Kaya 400 zaathiriwa na mafuriko Momba, wananchi wakimbia makazi

Songwe. Wananchi wa Kijiji cha Ntinga, wilayani Momba mkoani Songwe, wamelazimika kuyakimbia makazi yao na kutafuta hifadhi katika Shule ya Msingi Msangano kutokana na mafuriko.

Mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia Januari 8, 2026 katika wilaya za Ileje, Mbozi na Tunduma, zimesababisha maji kuvamia makazi ya watu.

Mafuriko hayo yamesababisha zaidi ya nyumba 400 katika Kata ya Msangano kilipo kijiji hicho kuzingirwa na maji baada ya Mto Nkana kufurika.

Vilevile, baadhi ya mazao yamesombwa na mafuriko.

Prisca Msukwa, mkazi wa kijiji hicho amesema pamoja na kukosa makazi mashamba yao yamesombwa na maji na kuharibu mazao.

Amesema mashamba hayo ni ya mahindi, maharage, ufuta na mazao mengine.

Diwani wa Msangano, Musa Siame amesema mafuriko yalianza saa tisa usiku wa kuamkia Januari 8, 2026 na kuzingira makazi ya wananchi hali iliyozua taharuki.

Amesema hadi kufikia saa moja usiku wa Januari 8, 2026 hapakuwa na madhara ya vifo yaliyoripotiwa, jambo ambalo ni la Faraja.

Siame amesema wananchi wamepata hasara kubwa kwani baadhi ya mifugo imesombwa na maji, pamoja na mbolea waliyokuwa wamehifadhi kwa ajili ya matumizi ya kilimo.

Amesema vyakula na vitu vingine vya thamani vilivyokuwa majumbani vimeharibiwa na baadhi kusombwa na mafuriko.

“Katika hatua za dharura, kaya zote zilizoathirika na kuzungukwa na mafuriko zimehamishiwa kwa muda katika Shule ya Sekondari Msangano ili kuhakikisha usalama wao, huku wakisubiri hali kurejea katika hali ya kawaida,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Momba, Elius Mwandobo, aliyefika eneo hilo jana Januari 8, ametoa maagizo kwa baadhi ya taasisi ikiwamo Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) Wilaya ya Momba kupima maji yanayotiririka kwenye makazi ya watu ili kuona kama yana usalama.

“Ruwasa mfike hapa Msangano mpime haya maji muone kama yanafaa kwa matumizi kwani yanatiririka kutoka kwenye vyoo vya wananchi ambavyo vimepasuka kutokaka na mafuriko ili kuzuia magonjwa ya mlipuko,” amesema.

Mwandobo amesema tayari kamati ya maafa ya halmashauri imefika kufanya tathmini na itakapokamilisha wataona ni msaada wa aina gani unahitajika kwa walioathirika.

Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, ilitoa tahadhari kwa wavuvi na wananchi waishio mabondeni katika kipindi cha msimu wa mvua za wastani na chini ya wastani.

Miongoni mwa tahadhari ni pamoja na uwepo wa mafuriko au makazi kuzingirwa maji kufuatia udongo kushiba kwenye maeneo yenye mikondo ya mifereji ya kutiririsha maji.

Meneja wa TMA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Elius Lipiki akizungumza na Mwananchi jana Alhamisi Januari 8, 2026 alisema:

“Tunatoa tahadhari kwa wavuvi kufuatilia taarifa ya mamlaka husika kutokana na kuwepo kwa hatari ya kupata uoni hafifu, vyombo kupoteza mwelekeo au kupinduka.”

Lipiki alisema kwa sasa kuna mvua za wastani na chini ya wastani ambazo zimesababisha udongo kushiba maji. Pia alizungumzia vipindi vya mvua zinazoweza kuleta madhara kutokana na kasi maji kwenye maeneo yenye mitiririko hususani mito na vijito.

“Utabiri unaonyesha mwisho mwa wiki hii kutakuwa na ongezeko la mvua za wastani ambazo zinaweza kuleta madhara, hivyo tunatoa wito kwa wananchi waishio mabondeni na pembezoni mwa mikondo ya maji na mifereji kuchukua tahadhari na kufuatia taarifa ya TMA,” alisema.