Said Zanda atua JKT Tanzania

UONGOZI wa JKT Tanzania uko katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa mshambuliaji nyota Said Zanda ‘Ronaldo’ kutoka Bigman inayoshiriki Ligi ya Championship baada ya pande mbili kufikia makubaliano.

Taarifa ambazo Mwanaspoti limezipata zinaeleza kwamba Zanda aliyeifungia mabao mawili Bigman msimu huu, amefikia makubaliano ya kujiunga na maafande, huku akiwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa katika dirisha hili.

Akizungumza na Mwanaspoti, rais wa Bigman, Ahmed Waziri Gao, alidai kupokea ofa za timu mbalimbali ambazo zimeonyesha kumhitaji nyota huyo na tayari mazungumzo yameanza huku kilichobaki ni mchezaji kuamua sehemu atakayokwenda.

“Miongoni mwa masharti tuliyompa ni kuhakikisha hasaini mkataba na timu yoyote inayoshiriki Championship na kiukweli kwa sehemu anayokwenda tunaamini atafanya vizuri, japo nisingependa kuiweka wazi kwa sababu bado hawajamtangaza,” amesema Gao.

Hata hivyo, licha ya kauli ya kiongozi huyo, lakini Mwanaspoti linatambua mchezaji huyo tayari amepewa barua ya kuachana na Bigman, ambapo muda wowote atatambulishwa kukitumikia kikosi cha maafande msimu huu.

Zanda alikuwa mhimili muhimu Bigman alikojiunga katika dirisha dogo la Januari 2025, akitokea Stand United ‘Chama la Wana’, huku akiziwahi pia kuzichezea Songea United, Ruvu Shooting na Azam FC.