Dar es Salaam. Chama cha ACT – Wazalendo kimeshatanguliza mguu mmoja mbele kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), huku majadiliano ya makubaliano yakielekea hatua za mwisho.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya juhudi mbalimbali zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kushawishi na kuanza kutekeleza baadhi ya masharti yaliyowekwa na chama hicho ili kikubali kuingia SUK, ambalo ni takwa la Kikatiba.
Novemba 10 mwaka jana wakati akizindua Baraza la Wawakilishi, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alisema yupo tayari kutekeleza maridhiano na kuunda SUK.
“Nitaheshimu maridhiano na nipo tayari kuunda SUK kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar,” alisema Dk Mwinyi.
Hata hivyo, alipoteua baraza la mawaziri, aliacha nafasi nne zitakazozibwa na wajumbe kutoka ACT- Wazalendo.
Katika kutekeleza hilo, Novemba hiyo hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi wa Zanzibar, Zena Ahmed Said aliwaandikia barua ACT – Wazalendo akiitaka ipeleke jina la Makamu wa Kwanza wa Rais.
Hata hivyo, Novemba 13, mwaka jana, Mwenyekiti wa chama hicho, Othman Masoud Othman aliwaambia wanachama akiwa ziarani Pemba visiwani humo kuwa, hawakupeleka jina wakati huo kwa madai ya kutoridhishwa na mazingira ya kisiasa.
Lakini, kwa hatua za majadiliano zilizofikiwa ni dhahiri kwamba, chama hicho kipo mbioni kuingia SUK, ili kuimarisha umoja na mshikamano wa Zanzibar na kujiimarisha chenyewe.
Mwananchi imetaarifiwa kuwa, kati ya Januari 17 au 18, 2026 Kamati Kuu ya chama hicho itaketi jijini Dar es Salaam, huku suala la kuingia katika SUK, likiwa moja ya ajenda kuu.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, kikao hicho ndicho kitakachotoka na uamuzi wa dira ya namna ya kuliendea jambo hilo, ambalo hadi kesho litakuwa limebakiza siku 36 kati ya zile 90 kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.
Lakini kikao hicho si cha kwanza, kamati ya uongozi ya chama hicho, ilishaketi Novemba 23, mwaka jana visiwani Zanzibar kutathmini kuhusu uchaguzi na iligusia suala la SUK, ingawa sio kwa mapana yake.
Chanzo kinaeleza ugumu wote kwa chama hicho kuingia SUK, unadaiwa kusababishwa na Serikali kukiuka baadhi ya makubaliano na chama hicho, kilipoingia SUK enzi za hayati Maalim Seif Sharif Hamad, mwaka 2020.
Kwa sababu hiyo, chanzo hicho kinaeleza ACT -Wazalendo mwaka huu kinajadiliana kuhusu SUK kwa tahadhari kubwa, hasa ukizingatia baadhi ya makubaliano ya awali hayakutekelezwa.
Pamoja na yote hayo, chanzo hicho kimeieleza Mwananchi kuwa, suala la kususia kuingia SUK halitakuwepo, kwa sababu kuna kumbukumbu mbaya za kususa mwaka 2016, iliyosababisha kupitishwa kwa baadhi ya sheria ikiwamo ya kura ya mapema.
“Kuingia wataingia, lakini viongozi wanachukua tahadhari kubwa ili yasijirudie yale ya 2020. Pia, haiwezekani kususa kwa sababu ukimsusia bucha fisi anakula zote. Bora tuingie tupambane tukiwa ndani ya Serikali kuliko tukiwa nje,” kimeeleza chanzo hicho.
Chanzo kingine kinaeleza, ACT-Wazalendo imeweka masharti kadhaa ili kuingia SUK na baadhi inadaiwa yameshaanza kutekelezwa, ingawa hayajawekwa wazi.
Kwa hatua hiyo, chanzo hicho kimesema kinachofanya chama hicho ni kutanguliza mguu mmoja ndani ya SUK, huku jitihada nyingine zikiendelea kuhakikisha mwafaka baina ya pande zote unapatikana.
Hata hivyo, chanzo hicho kinaeleza kumekuwa na juhudi za kila namna zinazofanywa na Serikali ya Zanzibar kuishawishi ACT- Wazalendo iingie SUK, ikiwamo kuwatumia wazee maarufu wa bara na Zanzibar na watu wengine maarufu.
Pia, kinasema wapo viongozi wasiotaka kabisa chama hicho kiingie SUK kwa sababu wanadai walidhulumiwa uchaguzi, hivyo ziendelee juhudi za kudai haki.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, ndio maana chama hicho kimefungua kesi za uchaguzi kushinikiza kupatikana kwa haki zake, wakati huohuo kimeshatanguliza mguu kuingia katika SUK, bila kuathiri mapambano ya kudai haki.
Alipotafutwa kuzungumzia hilo, leo Jumapili Januari 4, 2026 Makamu Mwenyekiti wa ACT – Wazalendo Bara, Issihaka Mchinjita amesema msimamo wao ni kwamba, kabla ya kuingia au kutoingia, wanaangalia mazingira yaliyopo sasa na kama malengo ya kuanzishwa SUK yatafikiwa.
Mchinjita amesema SUK ilianzishwa kuepusha mitafaruku na migogoro ya kisiasa na kijamii, uhasama wa kiraia na kinachofanywa na ACT – Wazalendo ni kutathmini iwapo hatua yao ya kuingia mwaka 2020 imeleta matokeo chanya.
Kwa tathmini yao, Mchinjita amesema wanaona pamoja na chama hicho kuingia SUK 2020, hakuna matokeo chanya yaliyopatikana, hivyo wanatafakari kuona je, wanapaswa kuingia kwa namna ile ile au kwa namna ipi itakayoleta tija kwa umma.
“Tunaona kuingia kwa namna tulivyoingia hatuoni malengo ya kuanzishwa kwa SUK yakitimia. Ikiwa kuingia kwa namna ya zamani itakuwa muarobaini tutaingia, lakini ikiwa kuingia ni kwa sababu ya kupeana vyeo haitakuwa na maana.
“Tuko tayari kujadiliana kwenye eneo hilo na zipo hatua zinazochukuliwa ingawa ni za ndani kwa sasa, tunatazama na kuona kama itafika hatua ya kutoa taarifa kwa umma,” amesema Mchinjita ambaye ni mjumbe wa kamati kuu.
Kuhusu kikao cha kamati kuu, Mchinjita amethibitisha kitafanyika Januari 18, 2026 na kwamba, suala la SUK ni miongoni mwa yatakayojadiliwa.
“Suala la SUK ni moja ya mambo ambayo kamati kuu itapokea taarifa yake na kutoa mwongozo. Kikao hicho pia kitafanya tathmini ya jumla ya masuala ya uchaguzi,” amesema.
