127 wagundulika kuwa na mabusha Dar

Dar es Salaam. Wanaume 127 kati ya 165 waliofanyiwa uchunguzi  wa mabusha mwezi huu jijini Dar es Salaam wamegundulika kuwa na ugonjwa huo.

Hata hivyo 27 kati ya waliogundulika kuwa na mabusha tayari wamefanyiwa upasuaji na wanaendelea vizuri.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 8, 2026 wakati wa kutangaza kambi ya uchunguzi na ufanyaji upasuaji wa mabusha bure iliyoanza Januari 5, 2026, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Mohamed Mang’una amesema wagonjwa hao waligundulika baada ya kufanya uchunguzi katika kambi hiyo inayoendelea.

Amesema  katika kambi hiyo, watafanya  uchunguzi na upasuaji  bure hadi Januari 30, 2026.

“Baada ya muda huo, wale watakaohitaji kufanyiwa upasuaji wataendelea na utaratibu wa kuchangia kama kawaida,” amesema.

Akizungumza hali ya ugonjwa huo ulivyo, amesema tatizo lipo sana katika mikoa ya ukanda wa Pwani kuanzia Mtwara.

“Hii haimaanishi mtu wa mkoa mwingine hawezi kupata, lakini kwa ukanda wa Pwani ndipo wagonjwa wapo sana.

“Katika kambi ya uchunguzi, pamoja na kwamba inayofanyika Dar es Salaam, tumepata watu kutoka mikoa ya Morogoro, Pwani na mmoja Lindi,” ameongeza.

Awali Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yasiyopewa Kipaumbele, Dk Clara Mwansasu amesema mkakati uliopo ni ifikapo 2030 kusiwe na halmashauri yenye maambukizi ya mabusha.

Akilizungumzia hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saadi Mtambule amesema kambi hiyo ya uchunguzi na upasuaji imelenga kuwafikia watu 500.

Amesema kambi hiyo itafanyika Kilakara Health Centre,Temeke na Kinondoni Health Centre, Kinondoni zikilenga kusaidia wakazi wote wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Amesema lengo ni kusaidia kuwakinga na kutoa huduma ya upasuaji wa mabusha katika kipindi cha mwezi mmoja.

“Nitoe hamasa, rai kwa wananchi wa maeneo mengine kuja kufanya uchunguzi na kuangalia kama wana changamoto ili kupatiwa matibabu kutoka kwa wataalamu,”amesema

Amesema magonjwa hayo huchukua muda mrefu kujionesha kwa hiyo ni vyema   wananchi  kujitokeza  kufanyiwa uchunguzi ili kufahamu changamoto na   kutoona aibu kwenda kufanyiwa upasuaji baada ya kugundulika kuwa wana matatizo hayo.