SIMBA katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 inayofanyika Zanzibar, ilianza hatua ya makundi na clean sheet ikishinda 1-0 dhidi ya Muembe Makumbi City, lakini ikajikuta ikishindwa kulinda lango lake mbele ya Fufuni licha ya kufuzu nusu fainali.
Aliyeitibulia Simba ni mshambuliaji wa Fufuni, Mboni Stephen Kibamba baada ya kuitanguliza timu hiyo kwa bao la dakika 14, kabla ya Simba kusawazisha katika dk23 kupitia Hussein Mbegu na Naby Camara akaihakikishia ushindi dakika ya 90.
Mwamba huyo aliyekuwa wa kwanza kutikisa nyavu za Simba katika Kombe la Mapinduzi, ndiye kinara wa mabao katika Ligi Kuu Zanzibar msimu huu wa 2025-2026 akifunga 10 na asisti sita katika mechi 15 za duru la kwanza.
Katika mahojiano maalum na Mwanaspoti yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mao Zedong vilivyopo Mjini Unguja, nyota huyo amesema ushirikiano kutoka kwa wachezaji, bidii na maelekezo ya mwalimu ndiyo yaliyosababisha kuwa hapo alipo.
Mboni mwenye hat-trick moja msimu huu, anasema kwa kiwango alichonacho sasa, hakudhani itakuwa hivyo kwani kimeongezeka zaidi ya matarajio yake.
Anasema, mafanikio hayo yamechangiwa na kujituma kwenye mazoezi na mechi kwa kushirikiana na wachezaji wenzake wakiwa uwanjani.
Anasema hana uzoefu mkubwa kwenye Ligi Kuu Zanzibar kwani hiyo ni mara yake ya pili kushiriki, alianza kushiriki ligi hiyo akiichezea timu ya Maendeleo (2020), kisha Fufuni msimu huu.
“Ligi imekuwa na ushindani mkubwa kwa sababu inafuatiliwa na watu wengi na kila mchezaji ana hamu ya kuyafikia mafanikio yake, hivyo hayo yanaleta ladha halisi ya burudani ya soka kisiwani hapa,” anasema.
Anasema, safari yake ilianzia kwenye kituo cha Moro Kids kilichopo Morogoro kinachoshiriki First League Tanzania Bara.
Mwaka 2023, alipata nafasi ya kucheza timu ya vijana ya Simba chini ya umri wa miaka 20, ikinolewa na Kocha Mohammed Mrishona ‘Xavi’ na baada ya kutoka hapo alirudi Morogoro, ndipo alipofanikiwa kusajiliwa Fufuni msimu huu.
Anasema, Fufuni ni timu ambayo imempa nafasi na mwamko mkubwa wa kuona ipo siku atazifikia ndoto zake za kuwa mchezaji mkubwa Tanzania na mwenye ushawishi kwa vijana wenzake.
Mboni ni miongoni mwa washambuliaji wanaoishi kwenye ndoto za kuamini kuwa juhudi na bidii ndio njia ya kufika unapostahili kwani anasema hakuna mchezaji ambaye alivutiwa naye hadi kuamua kuwa mchezaji.
Mshambuliaji huyo amejizolea umaarufu mkubwa kisiwani hapa baada ya kufunga bao la kwanza lililofungua pazia la timu hiyo kwenye mechi iliyochezwa Oktoba 2, 2025 kati ya Kipanga na Fufuni, kwenye Uwanja wa Mao B, Mjini Unguja.
Jina la Mshambuliaji huyo linaakisi kwa vitendo uhalisia wake kwani Mboni amekuwa jicho la timu ya Fufuni huku akiijengea historia nzuri kwa kutupia mabao kwa timu ngumu na kongwe za kisiwani hapa.
Mshambuliaji huyo amejenga utawala mzuri kwenye duru ya kwanza ya Ligi Kuu Zanzibar kwa kuzifunga timu zenye rekodi kubwa ikiwamo KVZ, Uhamiaji, Kipanga, Polisi, Muembe Makumbi na Zimamoto.
Mboni anasema anajisikia furaha sana baada ya kuweka kimiani mabao manne peke yake kwenye mechi yao dhidi ya Muembe Makumbi iliyochezwa Uwanja wa Gombani uliopo Pemba, mchezo ulioongeza idadi ya mabao yake kwa duru hiyo.
Katika kipindi hiki cha mafanikio hayo, anatamani kucheza Ligi Kuu Tanzania na anasema timu itakayokuja mezani na kukubaliana naye atakuwa tayari kuitumikia kwa nguvu zake zote.
KUSHIRIKI MAPINDUZI CUP 2026
Anasema anajivunia kushiriki mashindano ya Kombe la Mapinduzi ikiwa ni mara yake ya kwanza kucheza na kinachofanya ajivunie zaidi ni kuwa miongoni mwa wachezaji waliofunga na kuipatia timu yake pointi moja katika mechi ya kwanza, kisha kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo huku akivuna Sh1 milioni na tuzo kwenye mechi iliyochezwa Desemba 29, 2025 dhidi ya Mwembe Makumbi iliyomalizika kwa sare ya 1-1. Baada ya hapo, mechi ya pili Fufuni ilifungwa 2-1 na Simba, yeye ndiye aliyefunga bao pekee la Fufuni.
Anafafanua kuwa: “Sikutarajia kucheza kwenye mashindano haya, lakini imekuwa jambo la bahati sana kwangu kuonyesha kile nilichonacho,” anasema.
Fufuni yenye makao makuu kisiwani Pemba ambayo imepanda daraja msimu huu, imemaliza ya pili katika kundi B la Kombe la Mapinduzi nyuma ya vinara Simba huku Muembe Makumbi ikiwa mkiani ingawa zina pointi sawa na Fufuni.
Fufuni imeonekana kuwa na ushindani mkubwa kwenye Ligi Kuu ya Soka Zanzibar ikitazamiwa kuleta upinzani kama ilivyokuwa kwa Jamhuri, Super Falcon na Chipukizi miaka ya nyuma.
YONDANI ANAMNYIMA USINGIZI
Mboni anasema, kati ya mabeki wanaompa changamoto kubwa kwenye Ligi ya Zanzibar ni Kelvin Yondani kwani ana uzoefu mkubwa katika mashindano mbalimbali ikiwamo Ligi Kuu Tanzania Bara.
Yondani anayechezea New Kings ya kisiwani Unguja, ni miongoni mwa mabeki wanaotikisa katika Ligi Kuu Zanzibar kutokana na kiwango chake kizuri.
Mboni anasema ili awe imara zaidi ya alipo sasa anatamani kupata kocha wa viungo ambaye atampatia maelekezo na mazoezi kulingana na nafasi anayoicheza, kwani kwenye kikosi cha Fufuni hakuna kocha rasmi wa viungo.
Anaeleza, endapo anaweza kupata kocha wa viungo atakuwa bora zaidi kwa sababu licha ya mazoezi wanayofanya kwa timu, yeye binafasi anatenga muda maalumu wa kufanya mazoezi.
Anasema, mashabiki wanampa morali ya kufanya vizuri katika soka hususani anapopata simu za pongezi kutoka kwao.
Hivyo, anawaomba mashabiki wake na Fufuni waendelee kumsapoti anaahidi hatowaangusha na atawapa burudani akiwa uwanjani.
Wakati mwingine ugumu wa kufanya jambo haupaswi kuonekana kama adhabu bali ni darasa la maisha linalotoa mafunzo ya uvumilivu, nidhamu, kujithamini na kujiamini.
Mboni analiambia Mwanaspoti: “Kipindi nasoma Shule ya Sekondari Bulonge iliyopo Kigoma Mjini mwaka 2014, nilipata nafasi ya kuchaguliwa kushiriki katika mashindano ya kikanda ya Umiseta.
“Nilitembea kwa miguu mwezi mmoja kufika sehemu za mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mashindano.
“Wakati tumemaliza mazoezi ya kujiandaa na safari siku mbili kabla tuliitwa ili kupewa taarifa ya kuondoka, wanafunzi 23 walipata nafasi isipokuwa mimi, ikanibidi niachwe, hili tukio siwezi kulisahau maisha yote,” anasema.
IMANI YA USHIRIKINA KATIKA SOKA
Anasema unaweza usiwe na imani kuhusu ushirikina kwenye soka, lakini pengine timu unayoichezea ina imani hizo hivyo inakubidi ufuate.
Mboni anasema, alishawahi kukutana na hilo katika timu fulani ambapo walitakiwa kuvunja nazi njiapanda na kunywa maji ambayo hawajui yamewekwa dawa gani.
Mbali na hilo, anasema siku akipata nafasi ya kuitwa kwa lengo la kuichezea timu ya Taifa jambo la kwanza atasali na kumshukuru Mungu kwa neema hiyo.
Mboni anaeleza kuwa, Mungu ndio msimamizi mkubwa na mwaminifu kwenye mapambano na ndiye anayeombwa na kufanikisha ndio maana ya kufanya hivyo ili kumshukuru kwa kujibu maombi yake.
Akiwa nje ya uwanja, mshambuliaji huyo anasema anapenda zaidi kuangalia maigizo na movies zilizotafsiriwa, kuweka akili sawa na kupata mawazo mapya.
