Duchu, Jusa na rekodi Mapinduzi

WAKATI tukisubiri kushuhudia fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026 ipigwe Januari 13, 2026 pale Gombani kisiwani Pemba baada ya jana usiku kuchezwa nusu fainali ya pili kati ya Yanga na Singida Black Stars, kuna nyota wawili wameacha rekodi.

Nyota hao ni David Kameta ‘Duchu’ na Yussuf Suleiman Haji ‘Jusa’ anayekipiga kwa mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Mlandege ambao wamevuliwa ubingwa mapema tu.

Duchu na Jusa kila mmoja ameweka rekodi yake katika Kombe la Mapinduzi 2026 wakati ambao Mlandege ikiishia hatua ya makundi kwa kupoteza mechi zote tatu, huku Simba ikiondoshwa nusu fainali ikifungwa 1-0 na Azam.

Alianza Jusa kuweka rekodi ya kukosa mkwaju wa penalti, pigo pekee ambalo kabla ya nusu fainali ya pili iliyochezwa jana, ndilo limepatika katika mechi 13 zilizopigwa kuanzia makundi hadi nusu fainali.

DU 02

Duchu nyekundu, Jusa kukosa penalti pekee iliyopatikana.

Jusa alikosa mkwaju huo wa penalti uliopanguliwa na kipa wa Singida Black Stars, Metacha Mnata wakati Mlandege ikilala kwa mabao 3-1 katika mechi ya ufunguzi wa michuano hiyo iliyochezwa Desemba 28, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja.

Kwa upande wa Duchu, ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza katika michuano hiyo kuonyeshwa kadi nyekundu ambapo tukio hilo lilitokea hatua ya nusu fainali, Simba ikifungwa 1-0 na Azam, Januari 8, 2026.

DU 01

Duchu kwanza alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 58 kwa kumuangusha Cheikna Diakite, kisha dakika ya 90+2 akaonyeshwa kadi ya pili ya njano iliyoambatana na nyekundu kwa kosa la kusukumana na mwamuzi Mohamed Simba akipinga uamuzi wake.