Dar es Salaam. Kama ambavyo rika hilo limeshika hatamu katika kila kona, Soko la hisa la Dar es Salaam (DSE) limeeleza kuwa vijana wenye miaka 20 mpaka 39 ndiyo kundi kubwa la wawekezaji wapya katika soko hilo kwa mwaka 2025.
Akitoa taarifa ya ufanisi wa DSE kwa mwaka 2025 Afisa Mtendaji Mkuu wa soko hilo, Peter Nalitolela amesema katika kipindi tajwa kulikuwa na mwamko mkubwa wa uwekezaji miongoni mwa vijana hata kama walifanya uwekezaji wenye thamani kiduchu.
Amesema katika kipindi cha mwaka husika, jumla ya akaunti mpya 123,547 za CDS zilifunguliwa na hivyo kufanya jumla ya akaunti za kipekee za CDS kufikia 740,639 hadi mwisho wa mwaka 2025.
“Ikilinganishwa na mwaka 2024, idadi ya akaunti mpya za CDS zilizofunguliwa imeongezeka kwa asilimia 316.28, ambapo mwaka 2024 ni akaunti mpya 29,679 pekee ndizo zilizofunguliwa. Sehemu kubwa ya akaunti mpya zilizofunguliwa ni za wawekezaji wenye umri wa miaka 21 hadi 30, wanaochangia asilimia 40.33 ya akaunti zote mpya,” amesema.
Kwa upande wa akaunti zilizofunguliwa kupitia jukwaa la kidijitali (MTP), jumla ya akaunti mpya 94,805 ziliongezeka mwaka 2025, na kufanya jumla ya akaunti za MTP kufikia 139,971 hadi mwisho wa mwaka huo. Hii ina maana kwamba idadi ya akaunti za MTP iliongezeka zaidi ya mara tatu, sawa na ongezeko la asilimia 309.90, ikilinganishwa na akaunti 45,166 zilizokuwapo mwishoni mwa mwaka 2024.
Ikilinganishwa na mwaka 2024, idadi ya akaunti zilizosajiliwa kwenye MTP mwaka 2025 iliongezeka kwa asilimia 248.41, ambapo mwaka 2024 ni akaunti 27,211 pekee ndizo zilizosajiliwa.
Jumla ya akaunti za MTP zilizokuwapo hadi mwisho wa mwaka 2025, ambazo ni 139,971, zinawakilisha asilimia 18.89 ya jumla ya akaunti zote za kipekee za CDS 740,639. Hii ni hatua kubwa ikilinganishwa na mwisho wa mwaka 2024, ambapo akaunti za MTP zilikuwa asilimia 7.32 tu ya akaunti zote za CDS.
“Kati ya wawekezaji waliosajiliwa kwenye MTP mwaka 2025, kundi kubwa zaidi ni la wenye umri wa miaka 20 hadi 29, likiwa na akaunti 41,574 sawa na asilimia 43.85, likifuatiwa na wenye umri wa miaka 30 hadi 39 ambao wana akaunti 31,617 sawa na asilimia 33.35,” amesema Nalitolela.
Amesema mafanikio hayo yanatokana na juhudi zinazoendelea za uhamasishaji na uelimishaji wa umma, sambamba na ubunifu endelevu, maboresho ya mifumo na uwekezaji unaofanywa kwenye jukwaa hilo, kupitia programu za simu za mkononi pamoja na mfumo wa kompyuta (desktop).
“Takwimu hizi hazimaanishi kuwa wazee kama mimi wanatengwa na soko, hapana jukwaa hili ni rafiki kwa watu wote, ni rahisi kulifikia ukiwa popote hata malipo yanafanyika kwa njia rahisi,” ameongeza Nalitolela.
Kwa mgawanyo wa kijinsia, Nalitolela amesema wawekezaji wanawake waliounganishwa kwenye MTP mwaka 2025 wanachangia asilimia 33, huku wanaume wakichangia asilimia 67.
Kwa upande wa kijiografia, Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa idadi ya akaunti zilizosajiliwa, ukiwa na akaunti 36,636 sawa na asilimia 38.64, ukifuatiwa na Mkoa wa Arusha wenye akaunti 6,278 sawa na asilimia 6.62.
Kuhusu malalamiko ya wawekezaji ambao wamekuwa hawapati gawio lao kwa wakati Mkuu wa usajili na hisa wa kampuni Tanzu ya DSE (CSDR) Gideon Kapange amesema mara nyingi husababishwa na kutokuwepo kwa taarifa zao sahihi za kibenki au matatizo ya kimtandao.
“Sio kazi ya kapuni zilizoorodheshwa kusambaza gawio wao wanalitangaza, ni jukumu la wasambazaji kama sisi kugawa, kumekuwa na changamoto wakati mwingine lakini nia ya kila msambazaji ni kuhakikisha gawio limelipwa mapema na haraka,” amesema Kapange.
