Shauri atamani kuvunja rekodi binafsi riadha

MWANARIADHA wa kimataifa wa Tanzania, Magdalena Shauri amesema anataka kuvunja rekodi yake ya taifa ya marathoni kwa wanawake akilenga kukimbia chini ya saa 2:18 katika mashindano yajayo ya kimataifa.

Shauri aliweka historia 2023 baada ya kuvunja rekodi ya taifa katika Berlin Marathon, Ujerumani, ambapo licha kumaliza nafasi ya tatu alitumia saa 2:18:41, muda ambao haujawahi kufikiwa na mwanariadha yeyote wa kike wa Tanzania.

Rekodi hiyo haikudumu kwa muda mrefu kwani baada ya miaka miwili aliiboresha 2025 kupitia Chicago Marathon, Marekani akimaliza nafasi ya tatu kwa muda wa saa 2:18:03, akiiboresha rekodi yake kwa sekunde 38.

Mbali na mafanikio ya Chicago, Shauri pia alinga’ara 2025 baada ya kushinda Sharqiyah International Half Marathon nchini Saudia Arabia, akimbia kilomita 21 kwa muda wa saa 1:12:47, matokeo yaliyoongeza imani yake ya kuendelea kushindana na wanariadha wakubwa duniani.

“Nilipokimbia Berlin niliona wazi kwamba naweza kushindana na wanariadha wa mataifa makubwa. Nikamuomba Mungu nirudi tena na nifanye kama wanavyofanya wanariadha wa Kenya na Ethiopia.

“Natamani kuwa miongoni mwa wanariadha wa kimataifa, na nikifika kwenye mbio wajue na mimi ni bingwa,” amesema Shauri.

Akieleza siri ya mafanikio yake, Shauri amesema jitihada binafsi, kumsikiliza kocha wake Antony Mwingereza pamoja na ushirikiano anaoupata kutoka kwa waajiri wake, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania vimekuwa nguzo muhimu katika safari ya riadha, pia anapata nafasi ya kutosha ya mazoezi na kuiwakilisha Tanzania vyema kimataifa.

Aliongeza kuwa lengo lake kubwakwa sasa ni kuvunja tena rekodi hiyo kwa kukimbia chini ya saa mbili na dakika 18, akiamini ndoto hiyo ipo karibu kutimia kutokana na maendeleo makubwa anayoyaona katika mazoezi na mashindano aliyoshirikia siku za karibuni.

Kocha Thomas John aliyemfundisha Shauri tangu akiwa sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi nne, amesema mafanikio ya nyota huyo yanatokana na nidhamu, uwezo wa kusikiliza maelekezo na kukubali kukosolewa.

Mbali na rekodi ya taifa ya marathoni, Shauri pia anajivunia yake binafsi ya saa 1:06:37 katika mbio za nusu marathoni aliyoiweka 2020 kupitia mbio za Ras Al Khaiman Half Marathon katika Falme za Kiarabu pamoja na muda wa dakika 32 sekunde 40 wa mbio za kilomita 10 alioupata 2016 jijini Marrakech nchini Morocco katika mashindano ya huko.