Wananchi wa vijiji vitano Pangani wataka kulipwa fidia mapema

Tanga. Wananchi wa vijiji vitano Wilaya ya Pangani, mkoani Tanga, wanatarajiwa kuondoka katika makazi yao kupisha utekelezaji wa mradi mkubwa wa uchimbaji wa madini ya Tembo (heavy minerals), baada ya kukamilika kwa utaratibu wa ulipaji wa fidia.

Vijiji vinavyohusika katika mradi huo ni Stahabu, Bweni, Mzambarauni, Mikinguni na Mwera, ambapo maeneo hayo yamegundulika kuwa na rasilimali za madini hayo.

Wakizungumza na Mwananchi jana Januari 2, baadhi ya wananchi wamesema tayari wamefanyiwa tathmini ya mali zao na sasa wanahitaji fidia ilipwe haraka ili waweze kutafuta maeneo mbadala ya makazi.

Mkazi wa Kijiji cha Mzambarauni, Ramadhan Mdoe amesema wameelekezwa kutofanya shughuli zozote za maendeleo katika maeneo yao baada ya tathmini kukamilika.

“Tumeshaambiwa hatupaswi kuendelea kujenga au kuendeleza chochote. Kuendelea kubaki hapa bila kulipwa fidia ni kupoteza muda,” amesema Mdoe.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mzambarauni, Idd Yakobo amesema kinachosubiriwa kwa sasa ni kuwasili kwa Mthamini Mkuu wa Serikali ili kuanza rasmi kwa zoezi la ulipaji wa fidia.

Yakobo amesema ni muhimu Serikali na mwekezaji kuweka mpango wa kuwasaidia wananchi kupata maeneo mapya ya makazi baada ya kulipwa fidia, ili kupunguza changamoto za kuhamia maeneo mengine.

Naye mkazi wa Kijiji cha Mwera,  Shehe Mwinchumu Ibrahimu amesema mchakato wa kuachia maeneo yao ulianza toka mwka 2023 na kwamba wanachotaka ni fidia  au maandishi ya kuendelea kwenye maeneo yao.

“Tulipewa taarifa za kutoendeleza maeneo yetu sasa tunavyokaa kimya muda mrefu tunakosa imani ,” alisema Shehe Mwimchumu ambaye anamiliki mashamba mawili katika eneo la Mzambarauni na Mikingumi.

Naye mkazi wa Kijiji cha Bweni, Alifa Hemedi amesema maeneo wanayoishi sasa yamekuwa mapori ambayo wadudu kama nyoka wanaishi akitolea mfano mtoto wa familia yake ambaye alinusurika kugongwa na nyoka.  

Akizungumza kwa niaba ya Kampuni ya Nyati, Mhandisi Heri Gombera, amesema tayari kampuni hiyo imeanza kulipa fidia katika Kijiji cha Stahabu kiasi cha Sh3 bilioni.

Ameeleza kuwa jumla ya Sh35 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi wa vijiji vyote vitano vinavyohusika na mradi huo.

“Fedha za fidia zipo tayari. Tunachosubiri ni idhini ya Mthamini Mkuu wa Serikali ili kuendelea na ulipaji kwa wananchi waliobaki,” amesema Gombera.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk Batilda Burian, amewahakikishia wananchi kuwa kila mmoja atalipwa fidia stahiki kwa mujibu wa tathmini iliyofanyika.

Amesisitiza umuhimu wa Mthamini Mkuu wa Serikali kukamilisha taratibu zake kwa wakati ili zoezi la fidia liendelee bila kucheleweshwa.