Takukuru yatoa kauli mabilioni ya Wachina, 137 wakamatwa

Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kinondoni jijini Dar es Salaam katika operesheni maalumu imekamata raia wawili wa China wanaotuhumiwa kuhusika katika mtandao mkubwa wa uhalifu wa kifedha.

Watuhumiwa hao wanajumuishwa kwenye matukio mbalimbali ikiwamo utakatishaji fedha, wizi wa taarifa za kadi za benki na uhujumu uchumi.

Hayo yamesemwa mbele ya waandishi wa habari leo Jumatano, Januari 7, 2026 na Mkuu wa Takukuru wa mkoa huo, Christian Nyakizee.

Amesema katika operesheni maalumu iliyofanyika Januari 5, 2026 walifanikiwa kuwakamata raia hao wakiwa na Dola 707, 075 za Marekani sawa na Sh1.732 bilioni na Sh281.45 milioni zikiwa ndani ya gari katika mifuko ya sandarusi.

Amesema waliokamatwa ni Yao Licong na Wang Weisi ambao ni wakazi wa Oysterbay Phonex Apartments zilizopo wilaya ya Kinondoni.

“Fedha hizo zinashukiwa ni mazalia ya fedha zilizotakatishwa kupitia taarifa za kadi za benki zilizoibwa kutoka kwa watu mbalimbali nje ya nchi,” amesema Nyakizee.

Ukamataji huo umetokana na matokeo ya operesheni maalumu ya miezi saba tangu Mei 2025 iliyoendeshwa kwa kushirikiana na vyombo vingine vya uchunguzi, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), benki za biashara na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Hata hivyo, amesema watuhumiwa hao wameshindwa kuthibitisha uhalali wa upatikanaji wa fedha hizo kwani hawana kampuni au biashara halali zilizowapatia kiasi tajwa na hawana uthibitisho au stakabadhi wa namna walivyonunua fedha za kigeni walizokutwa nazo.

Nyakizee amesema mtuhumiwa Licong alikuwa anatafutwa na taasisi hiyo kwa tuhuma za ufunguaji wa kampuni hewa tano zinazochunguzwa kwa makosa ya ukwepaji kodi na utakatishaji fedha Sh1.8 trilioni zinazodaiwa hazijatozwa kodi tangu mwaka 2019.

Amesema wanawafikisha watuhumiwa mahakamani ya Kisutu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuwafungulia mashtaka ya awali shauri la uhujumu Uchumi. (Tayari wamefikishwa kortini).

Akielezea kuhusu taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii cha kukamatwa na Sh6 bilioni, Nyakizee amesema ukamataji ulifanyika kwa kushuhudiwa na mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Oysterbay ambaye alithibitisha watuhumiwa walikamatwa na kiasi tajwa.

“Ieleweke maofisa wa Takukuru ndiyo waliomuita mwenyekiti wa Serikali ya mtaa ili ashuhudie tukio hili kwa mujibu wa sheria na taratibu za ushahidi na upekuzi,”amesema Nyakizee.

Mbali na hilo, Nyakizee amesema wamewakamata watuhumiwa wengine 137 wamepekuliwa na kuhojiwa katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Mwanza, Dar es Salaam pamoja na Visiwa vya Zanzibar.

Amesema uchunguzi wa awali umebaini zaidi ya Sh18 bilioni zimetakatishwa kwa kutumia malipo ya mashine za POS, payment links, majukwaa ya e-commerce pamoja na kumbukumbu namba kwa ajili ya huduma za utalii, afya, malazi, usafiri wa anga na kodi za ndani.

Amesema watuhumiwa wakuu wa wizi wa taarifa za kadi wanatoka katika nchi za Cameroon, Nigeria, Pakistan, Bulgaria, Macedonia, Poland, Romania na China, huku wakishirikiana na baadhi ya Watanzania waliotumika kupitisha fedha hizo kupitia akaunti zao binafsi na za kampuni.

“Ni genge la kihalifu la kimataifa linalojihusisha na utakatishaji fedha, ukwepaji kodi na uhujumu uchumi. Fedha zilipitia kwenye kadi kisha kuingizwa kwenye akaunti za kampuni binafsi, nyingi zikiwa za vijana Watanzania waliopata huduma za kibenki katika mabenki mbalimbali hapa nchini,” amesema.

Amesema baada ya fedha kuingia kwenye akaunti za kampuni, zilikuwa zinatolewa taslimu na kugawanywa kwa makubaliano ya asilimia fulani kati ya wahusika.

Katika hatua ya kisheria, amesema mashauri matatu tayari yamefunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa makosa ya wizi wa mtandao, utakatishaji fedha na uhujumu uchumi. Mashauri hayo ni ECC 21633/2025, ECC 29134/2025 na ECC 29143/2025.

“Kati ya washtakiwa waliopo mahakamani ni raia wa China saba, raia mmoja wa Bulgaria na Mtanzania mmoja. Hatua nyingine za kisheria zinaendelea kwa watuhumiwa wengine pamoja na jitihada za kurejesha fedha zilizoibiwa,” alalisema.

Pia, amesema zaidi ya Sh1 bilioni tayari zimerejeshwa kwa waathirika, huku Sh 3bilioni zikizuiwa kwenye akaunti za watuhumiwa kusubiri kukamilika kwa uchunguzi.