Polisi Kigoma: Ajali ya Shilole haijaripotiwa kituo chochote

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma limesema taarifa za ajali zinazosambaa kwenye mtandao wa kijamii wa TikTok zikimhusisha msanii wa muziki, Zuwena Mohamed maarufu Shilole, hazijaripotiwa popote.

Taarifa hiyo ya ajali ya Shilole ilitolewa Januari 3, 2025, na mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Revocatus maarufu Baba Levo, akieleza kuwa msanii huyo alipata ajali eneo la Malagalasi mkoani Kigoma, umbali mfupi kabla ya kuingia Mkoa wa Tabora.

Shilole alikuwa akitokea Kigoma kwenye hafla ya Pilau Day iliyoandaliwa na mbunge huyo, akielekea jijini Dodoma.

Baba Levo alisema gari walilokuwa wakitumia liligonga ng’ombe aliyekuwa barabarani, na msanii huyo amepelekwa Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Philemon Makungu, katika taarifa yake iliyotolewa jana Januari 3, 2026, amesema hadi sasa hakuna taarifa yoyote ya ajali hiyo iliyoripotiwa katika kituo chochote cha Polisi mkoani humo, licha ya madai kuwa gari aina ya Toyota Alphard aliyokuwa akisafiria msanii huyo liligonga ng’ombe katika eneo la Maragalasi, wilayani Uvinza.

“Ukweli ni kwamba taarifa hiyo ya ajali haijaripotiwa kituo chochote cha Polisi Mkoa wa Kigoma,” amesema Makungu.

Kamanda huyo amesema kwa mujibu wa sheria, dereva  yeyote anayehusika katika ajali ya barabarani inayosababisha kifo, majeruhi au uharibifu wa chombo cha moto, anawajibu wa kutoa taarifa katika kituo cha Polisi kilicho karibu.

Amesema utoaji wa taarifa ni kwa ajili ya kupata msaada wa matibabu, uchunguzi wa tukio na kuchukuliwa kwa hatua stahiki za kisheria dhidi ya mtuhumiwa aliyesababisha ajali hiyo.

“Tunashauri dereva yeyote anapopata ajali kutoa taarifa katika kituo cha Polisi ili uchunguzi ufanyike na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya mtuhumiwa aliyesababisha ajali,” amesema.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa endapo ajali hiyo ilitokea, msanii Shilole anatakiwa kufika kituo chochote cha Polisi na kuripoti tukio hilo rasmi.

“Endapo tukio hilo la ajali lilitokea, tunatoa wito kwa Shilole kufika kituo chochote cha Polisi kuripoti ajali hiyo ili uchunguzi ufanyike.”

Wakati huohuo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma limewataka madereva wa vyombo vya moto kuendelea kuzingatia na kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kusababishwa na uzembe.

Siku moja baada ya taarifa hiyo ya jeshi la polisi, leo Januari4, 2026, Shilole kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram ameandika,” Nimemwona Mungu kwa macho yangu. Baada ya ajali, nimesimama leo kwa neema yake. Sifa na utukufu ni zake milele, kila pumzi ninayovuta leo ni ushuhuda juu yake.

“Asante ni kwa jumbe zenu, asanteni kwa simu zenu kwangu na kwa watu wangu wa karibu. Asanteni sana kwa dua zenu, hakika Mungu ni mwema sana.”