendelea aliyekuwa kipa na kocha wa makipa wa Simba, Idd Pazi ‘Father’ amesema: “Japo Simba inatafuta kipa ni vizuri wangemjengea Hussein Abel kujiamini kwa kumpa nafasi ya kudaka. Ni kipa mzuri ila anakosa kujiamini kwa sababu hachezi mara kwa mara.”
Abel ni mmoja ya wachezaji walioenda na timu katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026, michuano iliyompaisha alipokuwa Taifa Jang’ombe kiasi cha Prisons kumsajili kabla ya kupita KMC na sasa Simba.
