Straika aipa mechi tano Transit Camp

STAA wa Transit Camp, Adam Uledi amesema licha ya kuongoza katika Ligi ya Championship kwa idadi ya mabao, lakini matokeo waliyonayo hayaendani na mahitaji akizitaja mechi tano tu zitakawapa mwanga maafande hao kupanda Ligi Kuu Bara.

Nyota huyo aliyewahi kung’ara akiwa Ken Gold kwa misimu miwili akiwa kinara wa mabao kikosini, ameendelea kuonyesha makali mbele ya wengine kwenye Championship kwa mabao tisa.

Hadi jana Transit Camp ilikuwa katika nafasi ya nne ikiwa na pointi 27 na ilitarajiwa kuwa uwanjani kuwakaribisha Hausung ya mkoani Njombe katika mwendelezo wa ligi hiyo kabla ya kuwafuata Mbuni, kisha kuwapokea Ken Gold na kuhitimisha mzunguko wa kwanza.

Akizungumza na Mwanaspoti, Uledi aliema licha ya juhudi anazoonyesha na mafanikio aliyonayo kuongoza ligi kwenye utupiaji mabao, lakini hajaridhishwa na matokeo ya timu kwa nafasi waliyopo.

Amesema kwa sasa mipango ya wachezaji ni kupamana ili kuwa nafasi mbili za juu kwa kuwa wanapigia hesabu mechi tano (sawa na pointi 15) ambazo zitawapa mwanga wa kujua hatma yao.

“Walio juu yetu (Geita Gold na Kagera Sugar) wanatuzidi pointi tatu, ambapo kwa mechi tatu za kumaliza raundi ya kwanza tunamleta Hausung (jana), tunatoka dhidi ya Mbuni kisha kumkabili Ken Gold.

“Baada ya hapo wanakuja hao vigogo nyumbani tukianza na Kagera Sugar kisha Geita Gold ambapo kwa hesabu zetu tukitoboa hapo tunaweza kujiona kwenye nafasi tunazotaka. Tunahitaji kupanda moja kwa moja na si vinginevyo,” amesema Uledi.

Nyota huyo alidai ligi ni ngumu na hata kwenye ufungaji mabao vita siyo rahisi kwa kuwa mkakati wake ni kuendelea kufumania nyavu kadri anavyopata nafasi.

Hadi jana staa alikuwa akiongoza kwa utupiaji nyavuni akiwa na mabao tisa akifuatiwa na nyota wa Mbeya Kwanza, Boniface Brown (manane) sawa na Abdereheman Mussa (Gunners), huku Obrey Chirwa (Kagera Sugar) na Raymond Lulendi wa Songea United wakiwa na saba.