Simba yaifuata Azam nusu fainali Mapinduzi Cup

NI rasmi sasa Mzizima Derby inapigwa kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi kati ya Azam dhidi ya Simba.

Hiyo ni baada ya timu hizo kila moja kuongoza kundi katika Kombe la Mapinduzi 2026 inayoendelea kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja.

Azam ilitangulia mapema leo Januari 5, 2026 jioni ilipoifunga URA na kuongoza kundi A, kisha usiku Simba ikaichapa Fufuni 2-1.

Mabao ya Simba yaliyoipa nafasi ya kuongoza kundi kwa pointi sita yamefungwa na Hussein Mbegu kwa kichwa dakika ya 23 na Naby Camara aliyeachia shuti dakika ya 90.

Kabla ya hapo, Fufuni ilitangulia kwa bao la dakika ya 14 lililofungwa na Mboni Stephen Kibamba ambaye naye aliachia shuti kali lililomshinda kipa kijana wa Simba, Alexander Erasio.

Kwa matokeo hayo, Azam na Simba zitakutana Januari 8, 2026 kuanzia saa 2:15 usiku.

Mara ya mwisho Azam kucheza na Simba ilikuwa Desemba 7, 2025 katika mechi y Ligi Kuu Bara iliyofanyika Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na Azam kushinda 2-0.