Watumiaji wa bahari watahadharishwa upepo mkali, mawimbi makubwa kuanzia leo

Dar es Salaam. Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) limewataka wavuvi na wasafirishaji kwa njia ya maji, kuchukua tahadhari ya upepo mkali na mawimbi makubwa katika Bahari ya Hindi kuanzia leo Jumatatu Januari 5, 2026 hadi Januari 8 mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Tasac kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana Jumapili Januari 4, 2026,  imepokea taarifa kutoka Mamlaka ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu uwepo wa upepo mkali unaofikia kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayofikia mita mbili katika baadhi ya maeneo ya ukanda  wa pwani na Bahari ya Hindi.

Tasac imeeleza kuwa, taarifa hiyo imetaja maeneo hayo kuwa ni mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani (ikiwamo Mafia), Lindi, Mtwara pamoja na visiwa vua Unguja na Pemba.

“Upepo huo, una uwezekano wa kusababisha athari kwa kiwango cha wastani  kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi, uvuvi na usafirishaji katika maeneo tajwa. Tasac inawataka wadau wote wa usafiri wa majini wakiwamo wavuvi, wasafirishaji na wananchi wanaotegemea bahari kwa shughuli zao, kuchukua tahadhari za kutosha.”

Inaeleza kuwa, miongoni mwa tahadhari hizo ni kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinazotolewa na TMA pamoja na kufuata ushauri na miongozo ya wataalamu wa sekta husika.

Aidha, Tasac imewakumbusha wananchi kuwasiliana mara moja na kituo cha kuratibu shughuli za utafutaji na uokoaji majini endapo kutatokea dharura yoyote.