Depu, Yanga kimeeleweka, siku ya kutua yatajwa

KIKOSI cha Yanga kinaendelea kujiweka sawa kabla ya keshokutwa Ijumaa kuvaana na Singida Black Stars katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026, lakini mabosi wanajiandaa kuupokea ugeni mzito kutoka Ulaya.

Ndio! Kama unakumbuka juzi kati Mwanaspoti lilikupa taarifa kwamba kocha mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves ameachiwa jukumu la kuamua ashushe straika gani kati ya Waangola wawili ambao majina yalikuwa mezani kwa vigogo na uamuzi umetolewa kwamba Laurindo Dilson Maria Aurelio ‘Depu’ ndiye aje.

Hivi unaposoma ni kwamba nyota huyo wa timu ya taifa ya Angola yupo njiani kuja nchini kabla ya kupanda boti kwenda Zanzibar kati ya leo Alhamisi na kesho Ijumaa, baada ya klabu aliyokuwa akiichezea ya Radomiak Radom ya Poland kukubali kumuacha kufuatia biashara iliyoifanya na mabingwa wa soka Bara.

DEP 01

Taarifa ambazo Mwanaspoti limezinasa ni kwamba, Radomiak imekubali kupokea Dola 250,000 (zaidi ya Sh600 milioni) ili kumuachia Depu na kwamba, alikuwa njiani kuja nchini kujiunga na timu hiyo ili kuungana na Clement Mzize aliyerejea kutoka katika majeraha pamoja na Prince Dube.

Depu anakuja kuziba pengo la Andy Boyeli aliyerejeshwa katika klabu yake ya Sekhukhune United ya Afrika Kusini iliyomtoa Jangwani kwa mkataba wa mkopo wa mwaka mmoja, lakini ameutumikia kwa nusu msimu na kushindwa kufanya maajabu.

Mwanaspoti lilisharipoti ujio wa mshambuliaji huyo  Yanga likiwa ni pendekezo la Goncalves ambaye aliuomba uongozi kuongezewa nguvu katika eneo hilo baada ya taarifa ya kuumia kwa Mzize, na uongozi wa Yanga umefanikisha dili hilo ambapo Depu inaelezwa tayari ameaga huko Radomiak.

DEP 02

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga kimeliambia Mwanaspoti kuwa mshambuliaji huyo wakati wowote atatua nchini kuungana na kikosi ili kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji.

“Ilikuwa ni lazima dili hilo likamilike kwa sababu ni pendekezo la kocha. Ni mchezaji ambaye anamfahamu na ameshawahi kufanya naye kazi, hivyo tunaamini ni mchezaji mzuri ataisaidia timu yetu kufikia malengo kwenye mashindano yote ya ndani na kimataifa,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:

“Usajili wa mshambuliaji huyo licha ya kuwa mbadala wa nyota aliyetoka ni sehemu ya maboresho ya timu ambayo ina wachezaji wengi bora, lakini wana uchovu kutokana na mafanikio ya misimu minne mfululizo, hivyo ilikuwa ni lazima kuongeza nyota wengine.”

Chanzo hicho kilisema mchezaji huyo ni sehemu ya wachezaji waliokuwa wamependekezwa kusajiliwa dirisha hili na dili lake limeenda vizuri, huku matarajio yakiwa makubwa kutoka kwake kwani tangu ameondoka Fiston Mayele bado hajapatikana mshambuliaji bora wa aina yake.

Depu akiwa na Angola alikuwa mfungaji bora wa Cosafa, kwani ndani ya mechi tano alizocheza alifunga mabao manane wakati katika Ligi Kuu Poland akiwa na Radomiak amecheza mechi tisa akifunga bao moja na asisti moja.

DEP 03

Mwanaspoti lilimtafuta Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe na kumuulizia juu ya taarifa za Depu, naye alijibu kwamba klabu inajiandaa kupokea mshambuliaji mpya bila kutaja jina lake.

“Kati ya kesho (leo) Alhamisi au Ijumaa Yanga inatarajia kumpokea mshambuliaji mpya matata, ila siwezi kutaja jina kwa sasa,” amesema Kamwe.

Yanga iliyomaliza kama kinara wa Kundi C katika michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya kuifunga TRA United kwa bao 1-0, keshokutwa Ijumaa itashuka kwenye Uwanja wa New Amaan kuumana na Singida Black Stars ikiwa ni siku moja baada ya watani wao, Simba, kupepetana na Azam FC katika nusu fainali nyingine inayopigwa kesho Alhamisi.