Uteuzi wa kamati waivuruga Chadema Kanda ya Nyasa

Dar es Salaam. Uteuzi wa wenyeviti na makatibu wa kamati za kudumu za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Nyasa umeibua mvutano miongoni mwa viongozi wa kanda hiyo.

Januari Mosi, 2026, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi alifanya uteuzi wa makatibu na wenyeviti wa kamati za kudumu za kanda hiyo, jambo linalopingwa na wajumbe wa kamati ya utendaji wa kanda hiyo wakidai kwamba utaratibu haujafuatwa.

Wajumbe hao (hawakutaka kutajwa majina) wamesema uteuzi huo ulifuata hatua moja tu ya kutangazwa, lakini mchakato wa sekretarieti ya kanda kupokea na kupendekeza kwa kamati tendaji ya kanda majina ya waombaji haukufanyika.

Pia, wajumbe hao wamedai kuwa hata mchakato wa kamati utendaji kupokea mapendekezo ya sekretarieti na kuleta majina ya wajumbe na makatibu wa kamati, haukufutwa.

Mbali na hilo, wameeleza kuwa mchakato wa wajumbe wa kila kamati kuchagua mwenyekiti wa kamati na baraza la uongozi la kanda kuthibitisha majina ya mwenyekiti na katibu wa kila kamati, pia, haukufuatwa.

Kutokana na hilo, mmoja wajumbe hao, ameidokeza Mwananchi kuwa wamewasilisha malalamiko yao katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa chama hicho ili kufanyiwa kazi na kuondoa sintofahamu iliyoibua mvutano wa pande hizo mbili.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Sugu jana Januari Mosi, 2026, iliwataja viongozi walioteuliwa kuwa ni Fanuel Siame (mwenyekiti wa kamati ya fedha) na katibu wake ni Angumbwike Ntuli, kamati ya ilani itaongozwa na Leonard Fumbo na Elijah Simbeye (katibu).

Taarifa iliyo ilieleza kuwa kamati ya mafunzo itaongozwa na Frank Nkana (mwenyekiti) na Emily Mwakilembe (katibu), kamati ya wagombea, Obadia Mwaipalu (mwenyekiti) na Neema Kasinge (katibu), kamati ya ujenzi, Bruce Nyamwangi (mwenyekiti) na Frank Kifunda (katibu).

Wengine ni kamati ya Tehama mwenyekiti ni Daniel Naftari na Fikiri Zambi (katibu), kamati ya sheria na haki ya binadamu, mwenyekiti ni Fredrick Kihwelo na Irene Mhando (katibu) wakati kamati ya Chadema msingi itaongozwa na Pascal Haonga (mwenyekiti).

Alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia uteuzi huo na madai ya viongozi wengine wanaopinga, Sugu hakuweza kupokea simu yake kwani iliita bila kupokelewa, na hata alipotumiwa ujumbe mfupi, hakujibu.

Hata hivyo, Mwananchi lilimtafuta katibu wa kanda hiyo, Grace Shio ambaye alisema uteuzi huo ulifuata utaratibu na miongozo ya chama hicho.

“Hata hao wanaolalamika, madai yao hayana uhalisia wanajua hilo. Tumefuata hatua zote,” amesisitiza Shio.

Mmoja wa vigogo wa kanda hiyo (jina limehifadhiwa), ameliambia Mwananchi kuwa utaratibu wa kuwapata viongozi hao haukufuatwa, akieleza kwamba kwa mujibu wa mwongozo, uundaji wa kamati hizo utaanzia ofisi ya katibu wa kanda, anayetoa tangazo kwa wanachama kuhusu suala hilo.

“Wanachama wenye sifa watatuma maombi yao katika ofisi ya katibu wa kanda. Mara baada ya maombi kupokelewa, kamati ya viongozi wakuu wa kanda itachambua majina na kuyapanga kwa mujibu wa sifa za kila mwombaji dhidi ya kazi husika za kamati.

“Baada ya hapo kamati ya uongozi itapanga majina ya kamati kulingana na sifa za kila mwombaji na kazi za kamati na sio lazima mwombaji awekwe katika kamati aliyoomba iwapo ataonekana kuwa na nafasi ya kutoa mchango zaidi katika kamati nyingine ambayo hajaiomba,” amesema.

Aidha, kigogo huyo anaeleza kuwa kamati hiyo, pia, inaweza kuongeza au kuteua wajumbe nje ya waombaji ili kuziongezea thamani na kuleta tija kwa masilahi ya chama.

“Itakapomaliza kazi ya kutengeneza mapendekezo ya kamati hizo, kamati ya viongozi wakuu itawasilisha mapendekezo yake kwa kamati ya utendaji ya kanda itakayochakata na kutoa mapendekezo yake.

“Baada ya kuwapendekeza na kuwajulisha wajumbe hao, utaratibu unataka wapangiwa tarehe ya kukutana ili kuchaguana. Uchaguzi wa mwenyekiti ukifanyika, majina yatarudishwa kamati ya utendaji yenye wajibu kuchagua katibu,” amesema.

Naibu katibu mkuu atia neno

Wakati hayo yakijiri, Naibu Katibu Mkuu Chadema (Bara), Amani Golugwa amesema kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, kamati za utendaji za kanda zina mamlaka ya kufanya mapendekezo baada ya wanachama kuomba nafasi mbalimbali, kisha kuyapeleka katika baraza la uongozi.

“Wajibu huo hauwezi kuingiliwa na chombo chochote, lakini iwapo kuna malalamiko basi ofisi ya katibu mkuu itayafanyia kazi. Tutahitaji kamati ya utendaji ya kanda itupe taarifa za mchakato ulivyokwenda, je, ulifuata utaratibu na kanuni?

“Tukishaipokea na kujiridhisha kila kitu kimekaa sawa, tutafafanua pale panahitaji ufafanuzi. Kama kuna makosa ya kuvunjia Katiba na kanuni, tutasaidia hizo mamlaka zitimize matakwa ya kikatiba,” amesema Golugwa.

Alipoulizwa kama ameshaipokea barua za malalamiko, Golugwa amesema: “Nitafuatilia hizo barua ili kuzifanyia kazi maana hapa katikati kulikuwa na sikukuuu.”