Geita. Wakati wananchi wakiendelea kusherehekea sikukuu ya Mwaka Mpya, moto unaodhaniwa kusababishwa na hitilafu ya umeme umetekeza sehemu ya eneo maarufu la starehe la Suzy Bar and Lounge katika mji mdogo wa Katoro, mkoani Geita.
Moto huo ulizuka majira ya saa 6:15 mchana, Ijumaa Januari 2, 2026, wakati shughuli zikiendelea katika eneo hilo.
Mashuhuda wamesema kukatika na kurejea kwa umeme mara kwa mara ndiko kunakodhaniwa kusababisha moto huo.
Taarifa zinaeleza kuwa kabla ya tukio hilo, katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Geita, umeme ulikuwa ukikatika na kuwaka mara kwa mara, hali iliyopelekea mlipuko ulioanzia katika eneo lililokuwa na vifaa vya muziki kabla ya moto kuenea katika jengo hilo.
Mhudumu wa baa hiyo, Nancy Musa amesema moto ulitokea ghafla wakati wakikamilisha hesabu za mauzo ya siku.
“Moto ulianza ghafla. Tulijaribu kuuzima, lakini ulikuwa tayari umeenea. Sehemu kubwa ya vinywaji iliteketea, ingawa vyumba vya kulala viliathirika kwa kiwango kidogo,” amesema.
Hakuna taarifa za vifo zilizoripotiwa katika tukio hilo, huku jitihada za kutathmini kiwango cha uharibifu wa mali zikiendelea.
Mmiliki wa Suzy Lounge, Peter Cheyo amesema wakati tukio linatokea kulikuwa na kukatika na kurejea kwa umeme mara kwa mara kabla ya kusikika kwa mlipuko mdogo na kisha moto kuzuka.
“Umeme ulikuwa ukikatika na kurudi kila baada ya sekunde chache. Ghafla tukasikia kama mlipuko, ndipo tukagundua ni moto. Tulijaribu kuuzima lakini ulituzidi nguvu,” amesema Cheyo, akiongeza kuwa thamani ya mali zilizoteketea bado haijajulikana.
Baadhi ya wananchi walioshiriki katika jitihada za kuzima moto huo wameiomba Serikali kuharakisha uanzishwaji wa kituo cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika Mji wa Katoro ili kupunguza hasara pindi majanga yanapotokea.
Mkazi wa Katoro, Masanja Mapinda, amesema kuchelewa kwa huduma za zimamoto kunasababisha hasara kubwa.
“Katoro ni mji mkubwa wa kibiashara. Tunahitaji kuwa na kituo cha zimamoto hapa ili majanga kama haya yadhibitiwe mapema bila kusubiri msaada kutoka Geita,” amesema Mapinda.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Katoro, Mhandisi Kija Ntemi, ametoa wito kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuharakisha mchakato wa kuanzisha kituo katika mji huo.
“Kama kungekuwa na kituo cha zimamoto hapa Katoro, moto usingesababisha madhara makubwa. Kutegemea Geita kunachelewesha msaada,” amesema Kija Ntemi.
Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita, Mrakibu Msaidizi Wambura Fidel, amesema Serikali iko katika hatua za mwisho za kuanzisha ofisi ndogo ya zimamoto Katoro.
Amesema umbali wa kutoka Geita hadi Katoro ni kati ya kilometa 47 hadi 50, hali inayosababisha kuchelewa kwa kufika eneo la tukio, hasa pale taarifa zinapotolewa kwa kuchelewa.
“Ni kweli tunakumbana na changamoto ya umbali. Tunapokea taarifa kwa kuchelewa na maandalizi huchukua muda, lakini mpango wa kuanzisha ofisi ndogo Katoro upo na unatarajiwa kutekelezwa mwaka huu,” amesema Fidel.
Tukio hilo ni la pili ndani ya miezi sita katika eneo hilo, ambapo Juni 10, 2025, moto ulioteketeza maduka 17 ya wafanyabiashara katika Soko la Buseresere ulizua malalamiko makubwa ya wananchi kuhusu uchelewaji wa huduma za zimamoto katika mji wa Katoro, ambao kijiografia umeungana na eneo hilo na una shughuli nyingi za kibiashara.
