Uchaguzi mwingine mdogo kufanyika Kilimanjaro, Morogoro

Dar es Salaam. Wapiga kura 20,851 waliomo kwenye Daftari la Kudumu la Mpigakura wanatarajiwa kushiriki uchaguzi wa madiwani katika Kata ya Kirua Vunjo Magharibi, Halmashauri ya Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro na Kata ya Mindu, Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro mkoani Morogoro.

Kulingana na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), wapigakura waliopo kwenye daftari hilo ambao wamepoteza au kuharibikiwa kadi zao za kupigia kura, wataruhusiwa kupiga kura kwa kutumia Kitambulisho cha Taifa (Nida), leseni ya udereva au hati ya kusafiria.

Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufaa  Jacobs Mwambegele, amesema uchaguzi huo utafanyika kesho Jumatatu Januari 5, 2026 katika  vituo 55 vya kupigia kura vilivyoandaliwa katika kata hizo mbili.

Akizungumza leo Jumapili, Januari 4, 2026 wakati akisoma risala maalumu kuhusu uchaguzi huo, Jaji Mwambegele amesema wagombea watano kutoka vyama vinne vya siasa wanawania nafasi za udiwani zilizopo wazi, huku akiipongeza hali ya ushindani wa kisiasa unaooneshwa na vyama na wagombea waliokubali kushiriki.

Aidha, amevikumbusha vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huo kuhakikisha vinaweka mawakala katika vituo vyote vya kupigia, kuhesabu na kujumlishia kura ili kufuatilia kwa karibu mchakato mzima wa uchaguzi.

“Wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo na kata husika, wamekamilisha taratibu zote muhimu zinazowawezesha mawakala wa vyama vya siasa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kuzingatia sheria, kanuni na maelekezo ya tume,” amesema Jaji Mwambegele.

Amesema mawakala hao wana jukumu la kulinda masilahi ya vyama na wagombea wao, hivyo wanapaswa kuzingatia misingi ya haki, uwazi na uadilifu wakati wote wa zoezi la uchaguzi.

Kwa mujibu wa tume, vituo vya kupigia kura vitafunguliwa kuanzia saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni na wapigakura watakaokuwa tayari wapo kwenye mstari ifikapo muda wa kufunga wataruhusiwa kupiga kura hadi kazi itakapokamilika.

Jaji Mwambegele  amewahimiza wapigakura kuondoka eneo la kituo baada ya kupiga kura na kufuata maelekezo yote yatakayotolewa na wasimamizi wa uchaguzi wakiwa vituoni.