Bunge la Seneta lamjia juu Trump sakata la Venezuela

Dar es Salaam.  Bunge la Seneta nchini Marekani limewasilisha muswada wa kukomesha kufungwa kwa serikali ya Venezuela.

Uamuzi huo umekuja siku chache baada ya vikosi vya Marekani kumkamata Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro katika shambulio la kijeshi tukio ambalo limepingwa na  baadhi ya wabunge wa Seneta wakiituhumu serikali kwa kulipotosha Bunge juu ya sababu ya kukamatwa kwake.

Maseneta hao wameeleza kuwa lengo la muswada huo ni kupinga hatua za Trump juu ya matumizi ya nguvu za kivita zilizoanzishwa tangu utawala huo ulipoongeza shinikizo la kijeshi nchini humo, kwa mashambulizi dhidi ya boti karibu na pwani yake Septemba mwaka jana.

Muswada huo unalenga kumzuia Donald Trump kuchukua hatua zaidi za kijeshi dhidi ya Venezuela bila idhini ya bunge, huku wabunge wanaounga mkono wakisema kuwa hatua hiyo Italiheshimisha taifa hilo na kuwezesha matumizi ya sheria kushughulika na madai hayo.

Miongoni mwa Wabunge wanaounga mkono muswada huo, Rand Paul amesema kuwa kupitishwa kwa muswada huo ni hatua muhimu ya kusitisha matumizi makubwa ya mamlaka ya kivita dhidi ya mataifa mengine.

“Siwezi kukuhakikishia jinsi watakavyopiga kura, lakini hatua hii itaweka msingi wa matumizi ya njia bora katika kusimamia sheria ili kuimarisha ukaribu baina yetu na mataifa mengine,” amesema Paul.

Amesema Maseneta wanapinga azimio la mamlaka ya vita na wanaona kukamatwa kwa Maduro kuwa  si hatua ya kutekeleza sheria bali ni operesheni ya kivita dhidi ya mashtaka ya dawa za kulevya na bunduki, anayodaiwa kuwa nayo rais Maduro.

Hatua hii imepingwa na baadhi ya maseneta kutoka chama cha Republican ambao  walionekana kuzuia hatua zote, licha ya kupigwa kwa kura hizo  na kushuhudiwa maseneta wawili kutoka chama cha Trump wakiungana  na wa kutoka chama cha Democratic ili kuunga mkono azimio hilo.

Bunge hilo pia limeonyesha wasiwasi kuhusu kampeni ndefu na ghali ya mabadiliko ya utawala nchini Venezuela kutokana na hatua za Trump alizotagaza Jumatano katika tovuti yake ya Truth Social, kwamba alitaka bajeti ya kijeshi ya Marekani iongezeke hadi dola trilioni 1.5 kutoka dola trilioni 1.

Bunge hilo pia limemtaka rais huyo kuzingatia katiba ya Marekani ambayo inamtaka rais yeyote kupata idhini ya Bunge, kabla ya kuanzisha operesheni ya kijeshi ya muda mrefu.