Wahimiza kushughulikia chanzo cha watoto wenye uhitaji

Bagamoyo. Wakati jamii ikikumbushwa kusaidia wahitaji ikiwamo watoto wanaoishi vituoni pia imetolewa rai kushughulikia mzizi wa changamoto inayosababisha kukosa malezi ya wazazi kisha kuishia mtaani.

Sababu moja wapo iliyotajwa na msimamizi wa kituo cha kulelea watoto cha masista wa Passionist kiitwacho Kamelot kilichopo Bagamoyo mkoani Pwani, Sister Aschariah Severine ni familia zinaoanzishwa bila malengo wala mpangilio.

Msimamizi huyo amesema baadhi ya watoto walio kwenye mazingira hatarishi si kweli wote hawana wazazi bali wengine wapo lakini hawawathamini akitolea mfano baadhi yao wanaofikia hatua ya kutupa watoto.

Msimamizi Severine amesema hayo mwishoni mwa juma baada ya kupokea msaada wa vyakula na vifaa vya shule kutoka Ismaili Civic Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Lions Tanzanites Club katika kituo hicho cha Kamelot Home chenye watoto 30.

“Tuangalie sababu ya kuwepo kwa watoto hawa kama ni kutelekezwa basi tujue nini chanzo kisha ziwekwe sheria au zitiliwe mkazo. Lazima kuwe makini kwa watu wanaozaa watoto halafu wanakata tamaa kisha wanawatupa.

“Lazima tujue nini kifanyike ikiwamo kutumia busara na nguvu ya ziada ili kumaliza vitendo vya namna hii vinavyopelekea kuwepo kwa watoto wa namna hii,” amesema.

Amesema baadhi ya wazazi wako hai lakini wameacha majukumu yao. Upangaji mbaya wa familia na uhusiano usio imara umewaacha watoto katika mazingira magumu.

Ameongeza unyanyasaji na vurugu za nyumbani zinasalia kuwa miongoni mwa sababu kuu zinazowasukuma watoto kutafuta hifadhi mitaani.

“Baadhi ya watoto hukimbia baada ya kuvumilia unyanyasaji mkubwa wa kimwili na kihisia nyumbani. Wengine huachwa kabisa,” amesema.

Hata hivyo, amepongeza Serikali kwa kuimarisha sheria zinazolenga kuwalinda watoto dhidi ya adhabu ya viboko na unyonyaji mtandaoni, huku akibainisha kuwa utekelezaji na uelewa wa jamii bado unahitaji kuboreshwa.

“Sheria ni imara na zenye nia njema, lakini kubadilisha mawazo na kuhakikisha utekelezaji mzuri bado ni changamoto,” amesema.

Akizungumza kuhusu shughuli hiyo ya utoaji msaada Nazir Thawer, Makamu wa Rais wa Baraza la Shia Ismaili Tanzania, amesema Ismaili Civic inaongozwa na dhamira ya kina ya kuwahudumia wananchi na kuchangia kwa maana ustawi wa jamii kote nchini.

“Kupitia kujitolea kwa mpangilio na ushirikiano, tunalenga kuunga mkono elimu, huduma za afya, uhifadhi wa mazingira, na misaada ya kibinadamu, hasa kwa wale walio katika uhitaji mkubwa.

“Mipango kama hii iliyofanyika hapa Kamelot Home inaakisi imani yetu kwamba maendeleo ya kudumu ya kijamii hujengwa kupitia huruma, huduma, na mshikamano wa pamoja,” amesema Thawer.

Amewataka wadau kuendelea kufanya kazi pamoja katika kutoa huduma kwa watu.

“Ziara hii na iimarishe uhusiano wetu na kutukumbusha jukumu letu la pamoja la kuboresha jamii zetu na kulinda sayari yetu kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema.

Makamu wa Pili wa Gavana wa Wilaya wa Lions Club Tanzania Bhavika Pathi, amehimiza hatua za pamoja katika kushughulikia changamoto za kijamii.

 “Kama tunavyosema katika Lions, ‘kadiri mikono inavyoongezeka, ndivyo huduma inavyoongezeka.’ Kadiri watu wengi wanavyojitolea, ndivyo tunavyoweza kutoa mkono wetu na ubora wa huduma,” amesema.

Ameongeza zaidi kwa kumwalika mtu yeyote kushiriki kikamilifu katika jukumu hili la pamoja la kijamii, kwa sababu huduma kwa jamii ni wajibu kwa watu wote.

“Wakati watu wengi wanapojitolea, matokeo ni makubwa zaidi. Kuhudumia jamii ni jukumu la pamoja linalofaidi jamii kwa jumla,” amesema.