Venezuela tayari ipo kwenye unyayo wa Marekani. Wanajeshi wa Venezuela wanapiga mayowe kukataa uvamizi, lakini sauti zao hazipenyi kwenye masikio ya Rais wa Marekani, Donald Trump. Huwezi kupata haki kidiplomasia mbele ya mtu dhalimu.
Sasa, utajiri wa Venezuela unajadiliwa The Oval. Yaani, ndani ya ofisi ya Rais wa Marekani, Ikulu, White House. “Mapipa milioni 50 ya mafuta ya Venezuela, yatauzwa Marekani na fedha nitasimamia mimi,” ni kauli ya Trump. Kabla ya hapo alisema: “Wafanyabiashara wa mafuta wa Marekani, watafanya biashara Venezuela kwa miezi 18.”
Venezuela ikiwa tayari imeshapigishwa magoti, mjadala upo Greenland. Kisiwa kikubwa zaidi ulimwenguni. Greenland ni mamlaka ndani ya nchi ya Denmark. Trump anataka kuitwaa Greenland iwe chini ya Marekani.
Greenland ina ukubwa wa kilomita za mraba milioni 2.2. Inaweza kulingana na nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) au Saudi Arabia.
Uchumi wa Greenland, kwa miaka yote, unategemea shughuli za uvuvi, pamoja na ruzuku kutoka Denmark.
Ipo nuru ing’aayo Greenland miaka ya karibuni. Ni nuru ya rasilimali. Imegundulika kuwa Greenland ina utajiri mkubwa wa madini adimu, vilevile uranium na chuma. Ni hiki ndicho kinamfanya Trump atake kuitwaa Greenland.
Hata hivyo, Trump anasema; “Tunaihitaji Greenland kwa ajili ya usalama wa taifa, siyo madini. Greenland imezingirwa na meli za Urusi na China.” Nukuu hiyo ya Trump ikukumbushe kuwa operesheni ya uvamizi Venezuela ilibeba ujumbe kuwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Nicolas Maduro ni muuza dawa za kulevya na alikuwa akiingiza Marekani kiwango kikubwa cha dawa za kulevya.
Baada ya kufanikiwa kumtwaa Maduro na mkewe, Cilia, kisha kuwasafirisha hadi New York na kuwafungulia kesi za kuhusika na usafirishaji wa dawa za kulevya, habari kuu kwa sasa ni jinsi Marekani inavyonufaika na utajiri wa mafuta ya Venezuela.
Venezuela huenda ikawa kama Greenland!
Wakati ukiiwazia kesho ya Greenland, usisahau nadharia ya Trump ya kuifanya Canada kuwa jimbo la 51 la Marekani. Kwa sasa, na kwa karne zaidi ya mbili, Marekani inatambulika kuwa ni nchi ya muungano wa majimbo 50 na Trump anataka kuiongeza Canada.
Kuna vitisho pia vya Trump kuzivamia Colombia na Nigeria. Hatua kwa hatua kuhusu Trump, unamwona binadamu ambaye anataka kudhihirisha kwamba yeye ndiye binadamu mwenye nguvu kuliko yeyote ulimwenguni.
Ni binadamu mwenye mawazo yaliyoshindwa tangu zama za Kabla ya Kalenda (BC), yakaibuliwa tena enzi za kizazi cha ukimya (silent generation), matokeo yake ikatokea Vita Kuu ya Pili ya Dunia (WWII).
Karne nne kabla ya ujio wa kalenda, Ugiriki ya Kale ilitawaliwa na Alexander III of Macedon, kwa umaarufu zaidi alifahamika kama Alexander the Great.
Alexander aliunda jeshi lake na kutangaza azma yake ya kutawala dunia akitokea Ugiriki, kwamba dunia nzima ingefuata amri zake. Viongozi wa dola nyingine wawe kama magavana wenye kufuata maagizo yake.
Nyakati hizo Alexander the Great alikuwa anajidanganya. Ulimwengu wa kijima wakati huo, angeweza vipi kuifikia dunia yote? Akiwa Ugiriki hakuwa akijua chochote kuhusu nguvu za China na maeneo mengine.
Hata hivyo, Alexander anabaki kuwa mfano hai wa ulimwengu na walimwengu. Ni kipimo cha akili kwa dunia na busara za watu wake. Kwamba nyakati zote tamaa za kutawala dunia zimeendelea kuwepo.
Taifa moja linakuwa na sera ya kutaka kutawala dunia. Wakuu wa mataifa mengine wawe wafuata maagizo. Taifa moja linakuwa na mipango endelevu ya kutawanya mabavu yake ya kijeshi duniani ili kumiliki uchumi wa dunia.
Unapokuwa na uchumi imara pamoja na uwezo mkubwa wa kijeshi, dunia utaielekeza upande wako. Na hapo ndipo mahali akili ya Trump imelalia. ‘Miguvu’ ya Marekani kijeshi, inampa mzuka wa kujiona anaweza kuitawala dunia. Hatanii!
Trump ni muumini wa hegemony, yaani nadharia ya dola moja kuongoza nyingine kisiasa, kiuchumi na kijeshi. Taifa moja linakuwa kiranja wa mataifa mengine duniani. Trump anadhani kuwa Marekani ikiitawala dunia, yeye ndiye atakuwa bosi wa ulimwengu.
Ni mawazo hayohayo aliyokuwa nayo Kansela wa zamani wa Ujerumani, Adolf Hitler. Kupitia mpango wa kuunda dola kubwa ya Greater Germany Reich akilenga kutaka kuitawala dunia, matokeo yake ulimwengu ukaingia kwenye vita. Ulaya ikawa nyang’anyang’a kutokana na athari za mabomu.
Mahangaiko ya Trump yanakufanya uwaone Alexander The Great na Hitler, ndani yake. Dunia ya teknolojia, inashangaza Rais wa nchi bado ana mawazo ya kijima, kuvamia mataifa mengine, kuangusha dola zao, kubadili utawala, kisha kuyaendesha mataifa, mithili makabiliano ya himaya kwa himaya zaidi ya miaka 700 iliyopita.
Trump aliapishwa kuiongoza Marekani kwa muhula wake wa pili, Januari 20, 2025. Haikupita miezi miwili tangu alipoapishwa, maneno kuwa Trump alikuwa na mpango wa kugombea urais kwa muhula wa tatu yalianza.
Machi 2025, Trump alipoulizwa kama alihusika na maneno hayo ya muhula wa tatu, alijibu: “Ningependa iwe hivyo!” Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya mtandao wa BBC, Machi 31, 2025, ambayo waliihuisha Oktoba 27, 2025.
Aprili 2025, kambi ya Trump ilitoa kofia na kuziuza kwa dola 50, kila moja. Kofia hizo zimeandikwa “Trump 2028”, kwa maana ya kuwaandaa Wamarekani kwamba Uchaguzi wa Rais Marekani 2028, Trump atakuwa kwenye kinyang’anyiro.
Katiba ya Marekani ya mwaka 1789, katika mabadiliko yake ya 22 mwaka 1951, imeweka marufuku kwa mtu aliyechaguliwa kuwa Rais wa taifa hilo kwa mihula miwili, kuwania muhula wa tatu. Trump kupitia mahojiano yake na NBC News, alisema: “Ipo njia ya kufanikisha.”
Dhahiri, Trump haoni akifanikisha lengo lake la kuitawala dunia ndani ya muhula wake mmoja, kwa hiyo anataka kuongeza muhula wa tatu na ikiwezekana wa nne. Hilo la kuwa Rais wa Marekani hadi muhula wa nne ameshalitamka. Ipo siku atatamka pia kuhusu kuitawala dunia.
Kwa Marekani, Rais pekee ambaye amewahi kutawala zaidi ya mihula miwili ni Rais wa 32 wa nchi hiyo, Franklin Delano Roosevelt (FDR). Roosevelt alichaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1932, akachaguliwa mara ya pili mwaka 1936, kisha 1940 na 1944. FDR alifariki dunia Aprili 12, 1945, ikiwa ni miezi mitatu kasoro siku nane, tangu alipoapishwa kuwa Rais kwa muhula wa nne.
Miaka sita baada ya kifo cha FDR, Katiba ya Marekani ilifanyiwa marekebisho na kuwekwa ibara ya ukomo wa uongozi.
Kabla ya FDR, Marekani ilienda kiutamaduni wa ukomo wa mihula wa miwili, tangu Rais wa Kwanza wa Marekani, George Washington alipokataa kuongoza nchi hiyo kwa muhula wa tatu.
Utamaduni huo ulioanzishwa na Washington, ulivunjwa na FDR, kisha ukadhibitiwa kikatiba mwaka 1951. Trump anasema ipo njia!
