Simbu kushiriki Burji2Burji Half Marathon

MWANARIADHA wa Alphonce Simbu anatarajiwa kushiriki mbio za Burji2Burji Half Marathon zitakazofanyika Dubai, Februari 8, mwaka huu, akiwa miongoni mwa wanariadha maarufu wa kimataifa.

Mbio hizo zitakuwa sehemu ya maandalizi yake kuelekea Boston Marathon mwezi Aprili zikimuwezesha kuendelea na ushindani wa kiwango cha juu.

Simbu anaingia Dubai akiwa na hadhi ya bingwa wa dunia wa marathoni, baada ya kushinda medali ya dhahabu kwenye mashindano ya dunia ya riadha yaliyofanyika Tokyo, Japan, Septemba 2025, jambo linalomuweka katika nafasi nzuri ya kushindana na wanariadha bora kutoka pande mbalimbali duniani.

Mwanariadha huyo amejipanga vyema kuhakikisha anabaki katika kiwango chake cha juu na kuongeza rekodi zake binafsi, ambapo mbio hizo za Uarabuni zinatarajiwa kuwa jaribio muhimu, huku wapenzi wa riadha wakisubiri kuona kama ataibuka na kushika nafasi za juu.

Simbu ni miongoni mwa wanariadha bora duniani akiwa nafasi ya sita katika viwango vya dunia kwa marathoni ya wanaume na amejizolea medali ya dhahabu katika mashindano ya dunia, shaba kwenye mashindano ya dunia ya riadha na ameshika nafasi za juu mara mbili kwenye michezo ya Olimpiki.

Pia alishinda medali ya fedha kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola, huku rekodi yake binafsi ya marathoni ikiwa saa 2:04:38, iliyopatikana katika mbio za Valencia, Hispania, mwaka 2024.

Mwaka 2025 umemuwezesha nyota huyo mwenye cheo cha Staff Sergent kuonyesha kiwango chake cha kimataifa, baada ya kushinda medali ya dhahabu kwenye mashindano ya dunia, kumaliza nafasi ya pili Boston Marathon, na kumaliza nafasi ya pili mbio za kilomita 25 za Kolkata, India, ambapo alirekodi msimu wake bora, akiamini mwaka huu anaweza kuendeleza yale ya mwaka jana.