LEO usiku kikosi cha Simba kitakuwa Uwanja wa New Amaan Complex hapa Unguja kucheza mechi ya kwanza ya Mapinduzi Cup 2026 dhidi ya Muembe Makumbi City, lakini kocha mkuu wa timu hiyo, Steve Barker, amekuwa na jambo lake kimkakati ambalo ndani ya wiki tatu anataka kila kitu kiwe fresh.
Barker ambaye alitambulishwa kuwa kocha mkuu wa Simba Desemba 19, 2025 akichukua nafasi ya Dimitar Pantve, anataka kabla ya kuivaa Esperance, kikosi chake kiwe tayari kwa mapambano na si vinginevyo.
Katika kufanikisha hilo, Barker raia wa Afrika Kusini, anaitumikia michuano ya Mapinduzi Cup kujenga kikosi imara lakini pia kuwasoma wachezaji wake kuona udhaifu ulipo, kisha kufanya uamuzi mgumu wa kuongeza nguvu kwa kusajili majembe mapya mapema na kuwapiga panga atakaoona hawafai.
Taarifa kutoka katika kambi ya Simba iliyopo Unguja, zinasema Barker amezungumza na uongozi akitaka wale nyota wote ambao hawakuwa na majukumu timu za taifa katika Fainali za AFCON 2025 wawe wameungana na wenzao wikiendi hii.
Chanzo cha taarifa kimesema, Barker anataka wiki inayoanza kesho Jumatatu, angalau awe na majembe yake kwa asilimia kubwa ili atakapowafanyia tathmini afahamu haraka wapi kuna upungufu na kufanya uamuzi.
“Tangu tumefika Unguja kocha anaonekana kuhitaji zaidi kutumia hizi wiki tatu kabla ya kucheza na Esperance kujenga kikosi imara.
“Uwepo wa mashindano ya Mapinduzi ni sehemu ya kukiangalia kikosi chake, licha ya kwamba baadhi ya nyota wanakosekana kutokana na kwenda AFCON, lakini ameagiza wale waliokwenda mapumziko warudi fasta na waungane na wenzao.
“Katika kipindi hicho cha wiki tatu, ndipo atajenga kikosi chake cha kumalizia msimu kwa maana ya kutumia mwanya uliopo wa dirisha hili dogo kuongeza majembe na kuondoa anaoona hawafai,” kimesema chanzo.
Chanzo hicho kimeongeza kuwa, katika Mapinduzi, kutakuwa na wachezaji wanaofanyiwa majaribio, wakifaa wanapewa mkataba.
Simba iliyopo kundi B katika Mapinduzi Cup, jana baada ya kumalizana na Muembe Makumbi, Jumatatu itacheza dhidi ya Fufuni kukamilisha hatua ya makundi.
Baada ya kumaliza mashindano haya, Januari 23, 2026 itakuwa Tunisia kucheza na Esperance, kabla ya wiki moja baadaye kurudiana jijini Dar ikiwa ni mechi za kundi D katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Barker anafahamu ana mtihani mgumu mbele katika Ligi ya Mabingwa kutokana na Simba kupoteza mechi mbili za kwanza hatua ya makundi ikifungwa 1-0 nyumbani na Petro Atletico, kisha ikachapwa 2-1 ugenini na Stade Malien. Inaburuza mkia wa kundi hilo bila ya pointi.
“Tumekuja kushiriki Mapinduzi Cup kwa ajili ya kutoa ushindani, lakini pia kushinda ubingwa. Pia natumia michuano hii kuwafahamu vizuri wachezaji wangu.
“Ni nafasi nzuri kwangu kuja na kukutana na mashindano haya ambayo yatanisaidia kwa kiasi kikubwa kujenga timu na kujiandaa na mashindano mengine yanayotukabili hasa Ligi ya Mabingwa.
“Katika uwanja wa mazoezi tunapambana kujenga timu kuwa imara na tayari kwa mapambano kabla ya kucheza mechi ijayo ya Ligi ya Mabingwa,” amesema Barker.
Kwa upande wa mratibu wa Simba, Abas Ally, amesema: “Kuna baadhi ya wachezaji wetu tunawakosa kwa sababu wapo timu za taifa katika AFCON lakini kuna baadhi walikuwa wamesafiri kwa ajili ya hii likizo na watawasili hapa Zanzibar kuungana na wenzao.
“Lakini wengine asilimia 80 tumesafiri nao kuja Zanzibar na wapo tayari, wengi wao ni mara ya kwanza kuja kushiriki mashindano haya lakini tumewaambia ni mashindano makubwa yenye historia kubwa na yanaheshimika katika nchi yetu.” Katika kikosi cha Simba kilichopo Unguja, wanakosekana Shomari Kapombe, Kibu Denis, Yusuph Kagoma na Morice Abraham wanaoshiriki AFCON wakiwa na Taifa Stars. Steven Mukwala naye alikuwa AFCON lakini chama lake Uganda limeishia makundi, hivyo ana mapumziko ya muda kabla ya kurejea nchini kuungana na wenzake.
Yakoub Suleiman alikuwa na Stars huko AFCON, lakini majeraha aliyopata yamemlazimu kupelekwa kutibiwa kama ambavyo Moussa Camara akiendelea kuuguza majeraha ya goti.
Jean Charles Ahoua, Elie Mpanzu na Jonathan Sowah, wamechelewa kurudi kutokana na likizo fupi waliyopewa lakini muda wowote watakuwa Unguja.
