Mzizima Derby… Mechi ya kisasi

UMEPITA mwezi mmoja tu tangu ilipopigiwa Dabi ya Mzizima Ligi Kuu Bara, ambapo ilishuhudiwa Simba ikipasuliwa kwa mabao 2-0 na Azam FC.

Na leo usiku inapigwa mechi nyingine ya dabi hiyo, lakini ni katika mechi ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, mjini Unguja.

Lakini, kama haitoshi kesho pia kwenye uwanja huohuo kutakuwa na pambano jingine la kukata na shoka kwa Yanga kuvaana na Singida Black Stars katika nusu fainali nyingine inayokumbushia fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) iliyopigwa Juni, mwaka jana, visiwani hapa.

Kifupi ni kwamba mechi za nusu fainali zote za Kombe la Mapinduzi 2026 ni za kisasi, Simba ikiwa na kibarua mbele ya Azam na Singida dhidi ya Yanga ambayo usiku wa juzi ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya TRA United na kumaliza ikiwa kinara wa Kundi C.

Azam imetinga nusu fainali baada ya kuwa kinara wa kundi A ikimaliza na pointi saba baada ya kushinda mechi mbili dhidi ya Mlandege (2-0) na URA (2-1) na sare moja dhidi ya Singida Black Stars (1-1).

Kwa upande wa Simba, imemaliza kinara wa kundi B ikishinda mechi zote mbili ilizocheza dhidi ya Muembe Makumbi City (1-0) na Fufuni (2-1).

Rekodi zinaonyesha katika Kombe la Mapinduzi, timu hizi zimekutana mara saba tangu Azam FC ilipoanza kushiriki mwaka 2011.

Katika mechi hizo saba, hatua ya nusu fainali zimekutana mara tatu, mwaka 2012 ambapo Azam ilishinda 2-0, kisha mwaka 2013 Azam ikashinda kwa penalti 5-4 baada ya dakika tisini kuwa 2-2 na 2020 Simba ilishinda kwa penalti 3-2 baada ya muda wa kawaida matokeo kuwa 0-0.

Kwa ujumla, Azam imeshinda mechi tano dhidi ya mbili za Simba kwenye kombe la Mapinduzi.

Matokeo ya mechi hizo yapo hivi; Azam 2-0 Simba (nusu fainali 2012), Azam 2-2 Simba (Azam ikashinda kwa penalti 5-4 nusu fainali 2013), Azam 1-0 Simba (fainali 2017), Azam 1-0 Simba (makundi 2018), Azam 2-1 Simba (fainali 2019), Azam 0-0 Simba (Simba ikashinda kwa penalti 3-2 nusu fainali 2020) na Azam 0-1 Simba (fainali 2022).

Mara ya mwisho timu hizi zimekutana Desemba 7, 2025 katika Ligi Kuu Bara na Azam ikashinda 2-0 pale Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Safu ya ulinzi ya Simba ikiongozwa na Rushine De Reuck na Chamou Karaboue ambao walipumzishwa mechi iliyopita dhidi ya Fufuni, kutokana na ugumu wa mechi ya leo wanaweza kurudi kikosini.

Kikosi cha Simba kimepata nguvu baada ya kurejea kwa Jean Charles Ahoua na Jonathan Sowah ambao walikosekana mechi zote mbili za makundi, huku Elie Mpanzu akiiwahi moja iliyoipeleka Simba nusu fainali.

Azam ina mziki wake kamili, ukiachana na wale waliokuwa na kikosi cha Stars waliokwenda kushiriki AFCON akiwamo Feisal Salum, waliobaki ni watu wa kazi pia.

Jephte Kitambala anaongoza safu ya ushambuliaji huku akiwa miongoni mwa vinara wa mabao akifunga mawili.

Mshambuliaji huyu aliwaliza Simba mara ya mwisho walipokutana sambamba na Idd Nado ambaye anakosekana leo, lakini mpishi wa yale mabao ambayo Azam iliilaza Simba 2-0, Nassor Saadun yupo ndani ya nyumba licha ya kutocheza mechi hata moja ya Mapinduzi.

Kocha wa Simba, Steve Barker, amezungumzia mechi hiyo akisema ni kipimo kizuri kwake wakati huu akiwa anaijenga timu imara.

Kocha huyo Msauzi aliyetambulishwa kikosini hapo Desemba 19, 2025, hii ni mechi yake ya kwanza kukutana na Azam ambayo anafahamu mara ya mwisho Simba ililambishwa utamu ikiwa timu mwenyeji.

“Nafahamu tulipoteza mechi msimu huu dhidi ya Azam, kukutana na timu kubwa kama hii kipindi hiki kwangu inanipa motisha katika kujenga timu.

“Mechi hiyo itanipa picha ya kwamba tupo wapi hadi sasa katika maandalizi yetu kukabiliana na timu kubwa kama Azam kwa sababu tunafahamu mbele yetu tuna michezo mikubwa ya mashindano inakuja.

“Hata hivyo, ili tufanye vizuri lazima tucheze mchezo wa haraka, tuwe na mbinu bora zitakazorahisisha hiyo kazi.”

Kwa upande wa kocha wa Azam, Florent Ibenge, amesema: “Kila mechi imekuwa na changamoto yake, ukiangalia hatua ya makundi tumekutana na timu ngumu, sasa tunakwenda hatua ngumu zaidi kukutana na ushindani mwingine, tupo tayari kushindana tukiwa na malengo ya kubeba ubingwa na kuimarisha timu kuelekea mechi za CAF.”

YANGA v SINGIDA BLACK STARS

Baada ya Dabi ya Mzimma kupigwa, kesho kazi itakuwa tena palepale New Amaan Complex, Yanga ikicheza dhidi ya Singida Black Stars.

Hii ni mara ya kwanza Singida Black Stars inashiriki Kombe la Mapinduzi. Kumbuka timu hii ilikuwa ikifahamika kwa jina la Ihefu kabla ya kuuzwa na kuhamisha makazi kutoka Mbarali mkoani Mbeya hadi Singida.

Mara ya mwisho timu kutoka Singida kushiriki mashindano haya ilikuwa Singida Big Stars ambayo baadaye ikabadilishwa jina na sasa inaitwa Fountain Gate, imeweka ngome yake pale Manyara ikitumia Uwanja wa Tanzanite Kwaraa kwa mechi zake za nyumbani.

Sasa basi, ugeni wa Singida Black Stars katika Kombe la Mapinduzi si kitu, kwani imeonyesha ushindani mkubwa hadi kutinga nusu fainali.

Ikiwa kundi A, Singida Black Stars ilimaliza nafasi ya pili na pointi tano, ikishinda mechi moja dhidi ya Mlandege (3-1), kisha sare mbili dhidi ya Azam (1-1) na URA (1-1).

Singida Black Stars ilikuwa ya kwanza kufuzu nusu fainali, hivyo unaona si timu ya kubeza ukizingatia kwamba Septemba mwaka jana ilibeba Kombe la Kagame, mashindano yaliyofanyika jijini Dar es Salaam huku timu hiyo ikishiriki kwa mara ya kwanza.

Singida hivi karibuni imefanya mabadiliko ya benchi la ufundi kwa kumbadilishia majukumu aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Miguel Gamondi kuwa mkurugenzi wa ufundi, huku David Ouma aliyekuwa kocha msaidizi sasa akitambulika kama kocha mkuu, huku ikimuajiri Othmen Najjar kuwa meneja mkuu.

Licha ya kwamba ni mara ya kwanza zinakwenda kukutana katika Kombe la Mapinduzi, lakini Yanga na Singida Black Stars zinafahamiana vizuri, huku zikiwa zimepeana wachezaji kwa mkopo, Nickson Kibabage anacheza Singida akitokea Yanga, huku Mohamed Damaro, Frank Assinki na Marouf Tchakei wakitokea Singida na kutua Yanga.

Mara ya mwisho timu hizo zimekutana Juni 29, 2025 katika fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) iliyochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, hivyo mechi hii itakayopigwa kesho Ijumaa saa 2:15 usiku itakumbushia miezi sita iliyopita.

David Ouma ambaye aliiongoza Singida hatua ya makundi kama kocha msaidizi lakini sasa anaiongoza hatua ya nusu fainali akiwa kocha mkuu, amesema: “Hakuna kikombe ambacho tunashiriki hatuna malengo ya kushinda. Yanga ni timu nzuri, imekuwa ikitupa ushindani tunapokutana, lakini tumejipanga kukabiliana nayo na kuona tunafuzu fainali.”

Pedro Goncalves, kocha mkuu wa Yanga, amefichua kwamba: “Ili tuwe mabingwa tunapaswa kushinda kila mechi, tumefanya hivyo na tunatakiwa kuendelea kufanya hivyo mechi inayokuja.”

Wakati leo Alhamisi hatua ya nusu fainali ikianza, tulishuhudia makundi kukiwa na ushindani mkubwa zikipigwa mechi 12 zikihusisha timu kumi zilizopangwa katika makundi matatu.

Kundi A kulikuwa na Azam, Singida Black Stars, URA na Mlandege. Kundi B ni Simba, Muembe Makumbi City na  Fufuni wakati kundi C ni  Yanga, KVZ na TRA United.

Katika mechi hizo 12, yamefungwa mabao 26, huku mawili yakiwa ya kujifunga kutoka kwa beki wa KVZ, Rahim Andrea wakati wa mechi dhidi ya Yanga, huku KVZ ikichapwa 3-0.

Kwa upande mwingine, hadi sasa wanaoongoza kwa mabao ni Joseph Guede (Singida BS), Idrissa Diomande (Singida BS), Mboni Stephen Kibamba (Fufuni) na Jephte Kitambala (Azam) ambao kila mmoja ana mabao mawili.

Guede, Diomande na Kitambala, wana nafasi ya kuongeza mabao baada ya kutinga nusu fainali.

Katika hatua ya makundi, Morice Chukwu wa Singida Black Stars na Yakoub Said Mohamed wa Muembe Makumbi City ndio wachezaji waliobeba tuzo nyingi.

Chukwu amebeba tuzo mbili za Mchezaji Bora, alifanya hivyo katika mechi dhidi ya Mlandege na URA, wakati Yakoub akitunukiwa tuzo ya mchezaji aliyeonyesha mchezo wa kiungwana mara mbili dhidi ya Fufuni na Simba.

Katika kila tuzo ya mchezaji bora, mshindi hupewa kiasi cha Sh1 milioni, hivyo Chukwu amebeba Sh2 milioni. Kwa upande wa tuzo ya mchezaji aliyeonyesha mchezo wa kiungwana ‘Fair Play’, kila tuzo inaambatana na Sh500,000, kwa maana hiyo Yakoub amepata Sh1 milioni.

Kwa timu zote kumi katika Kombe la Mapinduzi 2026, Yanga ndiyo pekee nyavu zake hazijatikiswa ikiwa imeshuka dimbani mara mbili.

Hali hiyo inaonyesha safu yake ya ulinzi kuwa imara ambapo mechi ya kwanza iliposhinda 3-0 dhidi ya KVZ, safu hiyo iliundwa na kipa Aboutwalib Mshery, huku mabeki wakiwa Israel Mwenda, Chadrack Boka, Aziz Andabwile na Frank Assinki.

Mechi ya pili katika ushindi wa 1-0 dhidi ya TRA, Mshery aliendelea kukaa golini, Boka na Assinki kama kawaida walianza, huku Kibwana Shomary na Abubakar Othman ‘Ninju’ nao wakipata nafasi ya kuunda ukuta wa Yanga.