Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau imeeleza inakusudia kuifanyia mabadiliko idara ya uhamiaji nchini.
Maboresho hayo yametajwa kuwa mkakati wa kuendelea kuboresha sekta ya utalii ambayo imekuwa nyenzo muhimu ya uchumi wa nchi.
Mabadiliko hayo yametajwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene katika kikao chake na Maofisa wa Uhamiaji kilichofanyika Visiwani Zanzibar jana Jumatano, Januari 7, 2026.
Akizungumza katika Kikao hicho, Waziri Simbachawene amesema maofisa uhamiaji ni watu muhimu nchini kwa kuwa ndio wa kwanza mtalii au mgeni anapoingia nchini anakutana nao.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akizungumza na Maofisa wa Uhamiaji baada ya kikao kilichofanyika Visiwani Zanzibar jana Jumatano, Januari 7, 2026.
Amesema ikiwa maofisa utalii watakosa ukarimu na mapokezi mema kwa watalii sekta hiyo inaweza ikakosa mafanikio na hivyo kulinyima Taifa fursa ya mapato yanayotokana na sekta hiyo.
Amesema Sekta hiyo imekuwa ikikua kila mwaka hivyo juhudi zinatakiwa kuchukuliwa ili kujenga mazingira rafiki kwa watalii wanapoingia nchini.
“Sekta ya utalii imeliingizia Taifa watalii 1,924,240 mwaka 2024 huku mwaka 2025 wakifikia 2,097,823 ikiwa ni ongezeko la watalii 173,583,” amesema.
Akitaja sababu ya kupendekeza ajira ya uhamiaji kuhusisha taaluma ya utalii, Simbachawene amesema itawasaidia maofisa hao kuwa wakarimu pindi wanapotoa huduma kwa wageni wakiwemo watalii ambao amesema huliingizia Taifa kiasi kikubwa cha fedha.
Akitaja mapato ya Sekta ya Utalii, amesema kwa mwaka 2024 sekta ya utalii ililiingizia Taifa Sh10.14 trilioni jambo linalofanya sekta ya utalii kuwa moja ya nguzo muhimu za uchumi wa Tanzania.
‘’Mgeni yeyote anapoingia nchini anakutana na ofisa uhamiaji, anamwambia karibu na anapoondoka anaagana naye, ninyi ndio sura ya Tanzania, ndio mmebeba ukarimu wetu na utamaduni wetu, hivyo mnapaswa kuwa mfano wa kuigwa,” amesisitiza Simbachawene.
Akitaja kiwango cha elimu, Simbachawene ameweka mkazo elimu ya ofisa uhamiaji hata askari wa kawaida lazima iwe diploma na kuendelea, akitaja sababu hao ni wanadiplomasia na wanatakiwa wajue mambo mengi ikiwemo lugha fasaha ya kuongea na mtalii au mgeni anayeingia nchini.
‘’Unatakiwa ujue lugha zaidi ya moja, kinyume na hapo hautafika katika ngazi za hawa makamishna, wao walipita njia tofauti lakini kwa nyie vijana someni kwa sababu kufika huku baadaye patakua pagumu, tunataka pale anapotokea mgeni ofisa uhamiaji awe anaweza kuongea kiarabu, kachina, kifaransa na Kiingereza,” amesema.
Amesema mtu mwenye sifa hizo atafanya kazi vyema kutokana na uwezo wa kitaaluma wa kujiendeleza lakini pia atatakiwa awe na uwezo wa kuwasiliana na mgeni sambamba na kujifunza masuala ya masoko ya utalii.
Ameongeza ofisa uhamiaji aliyesoma utalii atafundishwa na kuvijua vivutio vya utalii vilivyopo nchini ili aweze kuwa balozi mzuri wa kuwapa taarifa sahihi watalii anapowapokea.
Akizungumza katika kikao hicho, Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, Hassan Ally Hassan amesema idara hiyo inaendesha miradi mbalimbali katika kuimarisha mazingira ya utendaji kazi visiwani humo akitaja miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa Ujenzi ya Ofisi na makazi bora ya maafisa na askari uliopo Micheweni, Pemba Kaskazini, Ofisi ya Mkoa wa Mjini Magharibi.
Pia amesema idara hiyo inaendelea kuimarisha ujenzi wa Chuo cha Uhamiaji uliopo Kitogani na Ofisi ya wilaya ya Uhamiaji iliyopo Paje.
