BINGWA mara mbili wa Kombe la Mapinduzi na bingwa wa kihistoria katika Ligi Kuu Bara, Yanga SC, leo Jumapili inatupa karata yake ya kwanza dhidi ya KVZ.
Hiyo itakuwa saa 10:15 jioni katika mechi ya kundi C kwenye michuano ya Mapinduzi Cup 2026 inayochezwa Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja.
Yanga ikiwa inaanza kutupa karata yake katika Mapinduzi Cup, mechi ya leo haitakiwi kukosa pointi tatu kwani ikifungwa tu, safari yao inaishia hapohapo bila ya kusubiri mechi ya mwisho dhidi ya TRA United itakayochezwa Januari 6, 2026.
Kwa sasa, kundi C Yanga ikiwa haijacheza mechi yoyote, TRA United na KVZ zina pointi moja kutokana na sare waliyoipata zilipokutana. Kumbuka kundi hili timu moja ndiyo inafuzu nusu fainali.
Ikitokea KVZ imepata ushindi leo, itafikisha pointi nne ambazo Yanga haiwezi kuzifikia hata ikishinda mechi ya mwisho dhidi ya TRA United kwani itamaliza na pointi tatu.
Lakini kama Yanga itashinda leo, basi itahitaji sare tu mechi dhidi ya TRA na kumaliza kinara wa kundi na kufuzu nusu fainali.
Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves tayari ameweka malengo ya kufanya vizuri katika michuano hii na kuongeza mataji ya Mapinduzi katika kabati la klabu hiyo baada ya kubeba 2007 na 2021.
Kwa upande wa KVZ, kocha msaidizi wa KVZ, Ali Khalid Omar, amesema hii ni mechi ya uamuzi kwao, hivyo hawana budi kupambana kuonyesha uwezo wao licha ya kukutana na timu kongwe na yenye historia kubwa kama Yanga.
TAIFA STARS YAPEWA HESHIMA
Wakati ratiba ya michuano ya Mapinduzi Cup inapangwa, kamati ya maandalizi iliipa heshima timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inayoshiriki Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2025) zinazoendelea nchini Morocco.
Mapinduzi Cup ilipoanza Desemba 28, 2025, Taifa Stars ilikuwa tayari imeshuka dimbani huko Morocco mara mbili, Desemba 23, 2025 dhidi ya Nigeria na Desemba 27, 2025 dhidi ya Uganda. Mechi iliyofuata ilikuwa Desemba 30, 2025 dhidi ya Tunisia.
Siku ambayo Taifa Stars inacheza dhidi ya Tunisia, hakukuwa na mechi ya Mapinduzi Cup, badala yake siku hiyo ilitengwa maalum kwa ajili ya kuwapa fursa Watanzania kushuhudia mubashara kupitia runinga.
Hata hivyo, matarajio ya wengi ilikuwa Taifa Stars itaishia makundi, lakini imetoboa 16 bora na leo inacheza dhidi ya mwenyeji, Morocco.
Kufuzu kwa Taifa Stars hatua ya 16 bora, kamati ya maandalizi ya Mapinduzi Cup 2026 imesema ratiba ya mechi ya leo kati ya Yanga dhidi ya KVZ imebadilishwa muda kutoka saa 2:15 usiku hadi saa 10:15 jioni.
Uamuzi huo umekuja kufuatia Taifa Stars leo inacheza na Morocco saa 1:00 usiku, hivyo kamati hiyo imetoa nafasi kwa Watanzania kulishuhudia chama lao, lakini pia kushuhudia mechi ya Yanga vs KVZ kwa utulivu.
