Rais Samia kuzindua bima ya afya kwa wote Januari hii

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua rasmi Bima ya Afya kwa Wote Januari hii, kwa kutoa kadi ya mfano kwa kaya maskini, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi yake ya siku 100 za kuimarisha huduma kwa wananchi.

Uzinduzi huo utaashiria kuanza rasmi kwa utekelezaji wa mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote nchini, unaolenga kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma za afya bila kikwazo cha gharama kubwa za matibabu.

Awali, Novemba 13, 2025, Rais Samia akilihutubia Bunge, alisema Serikali ilikuwa inajiandaa kuanza majaribio ya mfumo huo kama sehemu ya mageuzi makubwa ya sekta ya afya nchini.

Alieleza kuwa lengo la mfumo huo ni kuwezesha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wote bila kujali hali zao za kiuchumi.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Januari 4, 2026, Meneja Mawasiliano wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), James Mlowe, amesema uzinduzi wa Bima ya Afya kwa Wote unatarajiwa kufanyika Januari hii kutokana na ukubwa na umuhimu wa mpango huo.

“Kwa kuzingatia ukubwa wake, tunatarajia Rais Samia ndiye atakayezindua rasmi Januari hii kwa kutoa kadi ya mfano kwa kaya maskini. Hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi yake ya siku 100,” amesema Mlowe.

Akifafanua kuhusu mfumo wa utoaji wa huduma za afya, Mlowe amesema NHIF inafanya kazi kwa kushirikiana na zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, hospitali za rufaa za mikoa pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Amesema hospitali zote za umma tayari zimeingia makubaliano ya utoaji wa huduma na NHIF, huku baadhi ya hospitali binafsi nazo zikiwa zimeingia mikataba, hali itakayowawezesha wanachama wa NHIF kupata huduma katika vituo hivyo vyote.

“Hospitali zote za umma tumeingia nazo mkataba na pia kuna hospitali binafsi. Mtandao huo ndio utakaotumika kuwahudumia wananchi,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dk Irene Isaka, Desemba 22, 2025, akizungumza na Mwananchi kuhusu utekelezaji wake, alisema maandalizi yote muhimu yamekamilika kwa kushirikiana na Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Rais – Tamisemi.

“Kwa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa bungeni na msisitizo wa Waziri Mkuu, matarajio ni kuanza utekelezaji Januari 2026. NHIF tupo tayari na utekelezaji umeanza kwa baadhi ya makundi maalumu,” alisema Dk Isaka.

Aliongeza kuwa NHIF imeboresha mifumo yake ya Tehama ili kurahisisha wananchi kujisajili binafsi, waajiri kusajili wafanyakazi wao pamoja na kutuma michango kwa njia ya mtandao.

Aidha, mifumo hiyo imefanyiwa majaribio na kuthibitishwa kuwa na uwezo wa kuchakata madai kwa ufanisi.

Dk Isaka alisema mfumo mpya wa malipo umebadilishwa kutoka malipo baada ya huduma kutolewa na sasa kufikia mfumo wa malipo ya mkupuo kabla ya huduma, hatua iliyohitaji maboresho makubwa ya mifumo ya ndani.

“Tumehakikisha mifumo yetu inasomana na mifumo ya taasisi nyingine za Serikali, ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), vyuo vikuu, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), vyama vya ushirika pamoja na Wizara ya Afya na Tamisemi hadi kwenye vituo vya kutolea huduma,” alisema.

Ikumbukwe kuwa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ni sehemu ya makubaliano ya kimataifa yanayolenga kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 kila mtu, popote alipo, anapata huduma za afya anazohitaji bila kukabiliwa na changamoto za kifedha.

Ripoti ya Ufuatiliaji wa Kimataifa ya Bima ya Afya kwa Wote ya mwaka 2025 inaonesha kuwa upatikanaji wa huduma za afya duniani umeongezeka kutoka pointi 54 mwaka 2000 hadi pointi 71 mwaka 2023.

Aidha, idadi ya watu wanaokumbwa na matatizo ya kifedha kutokana na malipo makubwa ya moja kwa moja ya huduma za afya imepungua kutoka asilimia 34 mwaka 2000 hadi asilimia 26 mwaka 2022.

Hata hivyo, ripoti hiyo inaonya kuwa makundi ya watu maskini zaidi bado yanaendelea kubeba mzigo mkubwa wa gharama za huduma za afya, huku watu bilioni 1.6 wakiingia au kusukumwa zaidi katika umasikini kutokana na gharama za matibabu.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), inakadiriwa kuwa watu bilioni 4.6 duniani kote bado hawapati huduma muhimu za afya, huku watu bilioni 2.1 wakikumbwa na changamoto za kifedha katika kupata huduma hizo. Kati yao, watu bilioni 1.6 wanaishi katika umaskini au wamesukumwa zaidi katika umaskini kutokana na gharama za matibabu.