Arusha. Serikali imetangaza kipindi cha nyongeza cha miezi mitatu kwa taasisi za umma na binafsi zinazokusanya, kuchakata au kuhifadhi taarifa binafsi ambazo bado hazijakamilisha usajili wa hiari, hatua inayolenga kutoa fursa ya mwisho kwa taasisi hizo kutimiza matakwa ya kisheria.
Aidha, Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), imeelekezwa kuanza maandalizi ya utekelezaji wa ukaguzi wa uzingatiaji wa sheria, taasisi, kampuni au watu binafsi watakaobainika kukusanya, kuchakata au kuhifadhi taarifa binafsi bila kujisajili baada ya kumalizika kwa kipindi hicho cha nyongeza, watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Maagizo hayo yametolewa leo Ijumaa Januari 9, 2026 na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, alipokuwa akizungumza wakati wa kufunga mafunzo maalum kwa maofisa ulinzi wa taarifa binafsi yaliyoratibiwa na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC).
Waziri Kairuki amesema kipindi hicho cha nyongeza inaanza leo na kitamalizika Aprili 8, 2026, akisisitiza kuwa baada ya muda huo kuisha, hakuna taasisi, kampuni wala mtu binafsi atakayevumiliwa kukiuka Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi pamoja na kanuni zake.
Waziri Kairuki amesema Aprili 3, 2024 Rais Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo ya usajili wa taasisi zote zinazohusika na ukusanyaji, uchakataji au uhifadhi wa taarifa binafsi na kuweka ukomo Desemba 31, 202, kwa taasisi hizo kuanza utekelezaji kwa kujisajili na kuwateua maofisa wa ulinzi wa taarifa binafsi.
Amesema kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika utekelezaji wa maelekezo hayo, Serikali imeongeza muda wa usajili hadi Aprili 30, 2025, kabla ya sasa kutoa nyongeza ya mwisho ya miezi mitatu kwa taasisi ambazo bado hazijakamilisha taratibu za usajili.
“Serikali inatoa nyongeza ya mwisho ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia sasa hadi Aprili 8, 2026. Baada ya hapo, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya taasisi zitakazobainika kutokamilisha usajili wao wa hiari,” amesema Waziri Kairuki.
Aidha, ameiagiza Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), kuanza mara moja maandalizi na utekelezaji wa ukaguzi wa uzingatiaji wa Sheria, akisisitiza kuwa taasisi, kampuni au watu binafsi watakaobainika kuendelea kukusanya, kuchakata au kuhifadhi taarifa binafsi bila kujisajili, watachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria.
Amesema msimamo huo wa Serikali unalenga kulinda haki za wananchi, akibainisha kuwa taarifa binafsi ni nyenzo muhimu katika kipindi hiki cha uchumi wa kidijitali na Serikali imelenga kujenga uchumi unaoaminika na ulio salama.
Waziri huyo amesisitiza kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kujengwa juu ya matumizi mabaya ya taarifa binafsi au mifumo isiyo salama, hivyo maofisa ulinzi wa taarifa binafsi wana wajibu wa kuwa viongozi wa mabadiliko, washauri kwa menejimenti zao na wasimamizi wa utekelezaji wa Sheria ndani ya taasisi zao.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Dk Emmanuel Mkilia alisema mafunzo hayo ya siku mbili yalilenga kuandaa rasilimali watu wenye uwezo wa kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi katika taasisi za umma na binafsi.
Dk Mkilia amesema mafunzo hayo yatahakikisha ukusanyaji, uchakataji, uhifadhi na matumizi ya taarifa binafsi vinafanyika kwa kuzingatia kikamilifu matakwa ya kisheria na kanuni, ili kulinda faragha za watu.
Amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kujenga uchumi wa kidijitali unaoaminika, ulio salama na unaozingatia misingi ya haki na utawala wa sheria.
“Kupitia mafunzo haya, Tume inatarajia kuona mabadiliko ya wazi katika utekelezaji wa Sheria kwa taasisi za umma na binafsi, pamoja na kuimarisha ulinzi wa taarifa binafsi. Pia tutaendelea kutoa elimu na uhamasishaji nchi nzima ili kuhakikisha utekelezaji wa Sheria unazingatiwa na kulinda maslahi ya wananchi na Taifa,” amesema.
Dk Mkilia amesema mafunzo hayo yamehusisha maofisa 178, wakiwamo 38 kutoka kampuni za utalii, huku wengine wakitoka katika taasisi za umma na sekta binafsi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PDPC, Balozi Adadi Rajabu amesema mafunzo hayo yataendelea kufanyika mara kwa mara kwa maofisa wa ulinzi wa taarifa binafsi, akibainisha umuhimu wake hususan kwa sekta ya utalii.
Amesema sekta ya utalii ni miongoni mwa sekta muhimu zinazochangia kwa kiwango kikubwa pato la Taifa, hivyo kuwajengea uwezo maofisa wake katika ulinzi wa taarifa binafsi ni hatua muhimu katika kuimarisha uaminifu na usalama wa taarifa.
