Polisi Waendelea na Uchunguzi Ajali ya Lori Morogoro – Video


Polisi Mkoa wa Morogoro limetoa taarifa kwa umma kuwa linaendelea na uchunguzi wa ajali mbaya ya barabarani iliyotokea Desemba 31, 2025, majira ya jioni katika Kijiji cha Maseyu, Kata ya Gwata, Wilaya ya Morogoro, mkoani Morogoro, ambayo ilisababisha vifo vya watu 10 na majeruhi 18.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, ajali hiyo ilihusisha magari mawili yaliyogongana uso kwa uso na baadaye kuwaka moto.

Magari hayo ni lori aina ya Mitsubishi Fuso lenye namba ya usajili T.162 DMD mali ya Kampuni ya Bill Mawio, na lori la mizigo aina ya HOWO lenye namba T.956 ELU pamoja na tela T.828 ELW mali ya Kikori Company Ltd.

Gari hilo lilikuwa likisafirisha mbolea kutoka Dar es Salaam kuelekea Mbeya.

Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa lori aliyepoteza mwelekeo na kuingia upande wa kushoto wakati wa kupita magari mengine bila kuchukua tahadhari, huku kukiwa na mvua kubwa.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa majeruhi 18 wamekimbizwa hospitalini kwa matibabu, wakiwemo wanaume 9, wanawake 9 na watoto 5. Kati yao, majeruhi 6 wamepata majeraha makubwa.

Miili ya marehemu bado haijatambuliwa kutokana na kuungua vibaya.

Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina wa tukio hilo huku likitoa wito kwa madereva wote kuzingatia sheria za usalama barabarani, hasa katika kipindi cha mvua, ili kuepuka ajali zinazoweza kuzuilika.