Mwili wa dereva wa bodaboda waokotwa msituni Tabora

Tabora. Mwili wa dereva wa bodaboda umeokotwa katika Msitu wa Matitumbi, mkoani Tabora, ukiwa umefungwa mikono kwa kamba ya manila na miguuni kwa mpira, huku ukiwa na majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili.

Mwili huo umetambuliwa kuwa ni wa Sigela Hamisi, mkazi wa Kata ya Tumbi katika Manispaa ya Tabora.

Tukio hilo limebainika leo  Jumanne Januari 6, ikiwa ni siku ya tatu tangu Hamisi alipotoweka, baada ya kuondoka nyumbani Januari 4, 2026 jioni akiwa amepeleka abiria, na kutoonekana tena wala kupatikana kwa simu yake.

Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Costantine Mbogambi, amesema amepokea taarifa za awali kutoka kwa wasaidizi wake kuhusu tukio la mauaji katika Kata ya Tumbi, akibainisha kuwa anasubiri taarifa kamili kabla ya kulizungumzia kwa kina.

Hata hivyo, aliporejelewa tena na Mwananchi saa tisa kasoro robo alasiri, alisisitiza kuwa bado hajapokea taarifa za kina kuhusu tukio hilo na kwamba uchunguzi unaendelea ili kubaini mazingira ya kifo hicho na waliohusika.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Tumbi, Rajabu Hamsini amesema alipokea taarifa kutoka kwa waendesha bodaboda wenzake na marehemu wakieleza kuwa Hamisi  hajarudi tangu siku hiyo, hali iliyowalazimu kuomba barua ya utambulisho ili kuanza jitihada za kumtafuta.

Ameeleza kuwa yeye, vijana hao pamoja na wananchi wa eneo la Tumbi waliungana kumtafuta hadi leo walipofanikiwa kuuona mwili wa marehemu ukiwa umetupwa katikati ya Msitu wa Matitumbi.

Hata hivyo, pikipiki aliyokuwa akiitumia marehemu haikupatikana, ikidaiwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana.

Diwani wa Tumbi, Manispaa ya Tabora, Mwendapole Salma Juma, amesema tukio hilo limewaumiza kwa kiasi kikubwa wazazi na walezi wa eneo hilo, akibainisha kuwa marehemu Hamisi alikuwa kijana mwenye juhudi za kutafuta kipato kwa ajili ya familia yake.

Amesema taarifa za kuokotwa kwa mwili wake zimeacha majonzi katika jamii.

“Licha ya kuwa viongozi, sisi pia ni wazazi. Kama mama, kumpoteza mtoto aliyekuwa tayari ameshaanza kusaidia familia hata kwa mahitaji madogo kama chumvi ni maumivu makubwa sana. Ni uchungu kuona kijana anauawa kikatili kwa sababu ya pikipiki,” amesema diwani huyo.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Maofisa Usafirishaji Mkoa wa Tabora, Mrisho Shime, amewataka waendesha bodaboda kuacha tabia ya kubeba abiria wawili kwa wakati mmoja (maarufu kama mishikaki), hususan nyakati za usiku, akisema hali hiyo huongeza hatari ya kushambuliwa na kushindwa kujinusuru.

Ameongeza kuwa ni muhimu kwa dereva anapopigiwa simu ya kufuata abiria kutoa taarifa kwa wenzake, ikiwezekana akitaja namba ya simu ya abiria aliyempigia, ili kuwezesha ufuatiliaji wa haraka endapo kutatokea ucheleweshaji au tukio lolote lisilo la kawaida.

Hatua hiyo, amesema, itarahisisha kuwabaini wahalifu wanaowashambulia maofisa usafirishaji na kuiba pikipiki zao.

“Hakikisha mnapeana taarifa mnapoitwa na abiria, hasa hawa wa jioni, kwa sababu mara nyingi matukio haya yamekuwa yakitokea katika nyakati hizo,” amesisitiza Shime.

Akizungumza kwa masikitiko, baba mzazi wa marehemu, Hamisi Maulidi, amesema Sigela alikuwa kijana mwema, msikivu kwa wazazi na aliyeishi kwa amani na jamii.

Ameeleza kuwa marehemu alikuwa tayari ameanza kuwahudumia wazazi wake kwa mahitaji muhimu, jambo lililompa matumaini makubwa kwa maisha ya familia.

“Maumivu niliyonayo si rahisi kuyaeleza. Nilikuwa nimeanza kujisikia nafuu kwa sababu mwanangu alikuwa ameshaanza kunisaidia familia, lakini sasa wamejitokeza watu wasio na huruma wakamuua kikatili kwa lengo la kuchukua pikipiki,” amesema kwa uchungu.