Dar es Salaam. Kwa wazazi na walezi wengi, dhana ya kumpa mtoto elimu hujikita zaidi katika kulipa ada ya shule, kununua sare, vitabu na vifaa vya masomo.
Ingawa haya ni mambo ya msingi na muhimu, ukweli ni kwamba elimu ya mtoto ni zaidi sana ya ada na sare.
Elimu ni mchakato mpana unaomjenga mtoto kiakili, kimaadili, kihisia na kijamii. Mafanikio ya mtoto shuleni na maishani hutegemea kwa kiasi kikubwa ushirikiano wa karibu kati ya wazazi, walezi na walimu.
Wazazi na walezi ndio msingi wa kwanza wa elimu ya mtoto. Mtoto huanza kujifunza tangu akiwa nyumbani kupitia malezi, mazungumzo na mifano anayoiona kwa wazazi wake. Hivyo, jukumu la mzazi halipaswi kuishia katika kulipa ada pekee.
Kwanza, wazazi wana wajibu wa kufuatilia maendeleo ya mtoto kielimu. Hii inahusisha kuangalia daftari, matokeo ya mitihani, kazi za nyumbani na kuuliza mtoto anajifunza nini kila siku. Mtoto anapoona mzazi ana interest na masomo yake, hujihisi kuthaminiwa na huongeza bidii katika kujifunza.
Pili, wazazi wanapaswa kumsikiliza mtoto na kujua changamoto zake shuleni. Watoto hukutana na matatizo mbalimbali kama vile kuonewa, kushindwa kuelewa masomo, au kuwa na hofu kwa walimu au mazingira ya shule.
Mzazi anayempa mtoto nafasi ya kuzungumza humsaidia mtoto kupunguza msongo wa mawazo na kutatua matatizo mapema kabla hayajakuwa makubwa.
Tatu, wazazi wanapaswa kujenga mazingira mazuri ya kujifunzia nyumbani. Hii inaweza kuwa kwa kumpa mtoto muda wa kusoma, sehemu tulivu ya kufanya kazi za shule, na kumtia moyo badala ya kumkatisha tamaa. Maneno ya faraja na pongezi yana nguvu kubwa katika kumjengea mtoto kujiamini.
Aidha, wazazi wana wajibu wa kumlea mtoto kimaadili. Nidhamu, heshima, uaminifu na uwajibikaji ni misingi ya elimu bora.
Mtoto anayelelewa vizuri nyumbani huonyesha tabia njema shuleni na huwa tayari kujifunza. Elimu bila maadili humpa mtoto maarifa bila mwelekeo sahihi wa maisha.
Ushiriki wa wazazi shuleni
Ushirikiano kati ya wazazi na shule ni nguzo muhimu ya mafanikio ya mtoto. Wazazi wanapaswa kuhudhuria mikutano ya shule, kuwasiliana na walimu na kutoa mrejesho kuhusu maendeleo ya mtoto.
Kukaa mbali na masuala ya shule humfanya mtoto ajisikie kana kwamba elimu yake si kipaumbele kwa familia yake.
Pia, wazazi wanapaswa kuwajibika kifedha kwa wakati, si kwa sababu ya shule pekee bali kwa maslahi ya mtoto. Mtoto anapocheleweshwa au kurudishwa nyumbani kwa sababu ya ada, huathirika kisaikolojia na hupoteza muda wa kujifunza.
Hii inaonyesha kuwa kulipa ada kwa wakati ni sehemu ya kumpa mtoto utulivu wa kujifunzia, si tu kutimiza sharti la shule.
Walimu ni nguzo ya pili muhimu katika safari ya elimu ya mtoto. Mbali na kufundisha masomo darasani, walimu wana jukumu kubwa la kumlea na kumjenga mtoto kwa ujumla.
Mtoto hutumia muda mwingi shuleni, hivyo walimu huwa sehemu ya maisha yake ya kila siku.
Kwanza, walimu wanapaswa kuonyesha upendo, uelewa na subira kwa watoto. Kila mtoto ana uwezo na kasi yake ya kujifunza.
Mtoto anayeshindwa kuelewa somo anahitaji msaada zaidi, si adhabu au maneno ya kumkatisha tamaa. Walimu wanaotambua tofauti hizi huwasaidia watoto wengi kufikia uwezo wao kamili.
Pili, walimu wana wajibu wa kugundua mapema changamoto za kisaikolojia na kijamii kwa watoto. Mtoto aliyenyamaza sana, anayebadilika tabia au kushuka kielimu anaweza kuwa na tatizo nyumbani au shuleni.
Mwalimu makini anaweza kumshirikisha mzazi au uongozi wa shule ili kumsaidia mtoto kabla hali haijawa mbaya.
Tatu, walimu wanapaswa kuwa mfano wa maadili mema. Watoto hujifunza zaidi kwa kuiga. Mwalimu mwenye nidhamu, heshima na uadilifu humjenga mtoto kuwa raia mwema. Elimu bora si tu kufaulu mitihani, bali ni kumlea mtoto awe mtu mwema katika jamii.
Elimu ya mtoto inafanikiwa pale ambapo kuna mshikamano kati ya mzazi, mwalimu na mtoto mwenyewe. Mzazi anapowajibika, mwalimu anapofundisha kwa moyo na mtoto anapopata mazingira salama ya kujifunzia, matokeo yake huwa chanya. Kila upande unaposhindwa kutimiza wajibu wake, mtoto ndiye anayepata hasara kubwa zaidi.
Ni muhimu kwa jamii kutambua kuwa mtoto ni rasilimali ya taifa. Kumpa mtoto elimu bora leo ni kuwekeza katika maendeleo ya kesho. Hivyo, wazazi na walimu wanapaswa kufanya kazi kwa pamoja bila kulaumiana, bali kwa kushirikiana.
