Wadau walalamikia kanuni za kudhibiti uchovu wa madereva

Dar es Salaam. Wadau wa usafirishaji wametoa maoni kwa baadhi ya vipengele vya Kanuni za Kudhibiti Uchovu wa Madereva za mwaka 2026, wakisema vinawakandamiza madereva na wamiliki kutokana na changamoto kadhaa za kisheria na kiutendaji zinazopaswa kufanyiwa kazi kabla ya kanuni hizo kupitishwa.

Kifungu cha 45(2)(1) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, Sura ya 413, kinampa mamlaka waziri mwenye dhamana ya usafiri ardhini kutengeneza kanuni ili kutekeleza majukumu yaliyoainishwa katika Sheria, huku Kifungu cha 6 kikihusu usalama wa huduma zinazodhibitiwa na kulinda mtumiaji wa huduma.

Akizungumza leo Alhamisi, Januari 8, 2026, Mjumbe wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Elinas Kitua, amesema licha ya nia njema ya Serikali ya kudhibiti ajali zinazotokana na uchovu wa madereva, bado kuna changamoto kadhaa za kisheria na kiutendaji zinazopaswa kushughulikiwa kabla ya kanuni hizo kupitishwa.

Amesema Taboa na wadau wengine wamefanya utafiti shirikishi unaoonesha baadhi ya mapendekezo yaliyomo kwenye rasimu ya kanuni yanaweza kusababisha madhara makubwa endapo yatawekwa bila maboresho.

“Si kila kanuni ikitungwa lazima iwe suluhisho. Tuna uzoefu wa kanuni nyingi zilizopita, baadhi zimepitishwa lakini hazijawahi kuleta matokeo yaliyokusudiwa, na nyingine zimesababisha changamoto mpya kuliko faida,” amesema Kitua.

Ameeleza wasiwasi kuhusu baadhi ya vifungu vinavyohusu usajili wa madereva, akisema hatua hiyo inaweza kuonekana nzuri kwa nadharia, lakini kwa uhalisia inaweza kuwa na athari hasi zaidi kuliko chanya.

“Ukichunguza kwa kina, usajili wa madereva unaweza kuwabagua wenye uzoefu mkubwa lakini wasio na ujuzi wa teknolojia au elimu rasmi, huku ukimpa nafasi mtu asiye na uzoefu wa kutosha lakini anayejua kutumia mifumo ya kielektroniki,” amesema.

Amesema uendeshaji wa gari unahitaji zaidi uzoefu na nidhamu barabarani kuliko uwezo wa kutumia mifumo ya kidijitali pekee.

Mjumbe huyo amesema tafsiri ya neno ‘uchovu’ katika rasimu ya kanuni imejaa mkanganyiko wa kisheria, jambo linaloweza kuleta tafsiri tofauti wakati wa utekelezaji.

Baadhi ya tafsiri zinaeleza uchovu kama hali ya kutokuwa makini au kutotulia, lakini bila kuwekwa mipaka ya wazi, utekelezaji wake unaweza kutegemea mtazamo wa mtu mmoja mmoja.

“Kama tafsiri haitakuwa wazi, kila mtekelezaji atatumia akili yake mwenyewe kumhukumu dereva kama amechoka au la, na hapo ndipo migogoro na malalamiko yataanzia,” amesema.

Pia, amegusia kifungu kinachopendekeza dereva asiendeshe gari zaidi ya saa nane mfululizo, akisema bado hakijafafanuliwa vizuri maana ya ‘mfululizo.’

“Je, ni saa nane tangu safari ianze bila kusimama, au ni saa nane ndani ya safari yenye vituo na mapumziko? Bila ufafanuzi, dereva anaweza kujikuta anashtakiwa kwa tafsiri isiyo wazi,” amesema.

Kwa mtazamo wake, ingekuwa vyema zaidi kuweka vipimo vya umbali (kilomita) badala ya muda pekee, ili kuendana na uhalisia wa safari za barabara zenye vituo, foleni na mapumziko.

Hata hivyo, amepongeza wazo la kanuni kuweka wajibu kwa dereva na mtoa huduma, lakini akasisitiza kuwa wajibu huo unapaswa kuandikwa kwa lugha iliyo wazi na isiyoacha mianya ya kisheria.

“Kama dereva anawajibika na mtoa huduma pia anawajibika, basi kanuni ieleze wazi nani awajibike katika mazingira gani, ili kuepuka lawama zisizo na mwisho,” amesema.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (Latra), Habibu Suluo, amesema uchovu wa madereva ni miongoni mwa sababu kubwa zinazosababisha ajali za barabarani, ambazo zimekuwa zikigharimu taifa kwa kupoteza maisha, kuacha watu wakiwa ulemavu wa kudumu, na kuongeza gharama za matibabu.

“Dereva anapochoka na kuendelea kuendesha gari, hatari ya ajali huwa kubwa. Ajali ikitokea, tunapoteza uhai wa watu, wengine wanapata ulemavu, na taifa linaingia gharama kubwa za matibabu na kupoteza nguvu kazi,” amesema Suluo.

Amesema kanuni hizo mpya zinalenga kuweka mifumo madhubuti ya kudhibiti muda wa kazi na mapumziko ya madereva, usimamizi wa ratiba za safari, pamoja na wajibu wa waajiri na wamiliki wa vyombo vya usafiri katika kuhakikisha usalama unazingatiwa.

Kwa mujibu wa Suluo, Serikali imeona umuhimu wa kuchukua hatua mapema ili kuzuia madhara makubwa yanayotokana na uchovu wa madereva, hususani katika usafiri wa masafa marefu na usafirishaji wa mizigo.

“Lengo la Serikali si kuwakomoa wawekezaji, bali kulinda mitaji yao, kulinda afya na usalama wa madereva, na zaidi kulinda uhai wa wananchi,” amesema.

Ameongeza kuwa uchovu wa madereva hauathiri tu usalama barabarani, bali pia unaongeza hasara za kiuchumi, ikiwamo uharibifu wa vyombo vya usafiri, miundombinu na kupotea kwa rasilimali za taifa.

LATRA imesisitiza mchakato huo ni wa ushirikishwaji kabla ya kanuni kuanza kutumika rasmi mwaka 2026.

“Tunaweza kujadiliana, kutofautiana, lakini mwisho wa siku tunakubaliana kuwa usalama wa watu na rasilimali za taifa ni jambo la kwanza,” amesema Suluo.

Kaimu Naibu Katibu wa Umoja wa Madereva wa Coaster za Kukodi Dar es Salaam (Special hire), Issa Kisalu, amesema mazingira ya kazi, ikiwamo foleni, magari makubwa yanayotembea polepole na msongamano barabarani, huchangia dereva kuchoka hata katika safari fupi, jambo linalopaswa kuzingatiwa kabla ya kumtuhumu dereva kwa uchovu.

Amesema katika kanuni hiyo kuna kipengele cha 10(k) kinachowataka mtoa huduma kuhakikisha dereva mwenza hayumo ndani ya gari lilelile linalotarajiwa kubadilishana iwapo magari yatakayopita katikati ya jiji, jambo litakalotaka kuajiri madereva wengi katika kila mkoa.

“Hii itatupa wakati mgumu, inabidi tajiri aajiri madereva wengi katika kila mkoa jambo ambalo haliwezekani maana itasababisha gharama ya usafiri kupanda zaidi na kumtoza mteja nauli kubwa. Mfano kutoka Dar es Salaam hadi Tanga tutafanya Sh20 milioni, jambo ambalo si sawa,” amesema Kisalu.

Kwa upande wake, mmiliki wa magari ya Kimotco, Benedict John, amesema wamiliki wa magari na madereva wanalazimishwa kubeba mzigo wa uamuzi ambao haujazingatia uhalisia wa kazi zao.

Amesema iwapo Latra na Wizara ya Uchukuzi zinaona umuhimu wa kudhibiti uchovu wa madereva kwa kutumia vifaa maalumu, basi vifaa hivyo vinapaswa kufungwa kwenye mifumo ya Serikali, si kuwalazimisha wafanyabiashara kununua na kufunga kwa gharama zao.

“Kama airport kuna mashine za kukagua abiria, kwanini msifunge hizi mashine zenu kwenye vituo vya Serikali? Kwa nini mzigo wote mnatutwisha sisi?” amehoji.

Mwanasheria wa Wizara ya Uchukuzi, Manchare Suguta, amesema Serikali haijatunga kanuni hizo kwa nia ya kuwabana au kuwaonea madereva, bali kulinda uhai wao na wa watumiaji wengine wa barabara.

“Hakuna sheria inayokuja kwa lengo la kuumiza. Kanuni hizi hazikusudiwi kukusanya faini au kuadhibu madereva, bali kuzuia ajali zitokanazo na uchovu, ambazo kila siku tunazishuhudia, hasa zinazohusisha malori na mabasi,” amesema.

Amesema mkutano huo haukulenga kupitisha kanuni bila kusikiliza wadau, bali ni jukwaa la kukusanya maoni, yakiwemo yale yanayotishia migomo, ili yafanyiwe kazi kabla ya kanuni kuanza kutumika rasmi.

“Hatujaalika watu hapa ili tuwapuuze, tumekuja kusikiliza, kubishana na kupata suluhu ya pamoja. Hoja zote zitafikishwa kwa viongozi wakuu wa Serikali kwa ajili ya maamuzi,” amesema.

Suguta amewahimiza madereva kuwa wavumilivu na kushiriki kikamilifu katika mijadala ya kitaalamu, akisema kulinda usalama barabarani ni jukumu la wote na si la upande mmoja.

Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Usafirishaji wa Barabara, Andrew Magombana, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, amesema maoni yaliyotolewa wameyachukua na kuyafanyia kazi, na wakiona kama kanuni bado muda wake watasubiri.

“Sitaki kuamini kuwa kanuni hii haifai, tutakaa na kujadili vipengele ambavyo vimetolewa, vitaondolewa na tutarejesha kwenu. Pia bado kuna nafasi ya siku 14 ya kutoa maoni kwa maandishi, ambalo ni jambo muhimu zaidi,” amesema Magombana.