KMC yakomba noti usajili wa Pipino

KMC imeingiza zaidi ya Sh70 milioni baada ya aliyekuwa kiungo wa kikosi hicho, Ahmed Bakari Pipino kuvunja mkataba wa miaka miwili uliobaki, huku akikamilisha taratibu za kujiunga na Singida Black Stars.

Nyota huyo amekamilisha kujiunga na Singida baada ya kuomba uongozi umruhusu akatafute changamoto mpya, ambapo mabosi wa kikosi hicho waliridhia ombi hilo, ingawa kwa sharti la kuulipia mkataba uliobaki.

Chanzo kutoka KMC kimeliambia Mwanaspoti kuwa mchezaji huyo alikuwa na mazungumzo na viongozi pamoja na benchi la ufundi kujadili ofa ya Singida, ndipo wakaridhia kumuacha baada ya dirisha lililopita kumzuia kwenda Simba.

Nyota huyo alikuwa akihusishwa kujiunga na Simba jambo lililosababisha pia mgogoro kati ya uongozi wa KMC na mchezaji mwenyewe, ingawa safari hii imeona ni vyema kumuachia baada ya makubaliano.

“Ni uamuzi uliofanyika kwa kuzingatia maslahi ya mchezaji kwa sababu kuna leo na kesho. Tulimhitaji sana, lakini baada ya kusikiliza mahitaji yake tuliona ni vyema tukamuachia ili akapate changamoto sehemu nyingine,” kilisema chanzo hicho.

Pipino alianza maisha ya soka katika akademi ya vijana ya Magnet kwa miaka minane hadi kupata nafasi ya kujiunga  na akademi ya Celta Vigo ya Hispania 2022 kisha akarejea nchini na kuviteka vigogo.

Nyota huyo alijiunga na KMC katika dirisha dogo la Januari 2025 akitokea akademi ya Magnet, akiwa ni mchezaji wa pili kutoka kwenye kikosi hicho cha Kinondoni kujiunga na Singida baada ya beki wa kati, Abdallah Said Ali ‘Lanso’.