Trump asifu operesheni ya ‘kumkamata’ Maduro, Venezuela yatoa kauli

Washington/Caracas. Rais wa Marekani, Donald Trump, amesifu kile alichokiita operesheni “iliyopangwa kwa ustadi” wa kijeshi iliyodaiwa kusababisha kukamatwa kwa Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro, na mkewe Cilia Flores, huku Serikali ya Venezuela ikitaka ithibitishiwe uhai wa viongozi hao na kulaani hatua za Marekani.

Akizungumza na gazeti la The New York Times saa chache baada ya kutangaza operesheni hiyo kupitia mtandao wake wa Truth Social mapema Jumamosi, Trump amesema operesheni hiyo ilihusisha mipango mizuri na vikosi bora vya kijeshi.

“Ilikuwa operesheni ya hali ya juu, kwa kweli,” amesema, akiongeza kuwa maelezo zaidi yangetolewa katika mkutano na waandishi wa habari uliopangwa kufanyika Mar-a-Lago, Florida.

Kwa mujibu wa Trump, Marekani imetekeleza shambulio kubwa la kijeshi mjini Caracas alfajiri ya Jumamosi, ambapo milipuko ilisikika na moshi kuonekana katika maeneo mbalimbali ya mji huo.

Ripoti za vyombo vya habari vya kimataifa zilisema milipuko ilianza majira ya saa 2:00 usiku kwa saa za ndani, huku baadhi ya miundombinu ya kijeshi ikiripotiwa kukosa umeme.

Hata hivyo, hadi sasa hakuna uthibitisho huru kutoka Pentagon au Jeshi la Marekani unaothibitisha madai ya kukamatwa kwa Maduro.

Serikali ya Venezuela, kupitia Makamu wa Rais Delcy Rodríguez, imedai haijui alipo Rais wala mkewe, na kuitaka Marekani kutoa “uthibitisho wa uhai” wa viongozi hao, ikieleza hofu kuhusu usalama wao.

Wakati huo huo, Mwanasheria Mkuu wa Venezuela, Tarek William Saab, amelaani operesheni hiyo, akidai kuwa raia wasio na hatia wameuawa au kujeruhiwa katika kile alichokiita shambulio la kigaidi.

Ametoa wito wa maandamano ya amani, huku Serikali ya Venezuela ikiitaja Marekani kuwa imekiuka sheria za kimataifa.

Seneta wa Marekani, Mike Lee, amenukuliwa akisema mashambulizi ya angani yaliyoambatana na operesheni hiyo yamelenga kuunga mkono utekelezaji wa hati ya kukamatwa kwa Maduro, ambaye Marekani inamtuhumu kwa makosa ya “narco-terrorism.” Trump amesema anapanga kumsafirisha Maduro hadi Marekani ili akabiliane na mashtaka hayo.

Maduro alishtakiwa mwaka 2020 kwa tuhuma za kuhusika na usafirishaji wa dawa za kulevya kwenda Marekani, huku Trump wakati huo akiweka zawadi ya dola milioni 15 kwa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwake.

Kiasi hicho kiliongezwa hadi dola milioni 50 mwaka 2025. Trump anadai Maduro ni kiongozi wa mtandao wa dawa za kulevya unaojulikana kama Cartel de los Soles.

Tukio hilo limezua mshtuko kimataifa. Urusi, mshirika wa karibu wa Venezuela, imesema ina wasiwasi mkubwa kuhusu taarifa za kukamatwa kwa Maduro na mkewe, ikitaka ufafanuzi wa haraka na ikionya huenda Marekani imekiuka sheria za kimataifa.

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, CIA ilidaiwa kufuatilia mienendo ya Maduro kwa siku kadhaa kabla ya operesheni hiyo, huku ikielezwa kuwa rais huyo alikuwa ameongeza ulinzi na kubadili maeneo ya kulala mara kwa mara. Hali ya usalama Venezuela inaendelea kuwa tete, huku jumuiya ya kimataifa ikifuatilia kwa karibu maendeleo ya tukio hilo lenye athari kubwa za kisiasa na kiusalama katika eneo la Amerika ya Kusini na duniani.