DC Sweda amaliza mgogoro kati ya waumnii, viongozi wa Kanisa Moravian

Njombe. Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Juma Sweda, amemaliza mgogoro uliodumu kwa miezi kadhaa kati ya waumini wa Kanisa la Moravian Njombe na viongozi wao wa juu kutoka Jimbo la Kusini, huku akiwataka waumini kuhubiri upendo na kudumisha amani ili taifa liendelee kuwa salama na lenye utulivu.

Mgogoro huo ulianza Juni 2025, kufuatia kuondolewa kwa mchungaji wa kanisa hilo bila kufuatwa kwa utaratibu wa kikanisa, jambo lililosababisha taharuki na sintofahamu miongoni mwa waumini.

Akizungumza leo Jumapili, Januari 4, 2026, wakati wa ibada u iliyofanyika katika Kanisa la Moravian wilayani Njombe, Sweda ameeleza kuwa uwepo wake kanisani hapo ni ishara ya kazi ya Mungu ya kulileta kanisa hilo pamoja.

Amesema amefika kwa dhamira ya kujenga na si kubomoa, akisisitiza umuhimu wa amani ili waumini waendelee na shughuli zao za kikanisa na kuchangia ustawi wa taifa la Tanzania.

“Taifa linapokuwa na amani, misingi ya kiroho huwa imara. Amani ikitoweka kwenye familia au kanisa, haiwezi kubaki kwenye jamii. Amani ikiondoka kanisani, huondoka pia kwenye jamii nzima,” amesema Sweda.

Ameongeza kuwa Kanisa la Moravian ni taasisi kubwa, hivyo anatamani kuona waumini wake wakihubiri amani na upendo, ili shughuli za kanisa ziendelee vizuri na hatimaye kudumisha mshikamano wa kitaifa.

Aidha, amewataka waumini kuwa makini mwaka huu kwa kutoiruhusu chuki kupandikizwa mioyoni mwao, akisema kufanya hivyo kunaweza kuwagharimu zaidi badala ya kuwaletea faida. Hivyo, amewahimiza kumtazama Mungu na kumtumainia katika kila jambo.

Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Moravian Tanzania, Jimbo la Kusini, Kenan Panja, amesema amefurahishwa na kumalizika kwa tofauti zilizokuwepo baada ya kukaa pamoja viongozi wa dini, baraza la wazee wa kanisa hilo na Mkuu wa Wilaya ya Njombe.

“Baraza la wazee nimelipenda, baada ya kutoka kwa mkuu wa wilaya, walipendekeza tuendelee kufurahia tukio hilo kama ishara ya maridhiano,” amesema Askofu Panja.

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Kanisa la Moravian Tanzania, Jimbo la Kusini, Ezekiel Mwasambamo, amewapa pole waumini kwa kipindi kigumu walichopitia na kuwaombea uponyaji na nguvu ya kuendelea na shughuli za kanisa pamoja na ibada.

“Tunaishukuru Serikali kupitia mkuu wa wilaya kwa ushirikiano wake. Pia nawapa pole kwa kipindi cha mpito tangu Juni mwaka jana mlipopokea taarifa ya uhamisho wa mchungaji Tumaini Mlawa, ambacho kimekuwa na changamoto mbalimbali,” amesema Mwasambamo.

Baadhi ya waumini wa kanisa hilo, akiwamo Christopher Mbwilo, amesema kuwa baada ya kuondolewa kwa mchungaji wao, waliandika zaidi ya barua tatu kuomba ufafanuzi bila kupata majibu, hadi walipokutana na mkuu wa wilaya.

“Kinachotushangaza ni kupokea maelekezo kutoka eneo jingine, ilhali Jimbo la Njombe lina uongozi wake kamili wa mwenyekiti, katibu, wajumbe na halmashauri kuu ambao wangepaswa kutoa taarifa kwetu,” amesema Mbwilo.

Ameongeza kuwa walipohoji utaratibu huo, hawakupewa majibu ya kuridhisha, hali iliyoongeza sintofahamu miongoni mwa waumini, kabla ya mgogoro huo kumalizwa kupitia ushirikiano wa Serikali na viongozi wa kanisa.