SARE ya bao 1-1 dhidi ya URA, imeifanya Singida Black Stars kuwa timu ya kwanza kukata tiketi ya kucheza nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026.
Singida imefikisha pointi tano katika kundi A na kukaa kileleni ikiwa na uhakika wa kucheza nusu fainali, huku ikiacha msala kwa Azam na URA zenye pointi nne kila moja.
Katika kundi hili, timu mbili zitafuzu nusu fainali, hivyo mechi ya mwisho Azam dhidi ya URA itakayochezwa Januari 5, 2026, itaamua nani ataungana na Singida.
Katika mechi ya leo Januari 3, 2026 iliyochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja, URA ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 26 kupitia Mulikyi Hudu baada ya timu hiyo kuanzisha shambulizi la haraka.
Singida ikasawazisha dakika ya 45, mfungaji akiwa Idriss Diomande ambaye alitumia nafasi ya mabeki wa URA kujichanganya katika kuokoa hatari, akauweka mpira nyavuni.
Katika kikosi cha Singida, ilishuhudiwa Ayoub Lyanga akirejea baada ya kuwa nje ya timu kwa takribani miezi sita.
Kwa kuonyesha kiwango kizuri, kiungo wa Singida, Morice Chukwu alipewa Tuzo ya Mchezaji Bora, huku mfungaji wa bao la URA, Mulikyi Hudu akichaguliwa kuwa Mchezaji Muungwana.
