Kibaha. Serikali inajiandaa kuwasilisha bungeni katika Bunge lijalo Muswada wa Sheria ya Usajili wa Watoto Wachanga, hatua itakayoiwezesha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) kuanza kuwasajili watoto tangu kuzaliwa.
Lengo la hatua hiyo ni kuweka msingi imara wa utambuzi wa wananchi mapema, kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii, na kuimarisha mifumo ya usalama wa taifa.
Akizungumza Jumamosi Januari 3, 2025, katika kikao cha 28 cha Baraza la Wafanyakazi wa Nida kilichofanyika Kibaha, Mkurugenzi Mkuu wa Nida, James Kaji, amesema usajili wa watoto wachanga utasaidia mtoto kutambulika kisheria tangu mwanzo wa maisha yake na kuondoa changamoto zinazojitokeza wakati wa usajili wa watu wazima.
Wafanyakazi wa Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA) wakiwa kwenye kikao cha 28 kilichofanyika Kibaha Mkoa wa Pwani leo Junamosi Januari 3,2026 Picha na Sanjito Msafiri
Pia, amesema hatua hiyo itarahisisha upatikanaji wa huduma za afya, elimu, bima na huduma nyingine za kijamii, na kutoa takwimu sahihi za wananchi ambazo zitasaidia Serikali kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo kwa ufanisi.
Kaji pia amewataka wananchi zaidi ya laki tatu ambao vitambulisho vyao vimeshatengenezwa kuvichukua ofisini kwa ngazi ya wilaya.
Amesisitiza kuwa ucheleweshaji wa kuchukua vitambulisho unapelekea hasara kwa Serikali na kupoteza fursa ya wananchi kutumia nyaraka hizo kupata huduma mbalimbali.
Wafanyakazi wa Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA) wakiwa kwenye kikao cha 28 kilichofanyika Kibaha Mkoa wa Pwani leo Junamosi Januari 3,2026 Picha na Sanjito Msafiri
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ally Gugu, amesisitiza umuhimu wa weledi, uaminifu na maadili ya utumishi wa umma kwa watumishi wa NIDA, huku akihimiza mshikamano na ushirikiano kati ya taasisi za Serikali ili kuongeza uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Baadhi ya wakazi wa Pwani, akiwemo Swaumu Mfyome amesema Nida inatakiwa kuongeza juhudi za kutoa elimu na matangazo kuhusu vitambulisho vilivyo tayari ili kuwahamasisha wananchi kuvichukua na kuvitumia, hatua itakayosaidia kuepusha hasara kwa Serikali.