Dar es Salaam. Msingi wa maisha ya ndoa katika Uislamu ni upendo, kaulimbiu yake ni huruma na maelewano. Maisha ya ndoa katika Uislamu siyo tu kuizuia nafsi na tamaa ya mwili, wala si starehe pekee; bali ni jambo kubwa zaidi kuliko hayo.
Ni kushirikiana katika kujenga na kukuza. Ni hisia za kubadilishana mawazo yaliyoundwa na uhusiano wa karibu na upendo wa kina wa pande zote.
Ni kushirikiana katika kubadilishana furaha na huzuni, kushiriki vyanzo vya furaha na sababu za faraja. Taswira hizi zimeelewa wazi na Qur’an pale Allah Mtukufu aliposema: “Na miongoni mwa ishara Zake ni kwamba amekuumbieni wake zenu kutoka nafsi zenu ili mpate kutulia kwao, na amejaalia baina yenu mapenzi na huruma. Hakika katika hayo zipo ishara kwa watu wanaotafakari.” (30: 21).
Uislamu umeipa ndoa uangalizi mkubwa na umakini wa hali ya juu, kwa kutambua kwamba uadilifu wa ndoa humaanisha uadilifu wa jamii ya Kiislamu. Ndiyo maana Qur’ani Tukufu imeeleza hukumu za ndoa na familia, na yanayohusiana nayo, katika aya mia moja arobaini na sita; jambo hili ni ushahidi wa umuhimu mkubwa wa suala hili.
Vilevile, Mtume wa Allah (Rehema na mani ziwe juu yake) ametoa muongozo unaoleta furaha na neema. Hata hivyo, uhusiano huu wa Kisharia na ahadi nzito (mithaq ghalidh) unaweza kukabiliwa na matatizo mengi ya Kindoa na kifamilia yanayokwamisha maendeleo.
Kwa kuzingatia hilo, ndio maana Mtume wa Allah amesema:“Anapokujieni yule mnayemridhia dini yake na tabia yake, basi muozesheni; msipofanya hivyo kutakuwa na fitna katika ardhi na uharibifu mkubwa.”(Tirmidhiy).Na kauli yake Mtume:“Mbora wenu ni yule aliye bora zaidi kwa watu wa nyumbani mwake, na mimi ni mbora wenu kwa watu wa nyumbani kwangu.” (Tirmidhiy).
Hakika hadithi hizi za Mtume wa Allah zimeweka msingi imara katika uhusiano wa kindoa, kuanzia katika uchaguzi wa mchumba na kuishia kwenye ridhaa na kukubaliana kunakodhihirishwa na wema na ubora wa tabia.
Kwa msingi huo, jambo muhimu na lalazima katika maisha ya kila mmoja wetu, na kwa lengo la kuzuia matatizo katika maisha ya ndoa, ni kuchunguza kwa makini na kwa ueledi mkubwa mchakato mzima wa kumpata mchumba.
Kuchagua mwenza wa maisha, kama hatua ya kwanza katika maandalizi ya ya ndoa, ni miongoni mwa maamuzi muhimu na hatarishi zaidi katika maisha ya mwanaume na mwanamke. Ni hatua yakuamuausalama wa ndoa, kudumu kwake, furaha yake, kuyumba kwake, kuvunjika kwake na taabu zake.
Familia ni nguzo ya jamii, na ndiyo kiini cha kwanza katika ujenzi wake. Kadiri familia inavyokuwa imeshikamana na yenye ushirikiano, ndivyo jamii inavyokuwa imara. Ushirikiano kati ya wanafamilia msingi wake ni upendo na heshima ya pande zote, na mapenzi haya hayapatikani ila kwa kuchagua mwenza wa maisha kwa umakini na kumcha Allah katika jambo hilo.
Iwapo kila mmoja wa wanandoa atamchagua mwenzake kwa uangalifu na akamcha Allah katika namna ya kuamiliana naye, basi Allah Mtukufu Atawaneemesha kwa upendo na maelewano.
Hata hivyo, kuwepo kwa mapenzi na maelewano hakumaanishi kutokuwepo kwa tofauti na migogoro ya kindoa, wala maisha yasiyokuwa na changamoto.
Hili ni jambo la kawaida katika maumbile ya mwanadamu, na hata Manabii na Mitume hawakusalimika na hali hiyo. Imepokelewa katika Sunna kwamba Mtume wa Allah aliwahi kujitenga na wake zake kwa muda wa mwezi mmoja, kisha akawapa hiari ya kurejea au kuachana.
Kwa sasa tunaishi katika mabadiliko makubwa yanayotokana na mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na kitamaduni. Zamani, jukumu la kuchagua mwenza wa maisha lilikuwa linafanywa zaidi na mama au wanawake kwa ujumla (wazazi), na kijana au msichana aliyekuwa anakusudia kuoa au kuolewa hakuwa na nafasi kubwa ya kushiriki katika uamuzi au kuchagua mwenyewe.
Lakini leo hali imebadilika; jukumu hili limekuwa likifanywa moja kwa moja na kijana na msichana mwenyewe, kwa juhudi zao binafsi, bila kushauriana na wazazi wao au kutafuta msaada wao, kwa matumaini ya kufikia maelewano mkubwa zaidi katika maisha yao ya ndoa.
Kuchagua mwenza wa maisha kwa wanaotarajia kuingia katika ndoa ndio msingi unaojengewa juu yake maisha yao ya ndoa yaliyo salama, thabiti na yasiyo na matatizo.
Kwa kuwa ndoa inasimama juu ya miunganiko miwili mikuu, ambayo ni muungano wa Kisharia na muungano wa Kiroho, basi muungano wa Kisharia na utekelezaji wa mkataba hauhitaji zaidi ya kutimia kwa masharti ya Kisharia yanayohitajika ili mkataba wa ndoa uwe sahihi. Hata hivyo, muungano huu pekee hauhakikishi maisha ya ndoa yaliyo na usawa na utulivu. Ama upendo unaozaliwa kutokana na mvuto na maelewano kati ya jinsia mbili, hujenga Muungano wa Kiroho wenye msingi imara unaosaidia kuendelea na kudumu kwa maisha ya ndoa kati ya mume na mke. Itaendelea toleo lijalo In Shaa Allah. 0712 690811
