Arusha. Vijana wametajwa kuwa kundi lililo katika hatari kubwa zaidi ya kupata magonjwa ya moyo kutokana na mtindo usiofaa wa maisha, ikiwemo unywaji wa pombe kupita kiasi, uvutaji wa sigara, kutofanya mazoezi na matumizi makubwa ya mafuta ya wanyama.
Kauli hiyo imetolewa leo Januari 3, 2026, jijini Arusha na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Kisenge, wakati wa kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo inayofanyika katika Hospitali ya Arusha Lutheran Central (Seliani).
Dk Kisenge amesema lengo la kambi hiyo ni kusogeza huduma za kibingwa za moyo karibu na wananchi wa Kanda ya Kaskazini, ambao huchangia zaidi ya asilimia tano ya wagonjwa wote 23,000 wanaopata matibabu katika JKCI kila mwaka.
Amesisitiza umuhimu wa jamii, hususan vijana, kubadilisha mtindo wa maisha ili kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo.
“Cha kusikitisha ni kwamba vijana, ambao ndio nguvu kazi ya taifa, wanaongoza kwa kuishi mtindo wa maisha unaochangia ongezeko la magonjwa ya moyo,” amesema.
Amesema kuwa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara imeendelea kushuhudia ongezeko la wagonjwa wa moyo kutokana na sababu hizo, jambo lililoifanya JKCI kuandaa kambi hiyo ili kutoa elimu ya afya ya moyo, kufanya uchunguzi wa mapema na kuanza matibabu kabla hali haijawa mbaya zaidi.
“Tupo hapa si tu kusogeza huduma, bali pia kuwajengea wananchi uelewa wa afya ya moyo, kupima dalili mapema na kuzuia madhara makubwa yanayoweza kuepukika,” amesema.
Katika hatua nyingine, Dk Kisenge amewataka wananchi kubadili mtindo wa maisha kwa kuzingatia mazoezi ya mwili, kupunguza au kuacha unywaji wa pombe na uvutaji wa sigara, hatua ambazo zitapunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya magonjwa ya moyo.
Pia, amesisitiza umuhimu wa wananchi kukata bima ya afya ili kupunguza gharama za matibabu ya moyo, ambayo ni miongoni mwa huduma ghali na hivyo kuwa kikwazo kwa wengi.
“Changamoto kubwa tunayokutana nayo ni kumgundua mgonjwa wa moyo, lakini akakosa uwezo wa kugharamia matibabu,” amesema.
Amesema taasisi hiyo imekuwa ikisamehe zaidi ya Sh1.5 bilioni kwa wagonjwa wasiokuwa na uwezo kila mwaka.
Kwa mujibu wa Dk Kisenge, wagonjwa wengi hufika hospitalini wakiwa tayari wameathirika zaidi na kuhitaji upasuaji, ambao gharama zake ni kubwa, hivyo kusisitiza umuhimu wa uchunguzi wa mapema.
Akizungumza kuhusu kambi hiyo, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo, Mishipa ya Damu na Kifua kutoka JKCI, Dk Alex Joseph, amesema katika siku saba za kambi wamewahudumia wagonjwa 64 wenye matatizo ya mishipa ya damu na miguu, huku baadhi yao wakifanyiwa upasuaji.
“Tumefanikiwa pia kuwafanyia upasuaji wagonjwa tisa tangu kuanza kwa kambi hii na kuleta matumaini makubwa kwao kupunguziwa gharama za kufuata jiji Dar es Salaam.
“Tunatoa wito kwa wananchi wa Arusha na maeneo jirani, pamoja na taasisi za afya, kuwarejea wagonjwa wenye matatizo ya moyo na wawape rufaa kuja hapa ili wanufaike na huduma hizi wakati wa kambi,” amesema.
Mmoja wa wagonjwa waliopata huduma, Amina Husseni, mkazi wa Ngarenero, ameishukuru JKCI kwa kambi hiyo akisema ilimwezesha kugundulika tatizo la moyo baada ya muda mrefu wa kuugua kifua bila mafanikio.
“Nilikuwa nikiandikiwa dawa za kifua ambazo zilikuwa zinatuliza maumivu tu, lakini baada ya ushauri wa ndugu, nilikuja kupima zaidi na kugundulika nina tatizo la moyo,” amesema.
Amesema kuwa amepewa dawa na kupangiwa kurejea kwa matibabu zaidi jumatatu.
Kambi hiyo ya JKCI ilianza Desemba 29, 2025 na inatarajiwa kuhitimishwa Januari 5, 2026, ikilenga kuwahudumia zaidi ya wagonjwa 500 kutoka mikoa ya Kanda ya Kaskazini kwa upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo bila malipo.
