Geita Gold ugenini safi, nyumbani mmh!

GEITA Gold ni timu tishio msimu huu kwenye Ligi ya Championship ikiwa kileleni katika mbio za kupanda daraja, lakini licha ya makali yake hayo, uwanja wa nyumbani Nyankumbu umekuwa ukiwapa presha wachezaji na kujikuta wakiangusha alama sita mpaka sasa.

Timu hiyo haijapoteza mchezo wowote wa ligi, ikikamata nafasi ya kwanza kwenye msimamo baada ya michezo 13, imeshinda 10 na sare tatu, huku ikivuna alama 33.

Katika michezo 10 iliyoshinda, sita yote imeshinda ugenini sawa na kuvuna alama 18, huku nyumbani ikicheza mechi saba huku ikishinda nne na sare tatu.

Mechi ambazo Geita Gold haikushinda kwenye Uwanja wa Nyankumbu mjini Geita ni dhidi ya Kagera Sugar (1-1), Ken Gold (2-2), na Transit Camp (1-1), jambo linalotia wasiwasi kwamba huenda timu hiyo ikiwa nyumbani inakuwa na presha kubwa.

GEI 01

Kocha Mkuu wa Geita Gold, Zuberi Katwila alisikitishwa na matokeo hayo kwenye uwanja wa nyumbani kwani kupata sare kwao ni kama wamepoteza mchezo, huku akikiri kuwa ligi hiyo ni ngumu na timu nyingi zinajua kucheza na zina uzoefu wa Championship.

Amesema timu yao haina presha yoyote mbele ya mashabiki wao kwani wanajiandaa kila mchezo kulingana na namna walivyomsoma mpinzani na mbinu zake, hivyo, wakati mwingine matokeo yanayopatikana ni sehemu tu ya mchezo wa soka.

“Kwa hatua tuliyofikia huwezi kusema mechi inakuwa nyepesi ama namna gani, lakini sisi mechi tumezipa umuhimu sawa kuanzia mwanzo wa ligi kwa sababu malengo yetu ni kupanda Ligi na kufanya hivyo lazima ushinde mechi,” amesema Katwila.

Aliongeza kuwa; “Nawapongeza na kuwashukuru kwa yote wachezaji wangu, tuwe na uvumilivu safari bado inaendelea, zimebaki mechi mbili tunatakiwa tupate tena matokeo yatakayotuweka sehemu salama tumalize raundi ya kwanza tukiwa katika nafasi tunayoihitaji.”

GEI 02

Katwila amesema ushindi wa juzi ugenini dhidi ya Songea United umewaongezea imani baada ya sare ya 1-1 Nyankumbu dhidi ya Ken Gold, huku akisisitiza kuwa kila mechi wanaipa uzito na umuhimu kwa sababu wanatambua wanacheza na timu za namna gani.

“Sisi na wachezaji tuko tayari kwa kila mchezo, saikolojia wako sawa na utimamu umekamilika. Nawapongeza wachezaji wangu kwa kazi nzuri waliyoifanya, kwa maana ni mchezo mwingine wa ugenini baada ya sare tuliyoipata nyumbani na sare kwetu ni kama tumefungwa,” amesema Katwila.

Mshambuliaji wa timu hiyo, Maneno Kilaza amesema licha ya kupoteza alama sita kwenye uwanja wa nyumbani, msimu umekuwa mzuri kwao kutokana na mshikamano na ushirikiano walionao.

“Tunashukuru kwa matokeo tunayoendelea kupata maana haikuwa rahisi wapinzani wote ni washindani na wagumu. Mimi naamini mwalimu amekuwa akitupa mbinu sahihi ndiyo maana tunashinda mechi zetu.”