Serikali ya Venezuela yawaachia huru wanasiasa wa upinzani, waandishi

Venezuela. Serikali ya Venezuela imewaachia huru viongozi mashuhuri wa upinzani waliokuwa wamefungwa, wanaharakati na waandishi wa habari raia wa ndani na wa kigeni katika kile ambacho serikali ilieleza kuwa ni ishara ya kutafuta amani.

Hatua hiyo imefanyika jana Alhamisi Januari 8, 2026 ikiwa ni takribani wiki moja tangu Rais Nicolás Maduro wa nchi hiyo akamatwe na majeshi ya Marekani na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za biashara ya dawa za kulevya.

Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye amekuwa akiweka shinikizo kwa washirika wa Maduro ambao sasa wanaongoza nchi hiyo wakubali maono yake kuhusu mustakabali wa taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta, alisema kuwa kuachiwa kwao kulifanyika kwa ombi la Marekani.

Katika mahojiano na Fox News Alhamisi usiku, Trump aliisifu serikali ya rais kaimu Delcy Rodríguez, akisema: “wamekuwa wazuri sana… Kila kitu tulichotaka, wametupatia.”

Jorge Rodríguez, ndugu wa rais kaimu na mwenyekiti wa Bunge la Taifa la Venezuela, amesema kuwa idadi kubwa ya watu ingeachiwa, lakini hadi usiku wa Alhamisi haikuwa wazi ni nani hasa au ni watu wangapi wangeachiwa.

Kwa muda mrefu, serikali ya Marekani na upinzani wa Venezuela wamekuwa wakitaka kuachiwa wanasiasa waliokamatwa, wakosoaji na wanachama wa asasi za kiraia. Hata hivyo Serikali ya Venezuela imesisitiza kuwa haishikilii wafungwa kwa sababu za kisiasa.

“Chukulieni hili kama ishara kutoka kwa serikali ya Venezuela, inayolenga kwa ujumla kutafuta amani,” ametangaza.

Kuachiwa kwa watu mashuhuri

Miongoni mwa walioachiwa ni Biagio Pilieri, kiongozi wa upinzani aliyekuwa sehemu ya kampeni ya urais ya 2024 ya mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, María Corina Machado.

 Pia ameachiwa Enrique Márquez, aliyewahi kuwa kiongozi wa mamlaka ya uchaguzi na mgombea katika uchaguzi wa urais wa 2024.

Video zilizowekwa mitandaoni na waandishi wa habari zinaonyesha Márquez na Pilieri wakikumbatiana na wapendwa wao mitaani nje ya gereza.

Pia wamo raia watano wa Uhispania  pamoja na wakili mashuhuri wa Venezuela na Uhispania na mwanaharakati wa haki za binadamu Rocío San Miguel.

Makundi ya haki za binadamu na wanasiasa wa upinzani wamesema wametiwa moyo na hatua hiyo, ingawa wanafikiri ni ishara ya kisiasa tu ya kuiridhisha serikali ya Trump, ambayo imeruhusu waaminifu wa Maduro kuendelea kubaki madarakani huku ikiiwekea nchi hiyo shinikizo kupitia vikwazo vikali.

Alfredo Romero, rais wa Foro Penal, ameonyesha matumaini akieleza kuwa huo ni mwanzo wa kweli wa kuvunjwa kwa mfumo wa ukandamizaji nchini Venezuela.

Awali, iliripotiwa kuwa baada ya Uchaguzi Mkuu nchini Venezuela wa mwaka 2024 serikali ya nchi hiyo iliendesha msako na kuwakamata watu mbalimbali zaidi ya 2,000 ikiwatuhumu kuwa walipanga kuhujumu utawala wa Maduro.