Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika salamu za mwaka mpya 2026, kimetaka kuachiwa huru bila masharti Mwenyekiti wake, Tundu Lissu.
Mbali ya hayo, kinataka mageuzi ya kimfumo, Tume Huru ya Uchaguzi, Katiba mpya, uchunguzi huru wa kimataifa kuhusu matukio ya mauaji na utekaji, pamoja na kufutwa kesi ya kusitisha shughuli za chama hicho.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche katika hotuba aliyoitoa leo Januari 3, 2026, amesema mwaka 2025 haukuwa wa kawaida.
“Ulikuwa mwaka wa uamuzi mgumu, maumivu makubwa, lakini pia mwamko wa kihistoria wa dhamira ya Watanzania ya kudai haki, uhuru na demokrasia ya kweli,” amesema.
Amesema 2025 Chadema iliandika historia katika demokrasia ya ndani ya chama hicho kupitia mkutano mkuu wa taifa, ambao Lissu alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wake wa Taifa.
Hata hivyo, amesema leo Januari 3, 2026 ni siku ya 269, tangu alipokamatwa na kuwekwa mahabusu kwa kesi aliyodai ni ya uongo, batili na yenye uonevu wa makusudi. Lissu anashtakiwa kwa kosa la uhaini.
Heche amesema wanataka aachiwe bila masharti kwa kuwa si mhaini, hajasema uongo na wala hajafanya uchochezi wowote, akieleza aliyoyasema ni kweli.
Akizungumzia umoja ndani ya Chadema amesema: “Tofauti za mawazo ndani ya chama cha kidemokrasia si ufa, ni misingi ya kujenga hoja bora na uamuzi thabiti. Tunapokubaliana kutofautiana kwa heshima na kusimama pamoja mara uamuzi wa chama unapofikiwa, tunaifanya Chadema iwe na nguvu ya kimaadili na kisiasa isiyoyumbishwa.” Kuhusu uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 amesema uliiacha Tanzania ikiwa na jeraha la kisiasa ambalo litachukua muda mrefu kupona.
Amedai kulikuwa na matumizi mabaya ya vyombo vya dola, ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na mahakama dhidi ya wakosoaji wa Serikali, wanaharati na wapinzani wa kisiasa, hususan Chadema, ambacho kilifungiwa kufanya shughuli zake za kisiasa kwa alichoeleza visingizio vya kesi za uongo.
Amesema vuguvugu la No Reforms, No Election linabaki kuwa alama ya mwamko wa kihistoria, ushahidi kwamba wananchi waligundua ukweli wa kimsingi.
“Bila mageuzi ya kimfumo, uchaguzi si suluhisho bali ni tatizo linaloendelezwa. Hapo ndipo sauti ya wananchi ilipogeuka kuwa falsafa ya ukombozi wa kisiasa,” amesema.
Kuhusu matukio yaliyosababisha vifo wakati wa uchaguzi amesema: “Haya si matukio ya kawaida ya kisiasa; ni makosa makubwa dhidi ya ubinadamu yanayopingana na misingi ya haki za binadamu inayotambuliwa kimataifa. Ndiyo maana Chadema inasisitiza uchunguzi huru, unaoaminika, na wenye uwakilishi wa kimataifa.”
Alisema wanasema hivyo kwa sababu kiwango cha madhara kimevuka uwezo wa taasisi za ndani pekee kujihakiki. Taifa lolote linalojali heshima yake duniani haliwezi kunyamazia damu ya raia wake ikimwagika bila ukweli na uwajibikaji.
“Tunadai haki kwa wahanga, kwa waliopoteza viungo vyao, na kwa familia zilizobaki na majonzi yasiyo na majibu. Taifa haliwezi kujengwa juu ya damu ya raia wake, na haki ikicheleweshwa, kwa vigezo vya kitaifa na kimataifa, ni haki iliyonyimwa”.
Akizungumzia Katiba, amesema: “Tunaitaka Tanzania inayosimama juu ya Katiba iliyo hai, si maandishi matupu bali mkataba wa haki kati ya wananchi na dola. Tanzania inayotawaliwa na sheria, si matakwa ya wachache; inayolinda haki za binadamu kama msingi wa utu, si hisani ya watawala.”
Amesema wanadai Katiba mpya ya wananchi itakayorudisha heshima ya kura, kusimika uwajibikaji na kufungua njia ya haki kwa wote.
Vilevile, amesema: “Tunadai Tume Huru ya Uchaguzi ili sauti ya mwananchi isizimwe, ili uamuzi wa wengi usipinduliwe na wachache. Haya si matamanio ya kisiasa, ni haki za msingi zinazostahili kutekelezwa sasa, bila kuchelewa,” amesema.
Kwa msingi huo, amesema maridhiano hayawezi kuwapo bila haki na kwamba, hakuna haki bila uwajibikaji.
Amesema bila kukiri makosa na kuwawajibisha waliotekeleza vitendo husika, maridhiano hugeuka kuwa aina ya ukandamizaji wa kumbukumbu za mambo yaliyotokea.
Chadema imeigusa pia ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, ikiihusisha na kesi iliyopo mahakamani iliyosababisha chama hicho kusitishiwa shughuli za kisiasa na matumizi ya mali za chama, ikieleza inalenga kunyamazisha sauti ya haki na demokrasia.
